1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Marekani yapinga ujenzi wa makaazi mapya ya walowezi

24 Februari 2024

Marekani imelaani pendekezo la Israel la kujenga zaidi ya makaazi mapya 3,300 ya walowezi wa kiyahudi kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi kujibu shambulizi baya lililofanywa na Wapalestina mapema wiki hii.

https://p.dw.com/p/4cpVK
Makaazi ya walowezi wa kiyahudi huko Ukingo wa Magharibi
Sehemu ya makaazi ya walowezi wa kiyahudi huko Ukingo wa Magharibi Picha: Ariel Schalit/AP/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema katika mkutano na waandishi wa habari huko Buenos Aires, Argentina, kwamba amesikitishwa na tangazo hilo la Israel na kuongeza kuwa makazi hayo "yanakiuka sheria za kimataifa na kamwe hayataimarisha usalama wa Israel."

Waziri wa Fedha wa Israel Bezalel Smotrich alitangaza mipango ya ujenzi wa makaazi hayo mapya siku ya Alhamisi, baada ya Wapalestina watatu wenye silaha kuyafyatulia risasi magari karibu na makazi ya Maale Adumim, na kumuua raia mmoja wa Israel na kuwajeruhi watano.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zimeonyesha ongezeko la ghasia za walowezi wa kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi tangu kuzuka kwa vita vya Israel na Hamas Oktoba 7, mwaka uliopita.