1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi, China zazuia azimio la Baraza la Usalama kuhusu Gaza

22 Machi 2024

Urusi na China zimetumia siku ya Ijumaa kura zao za turufu kuipinga rasimu ya azimio lililopendekezwa na Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu usitishaji wa mapigano huko Gaza.

https://p.dw.com/p/4e2uc
Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo wa GazaPicha: Seth Wenig/AP Photo/picture alliance

Urusi na China zilitumia kura zao za turufu kuipinga rasimu ya azimio hilo la Marekani, huku Algeria ikipiga kura ya kuipinga na nchi ya Guyana ikijizuia. Wanachama wengine 11 wa Baraza la Usalama walipiga kura ya ndio, wakiwemo wanachama wa kudumu wa Ufaransa na Uingereza.  

Urusi imeituhumu Marekani kwa kuandaa kile ilichokiita kuwa ni "maonyesho ya kinafiki". Balozi wa Urusi, Vasily Nebenzia, amesema kuwa Marekani haifanyi chochote kuishinikiza Israel kuachana na vita, na kusema Washington inathubutu kuzungumzia suala la usitishaji vita wakati Gaza inaendelea kufutwa kabisa kwenye uso wa dunia.

 New York | Balozi wa Marekani katika UN- Linda Thomas-Greenfield
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield (Mwanamke aliyepandisha mkono juu)Picha: Angela Weiss/AFP/Getty Images

Urusi imeendelea kwamba azimio hilo litaihakikishia Israel kwamba haitowajibishwa kwa kuwa hata uhalifu wake haujatathminiwa katika pendekezo hilo la Marekani. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield, amelaani kura hizo za turufu za Urusi na China na kusema mataifa hayo hayakuwa na nia ya kuipigia kura azimio ambalo limependekezwa na Marekani.

 Israel yanyakua ardhi katika Ukingo wa Magharibi

Israel imetangaza siku ya Ijumaa kunyakua karibu hekta 800 ambazo ni sawa na ekari 1,977 za ardhi katika  Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, jambo ambalo wanaharakati wamelitaja kuwa hatua kubwa zaidi na ya aina yake katika miongo kadhaa.     

Hatua hiyo ya Israel ilitangazwa na Waziri wake wa Fedha Bezalel Smotrich ambaye amesema kuwa eneo hilo lililonyakuliwa huko kaskazini mwa bonde la Jordan, sasa ni "ardhi ya serikali."

Soma pia: Marekani yapinga mipango ya ujenzi wa makaazi mapya ya walowezi

Shirika la Israel la uangalizi wa makazi linalofahamika kama "Peace Now" limesema ukubwa wa eneo lililonyakuliwa ni kubwa zaidi tangu kusainiwe mkataba wa Oslo wa mwaka 1993, na kwamba  mwaka huu wa 2024 unaongoza kwa idadi ya ardhi zilizotangazwa kunyakuliwa.      

Eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu
Makazi ya walowezi katika eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavuPicha: AHMAD GHARABLI/AFP

Israel ilinyakua maeneo ya Ukingo wa Magharibi, Jerusalem mashariki na Ukanda wa Gaza katika vita kati ya mataifa ya kiarabu na Israel vya mwaka 1967. Kuweka maeneo ya makazi katika ardhi ya Wapalestina ni kosa kwa mujibu wa sheria za kimataifa, lakini licha ya shinikizo la kimataifa, Israel imejenga majumba ya makazi  wanakoishi waisraeli wapatao 490,000 katika eneo la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Umoja wa Mataifa uliripoti kuongezeka kwa kasi kwa ujenzi wa makaazi haramu eneo hilo tangu kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas huko Gaza, na kusema hatua hiyo inaondoa uwezekano wowote wa kuwa na taifa huru la Palestina. 

Soma piaIsrael yaidhinisha umiliki wa kipande kipya cha ardhi Ukingo wa Magharibi:  

Katika ibada ya Ijumaa ya pili katika mwezi huu mtukufu wa ramadhan, Mohammad Abu El-Ez, ni Mpalestina anayeishi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na amesema kwa masikitiko:

"Tunashuhudia Ramadhani ya aina yake, yenye huzuni na maumivu kwetu na kwa mataifa ya Kiislamu na Kiarabu. Ingawa niko umbali wa mita kadhaa kutoka Msikiti wa Al-Aqsa, kwa muda wa miezi sita nimezuiliwa kuingia. Leo, baada ya uratibu na mateso makubwa, nimeweza kupata kibali na kuingia, ingawa ninauona mnara wa msikiti huo kutoka nyumbani kwangu, lakini nilizuiwa."

Blinken ziarani Israel kujadili vita vya Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ambaye yuko ziarani huko Israel kwa mazungumzo kuhusu vita vya Gaza, amesema upanuzi huo wa makazi utakwamisha mpango wa kufikia amani ya kudumu kati ya Israel na Wapalestina.

Soma pia:Bado hakuna mwelekeo wa amani kati ya Israel na Hamas

Blinken amekutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mazungumzo yao yamejikita zaidi katika suala la kuwezesha misaada zaidi inawasilishwa huko Gaza. Lakini Netanyahu amemueleza Blinken kwamba wataendelea na operesheni yao iliyopangwa huko Rafah.

Jana, Blinken alikutana na viongozi wa mataifa ya kiarabu mjini Cairo nchini Misri na kujadiliana namna ya kufikiwa kwa makubaliano ya usitishwaji mapigano na mikutano kama hiyo inaendelea pia hii leo huko nchini Qatar.

(Vyanzo: Mashirika)