1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la kijeshi Sudan kuzungumza na makundi ya kisiasa

Grace Kabogo
12 Aprili 2019

Maelfu ya waandamanaji nchini Sudan wameweka kambi nje ya wizara ya ulinzi mjini Khartoum kushinikiza iundwe serikali ya kiraia, na wamekaidi amri iliyotolewa na baraza la mpito la kijeshi ya kutotoka nje usiku.

https://p.dw.com/p/3Gfb2
Demonstration Sudan Karthoum
Picha: Reuters

Waandamanaji hao ambao wamekuwa wakiandamana karibu kila siku kuipinga serikali ya Omar al-Bashir ambaye ameitawala Sudan kwa miaka 30, wameukataa uamuzi wa kuanzishwa kwa baraza la mpito la kijeshi ambalo limetangaza kuitawala nchi hiyo kwa miaka miwili na wameahidi kuendelea na maandamano hadi serikali ya kiraia itakapowekwa.

Wanaharakati wamewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi katika sala ya Ijumaa nje ya wizara ya ulinzi, eneo kuu ambako maandamano yamekuwa yakifanyika. Mahema makubwa yamewekwa katika eneo hilo na watu wameleta vyakula na kugawa maji kwa umati mkubwa wa watu. Ahmed al-Sedek, mwenye umri wa miaka 39 amesema hajalala nyumbani kwake tangu walipoanza kuweka kambi nje ya makao makuu ya jeshi Jumamosi iliyopita.

Chama cha upinzani cha Congress kimataka kuanzishwa kwa baraza la pamoja la kijeshi na kiraia ili kutawala katika kipindi cha mpito cha miaka minne. Pia kimelitaka jeshi kukabidhi mamlaka kwa raia. Na habari za hivi punde zinasema kuwa baraza la mpito la kijeshi limesema linapanga kuanza mazungumzo na makundi ya kisiasa baadae leo.

Sudan | Awad Ibn Auf als Präsident des militärischen Übergangsrates vereidigt
Rais wa baraza la mpito la kijeshi, Mohammed Ahmed Awad Ibn AufPicha: picture-alliance/AA

Akizungumza na waandishi habari, mkuu wa kamati ya kijeshi na kisiasa, Omar Zein al Abidin, ambaye ameteuliwa na Rais wa baraza la mpito la kijeshi, Mohammed Ahmed Awad Ibn Auf, amesema wanataka kujenga mazingira ya kufanyika mazungumzo na kwamba lenyewe halina suluhisho katika mzozo wa Sudan, bali suluhisho lilatoka kwa waandamanaji.

''Baraza letu linawajumuisha mkuu wa polisi, mkuu wa usalama na kamanda wa vikosi vya jeshi, na hatutalazimisha kitu chochote kwa wananchi. Tunatarajia kuwa kipindi cha mpito kitakuwa cha miaka miwili, ingawa kinaweza kuwa kifupi hata kwa mwezi mmoja, iwapo mambo yatatatuliwa bila ghasia,'' alisema Zein al Abidin.

Mataifa yenye nguvu duniani ikiwemo Marekani na Uingereza, yamelitolea wito jeshi kuwaachia raia kuamua kiongozi wanayemtaka kuwaongoza na kwamba miaka miwili ni mingi kwa jeshi hilo kutawala. Mataifa hayo yamesema yanaunga mkono kipindi cha mpito cha amani na demokrasia mapema zaidi ya miaka miwili.

Mexiko UN unterstützen Mexiko bei Ermittlungen zu verschleppten Studenten | Michelle Bachelet und Marcelo Ebrard
Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet Picha: Reuters/Str.

Umoja wa Ulaya kwa upande wake umelisihi jeshi kukabidhi haraka madaraka kwa utawala wa kiraia na kuwepo hali ya utulivu. Hata hivyo, Umoja wa Afrika umelaani njia iliyotumika kumuondoa Bashir madarakani ukisema haikuwa sahihi katika kuzitatua changamoto zinazowakabili watu wa Sudan pamoja na matakwa yao.

Mkuu wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameitaka Sudan kulinda haki za binaadamu na kujizuia na ghasia. Bachelet amewasihi viongozi wa Sudan kuwaachia huru watu waliokamatwa kutokana na kuandamana kwa amani na kuchunguza matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji ambao walianza kuandamana tangu mwezi Desemba mwaka uliopita. Amebainisha kuwa Sudan inakabiliwa na kipindi muhimu na tete na hakuna uhakika kuhusu mustakabali wa Sudan.

Ama kwa upande mwingi ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa imeitaka serikali ya Sudan kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC ambayo awali ilitoa waranti wa kukamatwa Rais Bashir kwa makosa ya uhalifu wa kivita.