1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken kuzuru Afrika kujaribu kuweka mambo sawa

Angela Mdungu
20 Januari 2024

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken anapanga kufanya ziara yake barani Afrika wiki Ijayo. Mataifa atakayoyatembelea ni pamoja na Cape Verde, Ivory Coast, Nigeria na Angola ambapo atajadili usalama.

https://p.dw.com/p/4bUrK
Waziri wa mambo y anje wa Marekani| Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken.Picha: Evelyn Hockstein/Pool/AP/picture alliance

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema kuwa Blinken, atayatembelea mataifa hayo kuanzia Jumapili Januari 21 hadi 26 atakapopata pia nafasi ya kujadili kuhusu ushirika wa Marekani na Afrika katika masuala ya biashara, hali ya hewa, miundo mbinu na afya.

Masuala mengine yatakayotupiwa macho ni pamoja na usalama wa kikanda, kuzuia mizozo na kukuza demokrasia.

Nigeria, moja ya nchi atakazotembelea Blinken ni taifa lenye nguvu kubwa katika Ukanda wa Afrika ya Magharibi na ina nafasi kubwa katika masuala ya kiusalama hasa yale yanayohusisha machafuko yanayofanywa na makundi ya itikadi kali kwenye ukanda wa Sahel.

Changamoto za kiusalama zinazoisibu Afrika ya magharibi hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika Niger zitajadiliwa Blinken atakapokuwa ziarani.

Msaidizi wa Blinken anayeshughulikia masuala ya Afrika, Molly Phee aliwaambia wanaandishi wa habari kuwa, Marekani ina historia inayofahamika na matumaini kuwa viongozi wa serikali ya kijeshi ya Niger itachagua kushirikiana na Washington badala ya Urusi.

Soma pia: Blinken: Marekani kutoa tangazo 'zito' kuiunga mkono Afrika

Msaidizi huyo wa Blinken ameongeza kuwa, iwapo watawala hao wa kijeshi watachagua kushirikiana na Urusi, mambo yatakuwa magumu.

Niger Niamey | Ziara ya waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Anthony Blinken
Blinken akikaribishwa na waziri wa mambo ya nje wa Niger Hassoumi Massoudou alipotembelea nchi hiyo Machi 16, 2023. Picha: Boureima Hama/AP/picture alliance

Phee aliitolea mfano Mali ambapo amesema kumekuwa na ongezeko la majeruhi pamoja na  mashambulizi ya kiusalama tangu serikali ya nchi hiyo ilipolikaribisha kundi la mamluki wa kijeshi wa kampuni ya Wagner ya Urusi.

Urusi yazidi kujiimarisha Afrika Magharibi

Wizara ya ulinzi ya Urusi mapema Jumanne ilisema kuwa nchi hiyo na Niger, zimekubaliana kuanzisha ushirikiano wa kijeshi tangu mapinduzi ya mwaka uliopita.

Viongozi wa kijeshi wa Niger walivifukuza vikosi vya Ufaransa na kukatisha mikataba ya kiusalama na Umoja wa Ulaya hali iliyowaacha washirika wa mataifa ya magharibi kuhofia kuwa nchi hiyo huenda ikageuka kuwa ngome mpya ya Urusi katika ukanda huo.

Molly Phee amesema kuwa ziara ya Blinken barani Afrika ni sehemu ya ufuatiliaji wa mkutano uliofanyika Washington na kuhudhuriwa mna viongozi wa bara hilo mwaka 2022 ambapo rais Joe Biden aliahidi kuwa Marekani ko kwa ajili ya mustakabali wa Afrika.

Niger imekuwa mshirika muhimu wa Marekani katika mapambano yake dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali ambao wameshawauwa maelfu ya watu katika ukanda wa Sahel huko Afrika ya magharibi.

Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa und Blinken
Blinken akiwa na mazungumzo na Rais wa Afrika Kusini Cyrill Ramaphosa, Agosti 2022. Marekani inajaribu kurejesha ushawishi wake Afrika baada ya kulitekeleza bara hilo kwa muda mrefu.Picha: Andrew Harnik/AFP

Suala jingine linalotarajiwa kuangaziwa kwenye safari hiyo ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani barani Afrika ni mivutano inayoendelea kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Soma pia: Wanaharakati wataka Blinken azingatia haki za binadamu katika safari Afrika

Blinken anaizuru Afrika wakati Marekani ikiwa na wasiwasi kuhusu uhusiano wake na bara hilo hasa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya Niger na Gabon pamoja na machafuko yanayoendelea Sudan na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Atakapokuwa Ivory Coast, Antony Blinken huenda akahudhuria michuano ya kombe la mataifa ya Afrika katika mechi itakayochezwa kati ya taifa hilo mwenyeji na Equatorial Guinea.

Itakumbukwa kuwa Marekani na China, zimekuwa zikipambania kupata ushawishi kote barani humo. Mada hii huenda ikawa katika ajenda zitakazojadiliwa Blinken atakapofika Angola, nchi ambayo China inailenga katika kufanya uwekezaji muhimu.

Chanzo: APE/Reuters