Baraza la Usalama latoa tamko dhidi ya Israel.
1 Juni 2010Matangazo
Tamko hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo
limetolewa mwisho mwa kikao cha dharura, kilichofanyika kwa zaidi
ya saa 12, limelaani kitendo hicho ambacho kimesababisha vifo vya
watu 10 na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Taarifa iliyotolewa imesema Baraza la Usalama limeizingatia
maelezo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya kufanyika kwa
uchunguzi wa haraka, usio na upendeleo wa uhakika na wenye uwazi
unaokidhi viwango vya kimataifa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka pia kuachiliwa
haraka kwa meli na wanaharakati wanaoshikiliwa na Israel.
Awali Radio ya Israel iliripoti kuwa Israel inawashikilia wanaharakati
wapatao 480 na kwamba imewafukuza wengine 48.
Balozi wa Mexico Claude Heller ambaye ndiye mwenyekiti wa muda
wa baraza la usalama amesema taasisi hiyo muhimu ya kimataifa
imesisitizia wasi wasi wake juu ya hali ya kibinadamu iliyoko Gaza.
Aidha taarifa hiyo imesisitizia pia kwamba ufumbuzi wa mzozo wa
mgogoro wa Israel na Palestina ni kuwepo kwa mataifa mawili na
kuelezea wasiwasi wake kutokana na tukio hilo kutokea wakati
mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanaendelea kati ya pande
hizo.
Kwa upande wake Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,
Oscar Fernandez-Taranco amesema shambulio hilo la umwagaji
damu lililofanywa na Israel lingeweza kuzuiwa.
Katika kikao hicho cha baraza la Usalama, mataifa ya kiarabu
ambayo yalikuwa yakiungwa mkono na wanachama wengine wa
baraza hilo ikiwemo Uturuki, wameitaka pia Israel kuondoa vizuizi
ilivyoweka dhidi ya Gaza, haraka kuiachia meli hiyo na wanaharakati
wa haki za binadamu na kuweza kuwaruhusu kupeleka bidhaa zao
hizo, ukanda wa Gaza.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Uturuki Ahmet amekielezea
kitendo hichio cha Israel kama ni janga baya kutokea katika historia
ya ubinadamu, mpaka kati ya ugaidi na taifa haupo tena.
Wakati serikali mbalimbali duniani zikiendelea kuilaumu Israel kwa
hatua yake hiyo, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa
litakutana leo kuzungumzia pia suala hilo mjini Geneva, huku Jumuia
ya Kujihami ya NATO na mabalozi kutoka nchi 27 za Umoja wa Ulaya
wakipanga pia kukutana kuzungumzia suala hilo mjini Brussels.
Waandamanaji kadhaa tayari wamejitokeza katika miji mbalimbali
duniani kupinga kitendo hicho cha Israel.
Wakati huo huo Israel imeonya leo kwamba itazuia meli zote za
misaada kufika katika Ukanda wa Gaza, wakati wanaharakati,
wakiahidi kufanya jaribio jipya kuhakikisha kuwa wanafika eneo hilo.
Mwandishi: Halima Nyanza(afp,dpa)
Imepitiwa na :Hamidou Oummilkheir:
Matangazo