Jivu la zu Guttenberg lakataa kupeperuka na hewa | Magazetini | DW | 10.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Jivu la zu Guttenberg lakataa kupeperuka na hewa

Pamoja na mengine, tahriri za leo (10.03.2011) zinazungumzia masuala ya uwezekano wa vikwazo vya anga dhidi ya Libya na kujiimarisha kwa Waziri mpya wa Ulinzi wa Ujerumani kwa wanajeshi vijana.

Karl-Theodor zu Guttenberg akisalimiana na wanajeshi

Karl-Theodor zu Guttenberg akisalimiana na wanajeshi

Mhariri wa Rheinische Post anasema kuwa, wakati leo mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wakikutana mjini Brussels, mada kuu itakuwa ni kuifunga mirija yote ya kifedha ya Libya iliyopo barani Ulaya.

Inajuilikana kuwa hata baada ya vikwazo kutangazwa, bado utawala wa Libya ungali ukiendelea kufaidika kifedha, kupitia biashara inayofanyika baina ya pande hizi mbili.

Kuhusu uwezekano wa kupitisha na kusimamia azimio la kuzuia ndege kuruka kwenye anga la Libya, Rheinische Post linamnukuu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Werner Hoyer, akisema kuwa, jambo hilo linaingia akilini sana, lakini utekelezaji wake ni lazima uwe na sura ya kimataifa.

Na kwa kuanzia, ni majirani wa Libya na Umoja wa Nchi za Kiarabu, ambao wanatakiwa kuongoza njia.

Kwa upande wake, mhariri wa Mittelbayerische Zeitung anataka sasa Wajerumani waache kuzungumzia masuala ya kashfa dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Karl-Theodor zu Guttenberg, na sasa wajielekeze kwenye masuala mengine muhimu yanayoathiri siasa zao za kila siku.

Jua na msimu wa mapukutiko limeanza kung'ara, ndivyo anavyosema mhariri huyo.

Na sasa, jivu la maiti ya kisiasa ya zu Guttenberg, nalo lapaswa kupeperuka na zama nyengine ianze. Mhariri anasisitiza kuwa kilichommaliza zu Guttenberg si kitu kimoja tu kama inavyotaka kuaminika.

Sio vile tu kutumia kwake maandishi ya wengine, kwenye tasnifu ya shahada yake ya uzamifu, bila ya kuwataja, bali pia ni misuguano ya siasa za kihafidhina ndani na nje ya chama chake cha CSU.

Mhariri anataka mjadala uelekezwe huko sasa, kabla wengine hawajamalizana, kwa staili na njia nyengine, ukiacha hii ya Googleberg, kama walivyoiita watani wa zu Guttenberg.

Hata hivyo, wakati mhariri wa Mittelbayerische Zeitung akitaka jivu la zu Guttenberg lipeperuke na upepo, mtu aliyechukuwa wadhifa wa mwanasiasa huyo kijana katika wizara ya Ulinzi, ni mwanasiasa wa makamo kidogo, Thomas de Maiziere.

Kati yao pana tafauti ya miaka 18. Na hili, ndilo linalomfanya mhariri wa Flensburger Tageblatt amuone de Maiziere kuwa na kibarua kigumu na kwamba jivu la zu Guttenberg bado limeganda, halipeperuki na hewa.

Karl-Theodor zu Guttenberg amemuachia mfuatizi wake, Thomas de Maiziere, mtihani mgumu, ndivyo asemavyo mhariri. Kujijengea imani ya wanajeshi vijana kwenye jeshi la Ujerumani, hapana shaka, litakuwa jaribio la kwanza la kupima ufanisi wa de Maiziere kwenye ofisi hii mpya.

Maana ukiacha tafauti ya umri baina yao, pana suala zima la haiba. Si jambo la kutia chumvi kwamba zu Guttenberg alikuwa ni mwanasiasa mwenye mvuto kwenye kundi la vijana, na jeshi linao wengi watu wa rika hilo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza