1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama: Kuipa Ukraine vifaru kutakuwa na athari kwa Ujerumani

John Juma | Rashid Chilumba
25 Januari 2023

Mwenyekiti wa chama cha wanajeshi wa Ujerumani André Wüstner asema kuipa Ukraine vifaru chapa Leopard kunaweza kudhoofisha utayari wa operesheni ya jeshi la Ujerumani.

https://p.dw.com/p/4MgI8
Deutschland Bundeswehr Kampfpanzer Leopard 2 A7V
Picha: Philipp Schulze/dpa/picture-alliance

Utayari wa jeshi la Ujerumani kwenye operesheni zake utadhoofishwa zaidi na hatua inayotarajiwa ya kuipa Ukraine vifaru vya kivita chapa Leopard. Hayo ni kulingana na mwenyekiti wa chama cha wanajeshi wa Ujerumani André Wüstner.

Lakini mataifa ya magharibi yanapoamini vifaru hivyo vya kisasa vitaongeza nguvu kwa vikosi vya Ukraine kupambana na Urusi, swali linaloulizwa ni kwa kiasi gani?

Marekani kuipelekea Ukraine vifaru chapa M1 Abrams

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Ujerumani ZDF, Wustner amesema kuipa Ukraine vifaru vya kivita chapa Leopard ni hatua nzuri kwa upande mmoja, lakini pia ni mbaya kwa upande mwingine, hususan kuhusu utayari wa operesheni za jeshi la Ujerumani.

Wito wa kuimarisha viwanda vya Ulinzi

"Ikiwa tunataka kuisaidia Ukraine, lakini vilevile kuwa na uwezo wa kujilinda wenyewe, basi ni sharti wanasiasa waimarishe sekta ya viwanda vya ulinzi, ili zana muhimu zinazohitajika ziwepo katika miaka ijayo,” amesema Wunster huku akiongeza kuwa "katika miaka ya hivi karibuni, imekuwa bayana kwamba tuko tayari tu katika hali ya ulinzi pale pasipo na budi”. Ukweli ni kwamba tangu Februari tumeendelea kuipa Ukraine zana na risasi.”

"Wanasiasa wana jukumu sio tu la kuisaidia Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi, bali pia katika ulinzi wa kitaifa na wa washirika wake," amesema Wunster.

Ujerumani yalaumiwa kwa kusita kwa sasa kupeleka vifaru aina ya Leopard nchini Ukraine.

Baada ya kuchelea kwa muda mrefu, hatimaye serikali ya Ujerumani imeamua kuipa Ukraine vifaru vya kivita chapa Leopard, na vilevile kuruhusu nchi nyingine zilizo na vifaru hivyo vilivyotengenezwa Ujerumani kuvipa Ukraine.

Kwa miezi kadhaa, Ukraine imekuwa ikiomba kupewa vifaru hivyo ili kujilinda na kupambana na vikosi vya Urusi.

Mwenyekiti wa chama cha wanajeshi Ujerumani amehoji kuwa ipo haja ya kuimarishwa kwa sekta ya viwanda vya Ulinzi ili zana muhimu zinazohitajika ziwepo.
Mwenyekiti wa chama cha wanajeshi Ujerumani amehoji kuwa ipo haja ya kuimarishwa kwa sekta ya viwanda vya Ulinzi ili zana muhimu zinazohitajika ziwepo.Picha: Moritz Frankenberg/dpa/picture-alliance

Ubora wa vifaru chapa Leopard

Waundaji wa vifaru aina ya Leopard chapa nambari 2 kampuni ya kijerumani ya Krauss-Maffei Wegmann wanavitaja kuwa "vifaru bora kabisa duniani" katika uwanja wa vita.

Kwa zaidi ya miaka 50 tangu vilipoundwa kwa mara ya kwanza, vifaru chapa Leopard vimesadifu kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya mashambulizi, kuwa na mwendokasi usio kifani, kutoa ulinzi, kukwepa hujuma za adui na kufanya kazi kwenye mazingira mengi kwenye uwanja wa mapambano.

Vifaru vya Urusi vyaivamia ardhi ya Ukraine

Kifaru hicho hicho chenye uzito wa tani 55 kwa kawaida hubeba watu wanne na kina uwezo wa kusafiri umbali wa kilometa 500 kwa safari moja kikiwa na mwendokasi wa kilometa 68 kwa saa.

Hivi sasa kuna aina nne ya vifaru hivyo na aina ya karibuni kabisa iliundwa mwaka 1979. Silaha yake kubwa ni mzinga wenye upana wa milimita 120 unaoweza kufyetuliwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa kabisa.

Idadi ya vifaru Leopard vilivyouzwa nje

Hadi sasa kuna zaidi ya vifaru vya Leopard 2,000 vilivyouzwa kwa mataifa mbalimbali ya Ulaya na Canada. Kwa jumla kampuni ya Krauss-Maffei Wegmann inasema vifaru 3,500 ndiyo vimesambazwa kwenye mataifa 19 duniani. Inaelezwa kuwa aina hivyo ya vifaru ndiyo iliyouzwa kwa nchi nyingi zaidi duniani kuliko kifaru kingine chochote cha kijeshi kilichowahi kuundwa.

Swali kubwa lakini ni kipi kitabadilika kwenye vita vinavyoendelea iwapo Ukraine itapatiwa vifaru chapa Leopard? Mtafiti wa masuala ya ulinzi wa taasisi ya sera ya mji London  Yohann Michel, anasema aina hiyo vifaru vitaliwezesha jeshi la Ukraine kujibu mapigo kwa uhakika bila kuhofia changamoto zozote katika uwanja wa mapigano.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amekuwa akiziomba nchi za magharibi kuipa nchi yake silaha zenye nguvu na ubora zaidi mfano vifaru chapa Leopard ambavyo vimetengeneza Ujerumani ili kujilinda na kupambana na vikosi vya Urusi vilivyoivamia nchi yake.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amekuwa akiziomba nchi za magharibi kuipa nchi yake silaha zenye nguvu na ubora zaidi mfano vifaru chapa Leopard ambavyo vimetengeneza Ujerumani ili kujilinda na kupambana na vikosi vya Urusi vilivyoivamia nchi yake.Picha: President of Ukraine/apaimages/IMAGO

Anasema kwa kuchanganya zana nyingine za kisasa ambazo Ukraine imepatiwa na nchi za magharibi pamoja na vifaru vya Leopard, Ukraine itaweza kumudu kusonga mbele na kuyakomboa maeneo zaidi yaliyokamatwa na Urusi.

Upelekwaji vifaru hivyo utaisaidia nchi hiyo kupata nguvu ya kupigana kwa silaha nzito kwa kubadili vifaru vyake vya enzi ya sovieti na hivyo vya kisasa na vyenye uwezo mkubwa. 

Raths anasema vifaru vya Leopard vina uwezo wa kisasa wa kiuendeshaji ikilinganishwa na aina ya vifaru vya Urusi chapa T ambavyo kwa mfano haviwezi kurudi nyuma kwa kasi. 

Vita vya Ukraine vimeupindua mfumo wa dunia - Olaf Scholz

Tahadhari ya baadhi ya wataalamu wa ulinzi

"Hebu fikiria bondia asiyeweza kujigeuza geuza kwa uhuru kwenye ulingo wa pambano , isipokuwa kuelekea upande mmoja pekee, bila shaka bondia mweingine mwenye uwezo wa kupinduka kila upande atakuwa na nafasi nzuri, na hilo ndiyo inapokuja suala la vifaru vya Leopard" amesema mtaalamu huyo wa masuala ya ulinzi.

Hata hivyo wako wataalamu wengine wanaotoa tahadhari wakisema upelekaji wa vifaru hivyo hakumaanishi kutaimarisha nafasi ya jeshi la Ukraine moja kwa moja. 

Mtafiti mwingine wa masuala ya ulinzi kutoka taasisi ya masuala ya ulinzi ya nchini Uswisi Niklas Masuhr, amesema ni lazima jeshi la Ukraine liwe na uwzeo wa kutosha wa kuvitumia vifaru hivyo tena kwa mbinu mahsusi pamoja na zana nyingine za kivita ndiyo matokeo yataonekana. 

Ni lazima kuwepo na mchanganyiko wa silaha za kufyetua makombora, mifumo ya ulinzi wa anga, wataalamu wa kuongoza vita na helikotpa ndiyo mtu ataweza kuona manufaa ya vifaru mamboleo chapa Leoparad kwenye uwanja wa mapambano, amesema Niklas Masuhr. 
Vyanzo: Dpa, Afp