1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kumchagua rais mpya Pakistan

Hamidou, Oumilkher19 Agosti 2008

Macho ya walimwengu yakodolewa Pakistan baada ya Musharraf kujiuzulu

https://p.dw.com/p/F0kz
Viongozi wa vyama vinavyounda serikali ya muungano nchini Pakistan:Nawaz Sharrif (kushoto wa chama cha PMLN na Asif Zardai wa chama cha PPPPicha: picture-alliance/ dpa



Watu wasiopungua 23 wameuwawa bomu liliporipuka hospitali,kaskazini magharibi ya Pakistan.Balaa hili limezuka katika wakati ambapo viongozi wa vyama vya kisiasa nchini Pakistan wanatazamiwa kukutana kumteuwa rais wa muda baada ya Pervez Musharraf kujiuzulu hapo jana.


Shambulio hilo la bomu ambalo chanzo chake bado hakijulikani,limetokea mjini Dera Ismael Khan,karibu na maeneo ya kikabila ambako jeshi la Pakistan linawaandama wafuasi wa itikadi kali wanaoshirikiana na Al Qaida na wataliban na ambako mashambulio yameshika kasi tangu mwaka mmoja uliopita.



Katika mkoa wa Bajour,unaopakana na Afghanistan,vikosi vya usalama vya Pakistan vimejibisha mashambulio ya waasi na kuwauwa wanamgambo 20.


Mkuu wa vikosi vya wanajeshi wa Pakistan,jenerali Ashfaq Kayani amewasili Kaboul hii leo kwa mazungumzo ya ghafla pamoja na maafisa wa kijeshi wa Afghanistan na wakuu wa vikosi vya kimataifa nchini humo.Ziara hiyo imetokea pakiweko mvutano mkubwa kati ya nchi hizi mbili jirani huku Washington ikizilaumu hadharani idara za upelelezi za Pakistan kuwaunga mkono wataliban.


Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Afghanistan,SULTAN AHMAD BAHIN anasema:


"Tunataraji kujiuzulu Musharaff kutaipa nguvu serikali ya kiraia.Tunataraji Pakistan itakua nchi tulivu,inayofuata demokrasia na kuheshimu sheria.Tunataraji pia mapambano dhidi ya ugaidi yataimarishwa na Pakistan kuwajibika zaidi katika kushirikiana na jumuia ya kimataifa na serikali ya Afghanistan kupambana na magaidi."


Mashambulio yameshika kasi katika wakati ambapo vyombo vya habari vya Pakistan vinawahimiza viongozi wa nchi hiyo waidhihirishie jamii na ulimwengu kwa jumla "wamemaizi,wana busara na wanaweza kuiongoza nchi yao katika njia ya maendeleo."



Viongozi wa serikali ya muungano wanatazamiwa kukutana baadae hii leo kuzungumzia nani anastahiki kukabidhiwa wadhifa wa rais aliyejiuzulu na pengine pia kuzungumzia jinsi ya kulishughulikia suala la kuwarejeshea nyadhifa zao majaji walioachishwa kazi..


Spika wa baraza la Senet Muhammedmian Somro amekabidhiwa kwa muda wadhifa wa rais tangu jana,hadi rais mpya atakapoteuliwa na bunge na mabaraza manne ya kimkoa ya nchi hiyo,siku 30 kutoka sasa.


Majina yameshaanza kutajwa ikiwa ni pamoja na Mehmud Khan Achakzai wa kutoka mkoa wa Baluchistan,Aftab Shoban Mirani wa mkoa wa Sid au spika wa bunge la taifa bibi Fehmida Mirza.


Wakati huo huo huo waziri wa sheria wa Pakistan,Farook Naek amewaambia maripota hii leo viongozi wa serikali watabidi waamue kama Musharraf aandamwe kisheria.Chama cha pili kwa ukubwa katika serikali ya muungano,kinachoongozwa na waziri mkuu wa zamani Nawaz Sharrif kimeshasema kinataka kumuona Musharraf anafikishwa mahakamani kwa makosa ya uhaini.