Barack Obama ziarani Berlin | Magazetini | DW | 18.06.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Barack Obama ziarani Berlin

Ziara ya rais Barack Obama nchini Ujerumani,hali nchini Uturuki na mivutano ndani ya chama cha SPD siku chini ya 100 kabla ya uchaguzi mkuu ni miongoni mwa mada zilizohanikiza katika magazeti ya Ujerumani

Kansela Angela Merkel na rais Barack Obama walipokutana katika mkutano wa kilele wa mataifa tajiri kiviwanda na yale yaliyoendelea G20 mjini Cannes Ufaransa

Kansela Angela Merkel na rais Barack Obama walipokutana katika mkutano wa kilele wa mataifa tajiri kiviwanda na yale yaliyoendelea G20 mjini Cannes Ufaransa

Tunaanza na ziara ya rais wa Marekani Barack Obama mjini Berlin,gazeti la Mittelbayerische Zeitung linaandika:"Nusu karne baada ya ziara ya John F.Kennedy,kinachohitajika hivi sasa sio tena kusifiana bali ufumbuzi thabiti wa matatizo yaliyopo.Kuanzia kuzorota ukuaji wa kiuchumi na mgogoro wa sarafu ya euro,kupitia Syria,Iran na Korea ya kaskazini hadi kufikia masuala ya nishati na kuhifadhiwa data za watu.Washirika wanakutana mjini Berlin wakiwa katika hali ya usawa.Jambo ambalo ni muhimu kwa ulimwengu na pia kwa Ulaya.

Gazeti la "Der neue Tag linazungumzia kuhusu makubaliano ya soko huru kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya.Gazeti linaendelea kuandika:"Kutangazwa tarehe ya kuanza mazungumzo kati ya Umoja wa ulaya na Marekani kuhusu makubaliano ya soko huru ni ishara njema.Soko hilo litazifaidisha pande zote mbili.Kwasababu biashara huru kati ya madola yaliyoendelea sana kiuchumi inafungua milango ya neema kwa wote wanaohusika.Na ukuaji wa kiuchumi,wanahitaji haraka tangu wamarekani mpaka wakaazi wa Ulaya.

Kwanini walimwengu wanakaa kimya?

Türkei Ankara Ausschreitungen Kennedy Street

Machafuko mjini Ankara:polisi wanafyetua gesi za kutoa machozi dhidi ya waandamanaji

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamemulika pia hali nchini Uturuki na kukosoa jinsi walimwengu wanavyofanya tahadhari.Gazeti la "Sächsische Zeitung" linaandika:Tahadhari za walimwengu katika kuikosoa Uturuki zinamaanisha kitu kimoja tu na kinahusu umuhimu wa kimkakati wa Uturuki.Hakuna anaetaka kutamka maneno makali kwa kuhofia yasije yakachochea mivutano ya kisiasa na kuitenga Ankara.Erdogan bado ana turufu mkononi:Wazungu na wamarekani wana msimamo wa ndumila kuwili.Kwa nchi za Umoja wa ulaya,halizuki suala angalao kwa sasa la kuichukulia Uturuki kama mshirika-seuze mwanachama kamili.Kwanini lakini nchi hiyo,inaendelea kuwa mshirika katika jumuia ya kujihami ya NATO licha ya matumizi yaliyokithiri ya nguvu dhidi ya waandamanaji"Hakuna aliyeweza kutoa jibu la kuridhisha la suala hilo hadi sasa.

.SPD watapa tapa

SPD-Kanzlerkandidat Peer Steinbrück mit Ehefrau Gertrud Steinbrück

Mgombea kiti cha kansela kutoka chama cha SPD Peer Steinbrück na mkewe Gertrud Steinbrück

Mada yetu ya mwisho magazeti inamulika mivutano ndani ya chama cha upinzani cha Social Democratic SPD,miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika:"Peer Steinbrück na SPD wana chini ya siku 100 kuugeuza mkondo wa mambo:Kila kitu kinaashiria hawatofanikiwa-hata kama SPD sasa wanaanza kuzindukana na kusimama kidete nyuma ya uongozi wao.Steinbrück anatambua fika kitakachojiri pindi SPD wakishindwa katika uchaguzi mkuu ujao.Atakaeshindwa zaidi ni yeye mwenyewe.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman