1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlin yapitisha sheria ya kupinga ubaguzi

Sylvia Mwehozi
5 Juni 2020

Jiji la Berlin limepitisha sheria ya kwanza ya kupinga ubaguzi, ambayo inawazuwia wazi maafisa wenye mamlaka, wakiwemo polisi, kumbagua mtu yeyote kwa misingi ya rangi ya ngozi yake, jinsia au masuala mengine.

https://p.dw.com/p/3dIh2
March against Racism in Berlin
Picha: picture-alliance/dpa/P. Zinken

Sheria hiyo inazuia dhahiri mamlaka ikiwemo polisi na shule za umma, kumbagua mtu kwa misingi ya asili yake, rangi, jinsia, dini, hali ya kimwili au kiakili, mtizamo wa kidunia, na umri.

Sheria hiyo inaeleza kuwa watu hawapaswi kubaguliwa kwa kutofahamu lugha ya Kijerumani, magonjwa sugu au kipato chao, elimu na hata kazi. Chini ya sheria hiyo wahanga wanayo haki ya kupewa fidia, ingawa mamlaka nazo zinayo nafasi ya kupinga madai ya ubaguzi.

Ingawa sheria hiyo imekuwepo kwa wiki kadhaa, lakini hivi sasa imechukua mwelekeo mpya kutokana na kile kinachoendelea ulimwenguni cha maandamano ya kupinga ukatili wa polisi na kupinga ubaguzi, yaliyozuka nchini Marekani na kusambaa katika maeneo mengi duniani, ikiwemo Berlin kwenyewe. Akizungumzia kuhusu mauaji ya George Floyd, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema yalikuwa ya kutisha.

''Mauaji ya George Floyd yanatisha, ubaguzi unatisha na jamii ya Marekani imegawika. Nadhani wanasiasa wanapaswa kuungana na kupatana. Nadhani mfumo wa siasa wa Rais Trump una utata. Hilo liko wazi. Ubaguzi siku zote umekuwepo, lakini kwa bahati mbaya upo hapa Ujerumani pia. Tunapaswa kuiweka nyumba yetu wenyewe vizuri na matumaini kwamba watu wa Marekani watasonga mbele kwa maandamano ya amani,'' alisema Merkel.

Deutschland Berlin Pressekonferenz zum Konjunkturpaket | Angela Merkel
Kansela Angela Merkel amesema tatizo la ubaguzi ni kubwa na linapaswa kushughulikiwa kwa dhati.Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Ni sheria pana zaidi

Sheria hiyo mpya inakwenda mbali zaidi ya sheria ya sasa ya shirikisho inayohusu usawa iliyopitishwa mwaka 2006. Shirika la kupinga ubaguzi katika mwongozo wa sheria hiyo iliyochapishwa mwaka jana, limesema kuwa sheria hiyo ilikuwa ikipinga ubaguzi katika eneo la ajira na kati ya raia wa kawaida, lakini ''haikuyagusa maeneo yanayoongozwa na sheria za umma''.

Hata hivyo shirika hilo limebainisha kwamba ''ubaguzi bado unapigwa marufuku katika muktadha wa namna hiyo'' kwa kuzingatia kwamba katiba ya Ujerumani inatamka suala la kuwalinda raia wake dhidi ya ubaguzi wote kutoka ndani na nje ya jimbo.

Serikali ya muungano ya Berlin inayoundwa na chama cha Social Democratic, chama cha mrengo wa kushoto Die Linke na chama cha Kijani, ilitoa hoja kwamba sheria ya sasa haikuwa inajitosheleza na kwamba sheria mpya itasaidia kuondoa pengo la kisheria.

Hata hivyo sheria hiyo ilipata ukinzani kidogo katika siku za hivi karibuni hususan kutoka kwa waziri wa mambo ya ndani, Horst Seehofer na vyama vya polisi wa Ujerumani, wanaodai kuwa sheria mpya inaweka shinikizo kubwa kwa mamlaka. "Tunapaswa kusimama na polisi na sio kuwatuhumu kwa ujumla”, Seehofer alilieleza gazeti la Tagesspiegel wiki iliyopita.

Waziri wa sheria wa Berlin na mwanasiasa wa kutoka chama cha Kijani, Dirk Behrendt aliitetea sheria hiyo ya kupinga ubaguzi akisema haitoingilia majukumu ya kila siku ya polisi badala yake itasaidia kuelezea ubaguzi wa kimfumo.

Mnamo mwezi Machi baraza la Umoja wa Ulaya liliitolea wito Ujerumani kuzidisha juhudi zake za kupambana na ubaguzi, ikiwemo kulitaka jeshi la polisi kushiriki kwenye mafunzo ya kuainisha aina za ubaguzi.

Berlin Unteilbar-Demonstration
Waandamanaji mjini Berlin wakipinga ubaguzi katika mmoja ya maandamano.Picha: Reuters/M. Tantussi

Chanzo: DW