Baraza la mawaziri la Ujerumani lakutana leo Berlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Baraza la mawaziri la Ujerumani lakutana leo Berlin

Baraza la mawaziri la Ujerumani linakutana leo mjini Berlin kujadili mpango wa kupeleka ndege za kivita aina ya tonado nchini Afghanistan. Wakati huo huo, mawaziri wa ulinzi wa shirika la NATO wanajiandaa kukutana kesho mjini Seville Hispania, kujadili mkakati wa kukabiliana na wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan.

Ndege aina ya Tonado zitakazopelekwa Afghanistan

Ndege aina ya Tonado zitakazopelekwa Afghanistan

Baraza la mawaziri la Ujerumani linakutana leo mjini Berlin kujadili mpango wa kupeleka ndege sita za kivita aina ya tonado kwenda nchini Afghanistan. Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, alisema ndege hizo huenda zipelekwe Aghanistan mwezi Aprili kama bunge la Ujerumani litaidhinisha swala hilo mapema mwezi Machi. Kuna uwezekano mkubwa wa baraza la mawaziri kuukubali mpango huo, ingawa idadi kubwa ya Wajerumani wanapinga kupelekwa ndege za kivita za Ujerumani kwenda Afghanistan.

Kamanda wa jeshi la NATO, John Craddock, amesema uamuzi wa Ujerumani kupeleka ndege zake kwenda Afghanistan ni muhimu sana na utakaribishwa.

´Ni muhimu sana. Sitaki kutoa maelezo ya kina, lakini bila shaka hakuna upelelezi wa kutosha unaofanywa kutumia ndege.´

Craddock amesema Afghanistan imepewa kipaumbele na shirika la NATO. Ni kibarua kigumu lakini mataifa yanayoshiriki katika juhudi za kuijenga upya nchi hiyo yanatakiwa kufanya kila yanavyoweza kufanikisha jambo hilo.

Bunge la Ujerumani Bundestag litatakiwa kuupigia kura mpango huo ifakapo mwanzoni mwa mwezi Machi. Kama mpango huo utaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge, ndege za tonado zitapelekwa nchini Afghanistan kuanzia katikati ya mwezi Aprili kwa kibarua cha kwanza. Ndege hizo zitatakiwa kufanya upelelezi katika maeneo yote ya Afghanistan na wala sio tu eneo la kusini linalokabiliwa na machafuko. Hayo yalithibitibishwa jana na waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung alipowatembelea wanajeshi wa Ujerumani kwenye kambi yao huko Mazar i Sharif nchini Afghanistan.

´Ndege za tonado zinaweza kuruka nchini kote zikitaka. Tuna eneo la kilomita 2,400 katika mpaka na Pakistan ambalo ni tete. Kwa msingi huo, kwa sisi kuwa tayari kuliziba pengo lililopo, ndilo ombi lilolowasilishwa kwetu na shirika la NATO.´

Waziri Jung amesema ndege za tonado zitapelekwa Afghanistan kwa kipindi cha miezi sita. Maofisa wa Ujerumani wamesema ndege hizo zitatumika tu kufanyia upepelezi. Kutumia kamera zake ndege hizo zitapiga picha za kuonyesha mienendo ya waasi wa Taliban. Hata hivyo waziri Jung amelionya jeshi la ISAF liwe tayari kukabiliana na wanamgambo wa Taliban.

´Bila shaka kama magaidi watashambulia kutakuwa na haja ya kuwa tayari kujilinda na pia kukabiliana nao. Tunajua kwamba nchini Afghanistan kumekuwa na mashambulio mengi yakiwemo mashambulio 2,000 yaliyofanywa na watu wa kujitolea mhanga maisha.´

Wakati huo huo, mawaziri wa ulinzi wa shirika la NATO wanajiandaa kukutana kesho mjini Seville, kusini mwa Hispania, kujadili mkakati mpya wa kupambana na upinzani mkali wa waasi wa Taliban unaowakabili wanajeshi wa NATO nchini Afghanistan. Katika mkutano huo wa siku mbili, Marekani itawashinikiza washirika wake wa NATO kuongeza idadi ya wanajeshi na rasilimali kama ilivyofanya, ili kuwachakaza waasi wa Taliban.

 • Tarehe 07.02.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHKc
 • Tarehe 07.02.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHKc

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com