1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Je, Ukraine inafanya maandalizi ya kulipiza kisasi?

20 Agosti 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ametishia kulipiza kisasi dhidi ya Urusi. Je, mashambulizi ya hivi karibuni ya miundo mbinu ya reli, vituo vya kijeshi na vifaa vya mawasiliano vya Urusi, ni maandalizi?

https://p.dw.com/p/4Folx
Ukraine Waffensystem Carl Gustaf M4
Picha: Andrew Marienko/AP Photo/picture alliance

Ben Hodges, ambaye ni jenerali mkuu wa zamani katika jeshi la Marekani na kamanda mkuu katika jeshi la Marekani barani Ulaya, aliiambia DW kuwa kuna ishara kwamba jeshi la Urusi linadhoofika, kufuatia milipuko iliyotokea katika uwanja wa ndege za kijeshi wa Urusi katika rasi ya Crimea na mashambulizi ya Ukraine katika hifadhi ya silaha za Urusi katika maeneo inayoyakalia.

"Hii inaonyesha kwamba hawana nguvu," alisema Hodges. "Inaonyesha pia kwamba mfumo wao wa kupanga mikakati umekwisha. Warusi hawana hata watu wa kutosha au uwezo wa kulinda mikakati yao ya operesheni."

Hodges alilinganisha hali hiyo na miezi kadhaa ya mapigano kati ya Ujerumani iliyokuwa chini ya Wanazi na Jeshi Jekundu la Sovieti kusini mwa Ukraine 1943 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.

Mfumo duni wa kupanga mikakati

Hali ya kijiografia nchini Ukraine iliwapelekea wanajeshi wa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia, kupata matatizo sawa sawa na yale wanayoyapata wanajeshi wa Urusi katika suala la kulinda vifaa wanavyowasilishiwa. Hodges anasema Urusi kwa sasa haina nguvu kabisa.

Ukraine-Krieg | Explosion eines Munitionsdepots auf der Krim
Moshi ukifuka katika kituo cha kuhifadhi silaha za Urusi CrimeaPicha: Sergei Malgavko/TASS/dpa/picture alliance

Anasema kila hifadhi ya silaha au kituo cha kijeshi kinaposhambuliwa, jeshi la Urusi linalazimika kurudisha nyuma zaidi vituo vyake vya kuwasilisha silaha jambo linalofanya ukarabati na uwasilishwaji wa silaha kuwa kibarua kizito.

"Hawawezi kupata vitu vipya," Hodges alisema. "Kuna vitu vingi sana vinavyohitaji mafuta na uerekebishaji kama tu gari lolote la ujenzi. Sehemu hizo lazima zitoke mahali. Huu wote ni mzigo kwa mfumo duni wa kupanga mikakati."

Kwa miezi sasa, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amekuwa akitangaza mashambulizi ya kulipiza kisasi kusini mwa Ukraine. 

Je, mashambulizi ya hivi karibuni ya miundo mbinu ya reli, vituo vya kijeshi na vifaa vya mawasiliano katika maeneo yanayodhibitiwa na Urusi, maandalizi hayo ya kulipiza kisasi? Katikati ya mwezi Agosti, Meya wa Kyiv Vitaly Klitschko aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter: "Usiwe sehemu anakokusubiri adui wako. Kuwa sehemu ambayo adui wako hakusubiri. Kuwa mtu mwenye kusogea sogea."

Uwasilishwaji wa silaha za Ujerumani

Ukraine inaweka mazingira ya kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi, alisema Nico Lange, mtaalamu wa usalama na mshauri kwa aliyekuwa waziri wa ulinzi Annegret Kramp-Karrenbauer katika serikali iliyopita ya Ujerumani, chini ya Kansela Angela Merkelwa chama cha Kihafidhina cha Christian Democratic Union CDU.

Infografik Ukraine Politik EN
Sera ya Ujerumani kwa Ukraine

Ila Ukraine haina "magari ya kivita ya kutosha yatakayoipelekea kufanya mashambulizi na kuchukua tena udhibiti wa maeneo kwa kufanya mashambulizi kutokana na upana wa ardhi ya Ukraine.," alisema Lange.

Lange hasa anakosoa hatua ya Ujerumani kutoipelekea Ukraine silaha nzito.

"Katika miezi ya hivi majuzi hapa Ujerumani, ilikuwa ikisemekana kwamba waukraine hawatoweza kujifunza kwa haraka kuitumia vyema mifumo ya silaha ya nchi za Magharibi." alisema Lange. "Lakini kwa kutumia mfumo wa HIMARS wa Marekani, wamethibitisha kwamba wanaweza kujifunza kuitumia kwa haraka sana. Sasa wanahitaji magari zaidi ya kijeshi."

Hakuna kitisho cha nyuklia

Hodges anawaunga mkono maafisa wa kijeshi, wanasiasa na wachambuzi wanaotoa wito wa Marekani na marafiki zake kuipa Ukraine mifumo ya silaha za kisasa kama ule wa wa masafa mafupi wa kurusha makombora wa ATACMS ambao unawez kurusha kombora hadi kilomita 300. Kombora hili pia linaweza kurushwa na mfumo wa Marekani wa HIMARS, ambao Ukraine iliutumia kupata ufanisi wake mkubwa wa hivi karibuni dhidi ya Urusi.

Ukraine I Zaporizhzhia I Saporischschja
Kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia nchini UkrainePicha: Dmytro Smolyenko/Ukrinform/IMAGO

Mshauri wa kitaifa wa usalama katika ikulu ya White House Jake Sullivan hataki kuwasilisha mifumo kama hiyo kwa Ukraine, akihofia kuenea kwa vita hivyo.

Lakini Hodges anasema, njia ya pekee inayoweza kuipelekea Urusi kupanua vita hivyo ni matumizi ya silaha ya nyuklia, na anasema hilo haliwezekani. Anasema hakuna maeneo ya Ukraine ambayo Urusi inayalenga yatakayowanufaisha katika vita hivyo. Hata kutumika kwa silaha ya nyuklia ambayo haina uharibifu mkubwa nchini Ukraine, ni jambo litakaloipelekea Marekani na Uingereza kuingilia vita hivyo.

Hodges alisema, "siamini kama Putin ni kichaa," alisema. "Ni mtu mbaya ila si kichaa wala haezi kujiua."

Ana matumaini kwamba endapo Marafiki wa Ukraine wataendelea kuwaunga mkono, majeshi ya Urusi yanaweza kusukumwa nyuma zaidi ifikiapo mwishoni mwa mwaka 2022, hadi wafikie kule walikokuwa kabla walipoanza uvamizi huo mnamo februari 24.

Chanzo: https://www.dw.com/en/ukraine-appears-to-prepare-counteroffensive-against-russia/a-62870896