Jopo la majaji katika kesi ya Ghailani lahitilafiana
16 Novemba 2010Jaji mmoja katika kesi ya kwanza ya kiraia dhidi ya mfungwa wa zamani wa Guantanamo, Ahmed Khalfan Ghailani. ameomba atolewe katika jopo la majaji, hatua inayoangaliwa kama mtihani mkubwa kwa upande wa mashtaka.
Katika risala aliyomtumia Jaji Lewis Kaplan, jaji huyo wa kike, anaejulikana kama jaji nambari 12, amesema uamuzi wake hauambatani na ule wa wenzake 11 wa jopo la majaji na kwamba anahisi "anahujumiwa. "Si wazi, lakini kama hoja zake zinamtia hatiani au zinataka aachiwe mtuhumiwe huyo.
Jaji Kaplan hajazungumza na jaji huyo, na amesema, hata hivyo, ni mapema mno kuingilia kati wakati majaji wanashauriana. Jopo la majaji linaendelea na mashauriano, na jaji Kaplan amekatalia mbali mwito wa wawakilishi wa mshatikiwa kutaka kesi ibatilishwe.
Kesi ya mwezi mzima ya Ghailani katika korti ya Manhattan imekuwa ikiangaliwa kama kipimo kwa mtazamo wa rais Barack Obama wa jinsi ya kuandamwa kisheria watuhumiwa 174 ambao bado wanashikiliwa katika kambi ya kijeshi ya Guantanamo, nchini Cuba-ikiwa ni pamoja na Khalid Sheikh Mohammed anaetuhumiwa kuwa muasisi wa mashambulio ya kigaidi ya september 11 mwaka 2001.
Ahmed Khalfan Ghailani, mwenye umri wa miaka 36, Mtanzania anaetokea Zanzibar,anatuhumiwa kuhusika na njama ya mashambulio ya mabomu ya Al Qaida mwaka 1998 dhidi ya ofisi za ubalozi wa Marekani nchini Kenya na Tanzania-mashambulio yaliyogharimu maisha ya watu 224.
"Nimeshafikia uamuzi na hauambatani na uamuzi wa majaji waliosalia", ameandika jaji huyo wa kike katika risala inayosemekana imejaa makosa ya sarufi. Amesema uamuzi wake hautobadilika, ndio maana anataka atolewe au nafasi yake apewe jaji mwengine.
Ingawa uamuzi unabidi uungwe mkono na wote, hata hivyo, jaji Kaplan amemtaka jaji huyo wa kike aendelee kushauriana na wenzake, akisema tunanukuu:"sio lazima ubadilishe uamuzi wako, kwasababu ya maoni ya majaji wengine." Mwisho wa kumnukuu jaji Lewis Kaplan.
Mwandishi: Ummil Hamidou/Reuters
Mpitiaji: Miraji Othman