Karl-Theodor zu Guttenberg - aibu kubwa kwa siasa za Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Karl-Theodor zu Guttenberg - aibu kubwa kwa siasa za Ujerumani

Baada ya wiki mbili za msukosuko na mjadala mkali juu ya tasnifu yake ya shahada ya uzamifu, waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg, amejiuzulu, kuepusha athari kwa ofisi, wanajeshi na chama chake

default

Aliyekuwa waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg

Hatimaye! Waziri wa ulinzi Karl-Theodor zu Guttenberg amekubali athari za kashfa ya tasnifu yake ya shahada ya uzamifu na amejiuzulu. Baada ya wiki mbili za mijadala iliyoendelea kuongezeka kuhusu tabia yake, uaminifu wake na kufaa kwake kushikilia wadhifu huu muhimu, hatimaye ameumaliza mchezo huu usio heshima.

Ni mfululizo wa ripoti za vyombo vya habari za siku zilizopita, zilizomuangusha, ni maandamano ya wanasayansi yaliyomuonyesha kama muongo, na hatimaye ukosoaji wa kila mara uliozidi kuongezeka ambao haukumpa nafasi nyengine ya kupumua. Waziri wa ulinzi ambaye anatukanwa waziwazi kama mtu muongo na tapeli, kwa shirikisho la Ujerumani ni jambo lisilovumilika. Mwanasiasa mashuhuri ambaye anapingana na tabaka zima la wanasayansi hakubaliki kwa nchi ambayo wajumbe wake wanapenda kuiita nchi ya elimu. Ukweli ni kwamba kujiuzulu kwake kumechelewa.

Zu Guttenberg tayari angejiuzulu wiki mbili zilizopita pale ilipobainika wazi kwamba alitumia maandishi ya watu wengine katika tasnifu yake bila kuwataja majina na kupata cheo cha heshima kwa kutumia ujanja. Kama kwa haraka angeamua kuchukua hatua hii, kama wengi walivyotarajia kutoka kwake, basi angeepusha athari kwa utamaduni wa kisiasa wa Ujerumani na kwa njia hiyo kuepusha athari kwa nchi nzima, kama alivyoahidi wakati wa kula kiapo cha kushika wadhifa wake wa uwaziri. Kama angeonyesha kujutia makosa yake kwa dhati na aibu, njia ya kurejea uongozini kwa hakika haingekuwa imefungwa. Lakini sasa hakuna uwezekano wa kurejea tena.

Shujaa wa siasa za Ujerumani, aliyefaulu kuwavutia watu na hata kuwatia moyo na msukumo vijana wapende siasa, amejimaliza mwenyewe! Kwa ukaidi usio mfano na kujiwekea kipimo cha juu, amejiandalia mazingira ya kuanguka kwake. Alijichimbia kaburi lake mwenyewe! Ameruhusu kwamba kila siku mambo yanayofichuka yaharibu utu wake na ofisi yake, na kwa uwazi uwezo wake wa kiakili kutiliwa shaka. Alilazimika kushuhudia jinsi wasifu wake mzuri kikazi ulivyoharibiwa, vituo vingapi katika maisha yake ya kazi vilivyomuona kama mtu muongo, hadi hatima ya mwanasiasa kijana mwenye kipaji, mtu aliyepigiwa upatu kuchukua uongozi wa chama chake, lakini sasa amebaki hana kitu.

Bila shaka sio zu Guttenberg pekee atakayeathiriwa na kashfa hii. Hata kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambaye alimtaka waziri huyo aendelea kushikilia wadhifa wake, sasa naye pia amepata pigo. Kupitia mbinu zake ambazo ziligonga mwamba ameyakanyaga mambo muhimu sana kama vile uaminifu na kusadikika.

Na hata makundi yaliyomo serikalini na yaliyomuunga mkono waziri huyo kwa utiifu na bidii ya kuchukiza, kana kwamba kuanguka kwake tayari hakungeweza kuzuiliwa, wamejifanya kuwa kichekesho.

Zilikuwa wiki mbili ngumu na za aibu kwa siasa za Ujerumani. Kwa bahati mbaya Karl-Theodor zu Guttenberg hakuwa na maneno ya kujikosoa na kuhuzunika wakati wa kujiuzulu kwake. Kwa hiyo hakuna haja ya kumpa heshima kwa hatua aliyochukua. Kwa bahati mbaya yeye amesababisha maudhi na aibu kubwa kwa siasa za Ujerumani kuwahi kutokea katika muongo mmoja uliopita.

Mwandishi: Marx, Bettina (DW Berlin)/ZPR/Josephat Charo

Mhariri: Aboubakar Liongo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com