Benki ya Amerika Kusini kuanzishwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Benki ya Amerika Kusini kuanzishwa

Tangazo lililotolewa na rais wa Venezuela, Hugo Chavez la kuanzisha benki mpya ya Amerika Kusini linasikika kama tangazo la vita. Benki hiyo itakayojulikana kwa jina Banco del Sur, inanuiwa kuchukua nafasi ya benki ya dunia katika siku za usoni.

Rais Hugo Chavez wa Venezuela

Rais Hugo Chavez wa Venezuela

Kwenye mkutano nchini Paraguay viongozi wa serikali na marais wanataka kuzindua benki hiyo kwa jina Banco del Sur yaani benki ya Amerika Kusini. Lengo la benki hiyo ni kutoa mikopo ya kudhamini miradi mbalimbali kama inavyofanya benki ya dunia na fuko la fedha la kimataifa, IMF.

Rais wa Venezuela, Hugo Chavez, amesema benki ya Banco del Sur inatakiwa kuwa chombo msingi kitakachowaletea watu wa Amerika Kusini maendeleo. Aidha kiongozi huyo amesema hawatatakiwa kuendelea kuitegemea benki ya dunia mjini Washington wala fuko la fedha la kimatafa, IMF, akisema taasisi hizo zinatumiwa kuendeleza ubabe wa nchi zenye uwezo mkubwa duniani.

Kupitia mradi huo wa benki mpya ya maendeleo ya kikanda, Argentina, Brazil, Bolivia, Ecuador, Paraguay na Venezuela zinataka kuvunja ushawishi mkubwa wa benki ya dunia.

Federico Foders ni mtaalamu wa maswala ya kiuchumi katika taasisi ya uchumi wa kimataifa kwenye chuo kikuu cha Kiel hapa Ujerumani. Anasema benki ya Baco del Sur ina malengo mazuri.

´Benki hiyo imejiwekea malengo mazuri, ikiwa ni pamoja na kudhamini juhudi za kujenga miundo mbinu katika Amerika Kusini au pia mambo ambayo hayajaonekana huko kama vile kuwapa mikopo watu wa tabaka la kati maishani. Kwa hiyo kama nilivyosema malengo haya yanaonekana kuwa mazuri.´

Hata hivyo mtaalamu huyo haamini kuwepo kwa taasisi ya fedha itakayofanana na benki ya dunia au fuko la fedha la kimatafa, IMF. Anapinga kiwango cha dola bilioni saba zinazotakikana kuanzisha benki ya Banco del Sur ambacho kimegawanywa sawa miongoni mwa nchi wanachama zichangie.

´Kiwango hicho si kikubwa sana. Nakumbuka mzozo nchini Argentina mnamo mwaka wa 2001 ulioikwamisha nchi kwa sababu nchi hiyo ilikuwa na deni la kima cha dola bilioni 150 za kimarekani na hiyo inadhihirisha kianzio cha dola bilioni saba si kikubwa.´

Hans Hartwig Blomeier, kiongozi wa idara inayohusika na maswala ya Amerika Kusini katika wakfu wa Konrad Adenauer, kwa upande wake anaona benki ya Banco del Sur huenda ikatumiwa kama chombo cha kisiasa na rais wa Venezuela Hugo Chavez.

Kwa sababu katika mpango mzima rais Chavez anata kuwa na usemi mkubwa na ushawishi katika bara zima. Kwa kufanikisha hayo anahitaji taasisi maalumu. Televisheni inayomilikiwa na mataifa kadhaa ya Tele Sur ilikuwa hatua ya kwanza na sasa benki ya Banco del Sur ni hatua ya pili.´

Mradi wa kwanza wa benki ya Banco del Sur ni mradi wa Gasoducto del Sur utakaodhamini ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Venezuela hadi Argentina litalakalokuwa na urefu wa kilomita 8,000. Cuba huenda ikawa nchi ya kwanza kuomba mkopo katika benki hiyo kwani ilisahaulika kama mteja na haikufaidi kutoka kwa benki ya dunia na fuko la fedha la kimataifa.

 • Tarehe 27.06.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHC3
 • Tarehe 27.06.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHC3

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com