1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel bado inaudhibiti Ukanda wa Gaza

Charo, Josephat30 Machi 2008

Misri kuchukua jukumu huko Gaza

https://p.dw.com/p/DXGY
Kifaru cha Israel kikiwa karibu na kivuko cha mpakani cha Karni kati ya Gaza na IsraelPicha: AP

Mkataba unaojadiliwa kati ya Israel na Misri huenda ukaifanya Israel ikate kabisa uhusiano na eneo la Ukanda wa Gaza. Chini ya mkataba huo Misri itakuwa msafirishaji pekee wa umeme katika Ukanda wa Gaza, kuchukua mahala pa Israel ambayo kwa wakati huu ndiyo muuzaji mkubwa wa umeme katika eneo hilo.

Kwa sasa Israel huipelekea Gaza asilimia 70 ya umeme inayouhitaji huku Misri ikipeleka asilimia 5. Asilimia nyingine ya mahitaji ya umeme ya Ukanda wa Gaza iliyosalia hutengenezwa katika kituo cha kutengeneza umeme kilicho mjini Gaza. Lakini ikiwa mpango mpya utatekelezwa, waya wa umeme wa megawati 150 utajengwa kutoka mji wa Arish katika jangwa la Sinai hadi Gaza, hivyo kumaliza kabisa hali ya Ukanda wa Gaza kutegemea umeme kutoka Israel.

Israel yataka kuondoka Gaza

Mwezi Februari mwaka huu wakati wanamgambo wa kipalestina walipovurumisha maroketi katika miji ya Israel, serikali ya Israel ilipunguza usafirishaji wa umeme katika Ukanda wa Gaza kama adhabu iliyolenga kuyakomesha mashambulio hayo.

Konflikt im Gaza Streifen Maskierte bewaffnete Hamas Kämpfer bei einer Demonstration in Gaza Stadt
Wanamgambo wa HamasPicha: AP

Wakati huo huo, mawaziri kadhaa waliitaka Israel ichukue hatua kadhaa zitakazokamilisha mchakato wa kuondoka kabisa kutoka Gaza ulioanza mnamo mwezi Agosti mwaka wa 2005 wakati waziri mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, alipoliondoa jeshi la Israel na walowezi takriban 8,000 wa kiyahudi kutoka Ukanda wa Gaza na kuvunja kila nyumba katika makazi zaidi ya 20 yaliyokuwa katika eneo hilo.

Mwezi uliopita naibu waziri wa ulinzi wa Israel, Matan Vilnai, alisema Israel inataka kujiondoa kabisa Gaza. "Tunataka kuacha kuwapelekea Wapalestina umeme, maji na dawa ili vitu hivi wavipate kutoka kwingine," alisema naibu waziri huyo. Mahali alipokuwa akipazungumzia naibu waziri Vilnai ni Misri, ambayo ilikuwa ikilidhibiti eneo la Ukanda wa Gaza kabla kutekwa na Israel katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka wa 1967.

Wapalestina waitegemea Israel

Huku mazungumzo ya kuikwamua Gaza isiitegemee tena Israel yakiendelea, miaka miwili na nusu tangu Israel kuondoka Gaza, wakaazi milioni 1.5 bado wanaitegemea Israel kwa karibu kila hitaji la kimsingi. Wapalestina wanasema kwamba kujiondoa kwa Israel kutoka Gaza ni aina tofauti ya kulikalia eneo hilo. Waisraeli lakini wanajibu kwa kusema kama wapalestina wangeitumia nafasi iliyojitokeza baada ya Israel kuondoka Gaza wangekuwa leo hii wanaweza kujitegemea katika maisha yao.

Mshauri wa zamani kuhusu maswala ya Wapalestina katika wizara ya ulinzi ya Israel, Shalom Harari, amesema kama Wapalestina wangeyashughulikia maendeleo ya kiuchumi badala ya kujiingiza katika machafuko, wangekuwa na uwanja wa ndege katika Ukanda wa Gaza na kama wavuvi wa kipalestina hawangekuwa wakivua makontena ya silaha yaliyoangushwa baharini, Israel haingelidhibiti pia eneo la pwani.

Israel haidhibiti tu umeme unaoingia Gaza bali pia chakula, dawa na misaada ya kiutu. Israel ni msafirishaji mkubwa wa maji huko Gaza na huamua ni wagonjwa gani mahututi wanaopewa vibali vya kwenda kupata matibabu mazuri ya dharura katika hospitali zake.

Mbali na kivuko cha Rafah kilicho katika mpaka kati ya Gaza na Misri, vivuko vyote vya kuingilia Gaza vinasimamiwa na Israel kama vile anga ya Gaza na mwambao wa pwani. Sarafu inayotumika katika Ukanda wa Gaza ni shekeli ya Israel.

Hamas yadhibiti Gaza

Tangu kundi la Hamas lilipolidhibiti eneo la Gaza kutoka kwa chama cha Fatah mnamo mwaka jana, Israel imeimarisha udhibiti wake wa eneo hilo, hivyo kupunguza bidhaa na umeme unaopelekwa huko. Serikali ya Israel inalieleza eneo la Gaza linalosimamiwa na kundi la Hamas kuwa eneo la adui kwa kuwa kundi hilo limejitolea kwa dhati kuiangamiza Israel na linakataa kulitambua taifa hilo la kiyahudi.

Terroristen stürzen Palästinenserbehörde
Wanamgambo wa Hamas wakishangilia utekaji wa GazaPicha: AP

Pande zote mbili zinalaumiana kwa ukweli kwamba miaka miwili na nusu baada ya Israel kuondoka Ukanda wa Gaza, eneo hilo bado linaitegemea sana Israel. Wapalestina wanasema ingawa jeshi la Israel na walowezi wameondoka Gaza, Israel bado inayadhibiti maisha ya kila siku katika ukanda huo na kwa hiyo kuikalia Gaza hakujaisha.

Ili mradi Israel inavidhibiti vivuko vyote vya mpakani, anga na pwani na inakataa kuruhusu watu wapite kati ya Gaza na Ukingo wa magharibi wa mto Jordan, maeneo mawili ya kijiografia ambayo wapalestina wana matumaini yataunda taifa lao huru katika siku za usoni, serikali ya Israel haiwezi kusema imeacha kulidhibiti eneo Gaza.