1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miili ya Wapalestina 15 yarejeshwa Ukanda wa Gaza

30 Januari 2026

Israel imeirejesha miili ya Wapalestina 15 katika Ukanda wa Gaza siku ya Alhamisi ikiwa ni siku kadhaa baada ya kukabidhiwa mwili wa mateka wa mwisho kutoka kwenye ukanda huo.

https://p.dw.com/p/57jo2
Sehemu ya athari za mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza
Ukanda wa GazaPicha: Ramadan Abed/REUTERS

Miili hiyo imerejeswhwa Gaza wakati ambapo mjumbe maalumu wa Marekani Steve Witkoff akisema kuwa ana imani kwamba kundi la Hamas litasalimisha silaha kama sehemu ya mpango wa amani katika ukanda huo.

Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza imethibitisha kuwa Israel imeirejesha nyumbani miili ya Wapalestina 15, hatua inayoashiria kuingia katika awamu ya pili ya mpango wa amani kwa Gaza unaosimamiwa na Marekani.

Shirika la Msalaba mwekundu limeeleza kuwa limesimamia shughuli ya kuirejesha miili hiyo ambayo kulingana na msemaji wa Wizara ya Afya ya ukanda huo ilepelekwa katika Hospitali ya Shifa katika jiji la Gaza.

Makabidhiano ya mateka walio hai au waliouawa yalikuwa sehemu muhimu ya awamu ya kwanza ya makubaliano yaliyowezesha vita kusitishwa. Chini ya makubaliano hao, Israel imeshawarejesha wafungwa 2,000 wa Kipalestina na miili 360.

Kutokana na kukamilika kwa awamu hiyo ya kwanza ya mpango wa amani, Mjumbe Maalumu wa Marekani Steve Witkoff akizungumza mbele ya kikao cha baraza la mawaziri amesema anaamini kuwa kundi la wanamgambo wa Hamas la Palestina litasalimisha silaha.

Trump asisitiza Hamas wasalimishe silaha

Kwa upande wake Rais Donald Trump aliyekuwa kwenye kikao hicho Alhamisi ameliwekea suala hilo msisitizo akisema kuwa, "Sasa tunataka Hamas wasiwe na silaha. Kuna uwezekano mkubwa tutalifanikisha hilo. Wengi walisema kamwe hawatasalimisha silaha. Lakini inaonekana watafanya hivyo na walitusaidia kuirejesha nyumbani miili iliyokuwa imesalia."

Wanamgambo wa Hamas wakilinda moja ya maeneo katika Ukanda wa Gaza 03.11.2025
Wanamgambo wa kundi la Hamas wa PalestinaPicha: Omar Al-Qattaa/AFP

Awamu ya pili ya mpango wa amani wa Gaza wenye vipengele 20 unalitaka kundi la Hamas kusalimisha silaha na kuanzishwa kwa kikosi maalumu cha kimataifa cha kuhakikisha uthabiti kwenye Ukanda wa Gaza. Hata hivyo, wanamgambo wa Hamas bado wana takriban bunduki 60,000 katika eneo hilo. Japokuwa wako tayari kuachia mamlaka, hawakubaliani kabisa na suala la kusalimisha silaha zao.

Wakati mpango huo wa kusitisha mapigano ukitazamiwa kuingia awamu ya pili, jeshi la Israel limesema mapema Ijumaa kuwa limefanya mashambulizi dhidi ya magaidi wanane kusini mwa Rafah na limefanikiwa kuwauwa watatu kati yao. Taarifa ya jeshi hilo imefafanua kuwa magaidi hao walitokea kwenye handaki na kuwa jeshi la anga lilianzisha mashambulizi mara moja.

Bila kutoa maelezo zaidi jeshi hilo limesema limefanya mashambulizi zaidi katika maeneo ambayo halikuyataja na kwamba wanajeshi wake wataendelea kufanya msako ili kuwapata na kuwauwa magaidi wote.