1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7 yaweka hazina ya miundombinu kwa nchi zinazostawi

Bruce Amani
27 Juni 2022

Viongozi wa Kundi la nchi saba tajiri ulimwenguni la G7 wanaokutana Ujerumani wametangaza mpango wa miundo mbinu wa dola bilioni 600 kwa ajili ya kuzisaidia nchi zinazoendelea kupambana na mabadiliko ya tabia nchi

https://p.dw.com/p/4DHjJ
Deutschland I G7-Gipfel auf Schloss Elmau in Garmisch-Partenkirchen
Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Mpango huo unaonekana kama jibu la nchi za Magharibi kwa Mradi mkubwa wa China wa ujenzi wa miundombinu ya usafiri na barabara unaojulikana kama Belt and Road Initiative - BRI. Beijing inatuhumiwa kwa kuzinasa nchi za kipato cha chini katika madeni ambayo haziwezi kumudu kuwa sehemu ya mradi wake wa BRI wa matrilioni ya dola.

Soma pia:Mataifa ya G7 yatakiwa kuzisaidia nchi masikini

Hazina mpya iliyotangazwa na G7 itaelekezwa kwenye miradi ya tabia nchi. Miradi hiyo ni pamoja na uwekezaji wa nishati ya jua nchini Angola wa dola bilioni 2, na ujenzi wa hospitali Cote d'Ivoire wa dola milioni 320. Mamia kadhaa ya waandamanaji wa mazingira walifanya maandamano katika mji mdogo karibu na kasri ambako mkutano huo wa kilele unafanyika.

Biden apongeza mshikamano dhidi ya Urusi

Deutschland I G7-Gipfel auf Schloss Elmau in Garmisch-Partenkirchen I  Joe Biden
Biden apongeza mshikamano dhidi ya UrusiPicha: Lukas Barth/AP/picture alliance

Rais Joe Biden wa Marekani amepongeza muungano wa kimataifa katika kukabiliana na Urusi, katika kipindi hiki ambacho yeye na viongozi wengine wa mataifa yaliyopiga hatua kiviwanda G7 wakiweka mikakati kuendeleza shinikizo katika jitihada zao za kuitenga Urusi kutokana na uvamizi wake wa Ukraine.

Katika mkutano wa utangulizi, kabla ule wa kilele wa G7 wa jimboni Bavaria, Biden akiwa na mwenyeji wake Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa ushirikiano wa mataifa hayo, amesema lazima kuwe na hakikisho la kuendelea kuwa wamoja.

Rais huyo wa Marekani aliongeza kwa kusema wataendelea kuzifanyia kazi changamoto za kiuchumi, kukabiliana nazo na kuzishinda. Biden na viongozi wenzake wanakutana kwa siku tatu kwa lengo la kujadili jinsi ya kupata uhakika wa nishati na kukabiliana na mfumuko wa bei, kwa lengo la kuzuia kuporomoka kwa uchumi kwa jitihada yao ya kuiadhibu Urusi.

Zelensky kuomba saada zaidi

Rais Volodymyr Zelensky atayahimiza madola yenye nguvu duniani kuongeza msaada wao kwa Ukraine wakati atakapouhutubia mkutano wa kilele wa kundi la G7 leo. Rais Joe Biden wa Marekani na wenzake kutoka kundi la nchi Saba Tajiri duniani, wanaokutana katika milima ya Bavaria hapa Ujerumani, wamesisitiza umoja wao katika wakati huu wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Zelensky atajiunga na viongozi wa Marekani, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa, Italia, Japan na Canada kwa njia ya video asubuhi hii. Hapo jana, Urusi ililipiga jengo la makaazi mjini Kyiv, na kumuuwa mtu mmoja huku wengine saba wakijeruhiwa. Biden aliyalaani mashambulizi hayo aliyoyaita ya kikatili, ambayo yalikuwa ya kwanza kuulenga mji mkuu baada ya karibu wiki tatu. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na mwenyeji wa G7 alisema shambulizi hilo lilionyesha tena kuwa ni vizuri kusimama pamoja na kuwasaidia Waukraine.

afp, reuters, ap, dpa