Zimbabwe hali ya kisiasa yazidi kutia mashaka uchaguzi ukikaribia | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.06.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Zimbabwe hali ya kisiasa yazidi kutia mashaka uchaguzi ukikaribia

Mugabe asema hatoki madarakani kumpisha kibaraka

Nchini Zimbabwe zikiwa zimesalia wiki kadhaa kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa Rais miito inazidi kutolewa na jumuiya ya kimataifa ya kuitaka serikali ya nchi hiyo ikubali kuwaruhusu waangalizi wa kimataifa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa njia ya haki na huru.Naibu katibu mkuu anayehusika na masuala ya kisiasa katika Umoja wa mataifa Haile Menkerios anatazamiwa kuwasili nchini humo hii leo kwa ziara ya siku tano kujadili hali ya mambo kabla ya uchaguzi wa tarehe 27.

Haya yote yanafanyika huku ghasia zikiripotiwa kuzagaa kwenye maeneo ya mijini karibu na mji mkuu Harare ambapo wapinzani wanasemekana kushambuliwa.

Ghasia zinadaiwa kufika kwenye maeneo ya miji ya karibu na mji mkuu Harare na wahanga wakubwa wa ghasia hizo ni wanaharakati wa upinzani.Inadaiwa polisi leo hii walipekuwa kwa muda wa saa tatu nyumba ya katibu mkuu wa chama cha upinzani cha Movement for Demokratic Change MDC Tendai Biti ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uhaini.Kwa mujibu wa wakili wa Tendai Lesis Uriri polisi walipekuwa kila kitu ndani ya nyumba hiyo ikiwemo computa ndogo ya laptop lakini hakuna kitu walichochukua. Biti alitazamiwa kufikishwa mahakamani leo lakini wakili wake anasema hatua hiyo huenda ikacheleweshwa. Kutokana na hali hiyo ya kisiasa nchini Zimbabwe kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2005 Umoja wa mataifa umemtuma mjumbe wake wa ngazi ya juu nchini humo kwa lengo la kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo juu ya hali ya kisiasa pamoja na uchaguzi wa rais wa tarehe 27 mwezi huu.

Ziara hiyo ya siku tano ya naibu katibu mkuu wa Umoja wa mataifa anayehusika na masuala ya kisiasa Haile Menkerios imekuja kufuatia shinikizo za nchi za kigeni na wanasiasa wa upinzani juu ya kumtaka rais Robert Mugabe akubali kuruhusu waangalizi wa kimataifa wasimamie uchaguzi huo wa rais.

Akizungumza leo hii katika mkutano wa pamoja na rais Bush na waandishi wa habari Brown ameutaja utawala wa rais Mugabe kuwa wa kihalifu na unaotapatapa kutaka kuingia tena madarakani. Wiki iliyopita balozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa Zalmy Khalilzad alitoa taarifa kali juu ya ziara hiyo ya Menkerios ikisema iwapo rais Mugabe hatoshirikiana na mjumbe huyo wa Umoja wa mataifa na hali ya sasa kuendelea kama ilivyo basi watabidi kuchukua hatua zinazostahili.

Kwa hivi sasa polisi imeweka sheria ya kutotoka nje ya saa 12 katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Masvingo eneo ambalo limeathirika vibaya na ghasia za hivi karibuni.

Halikadhalika rais Mugabe hajaacha kutoa shutuma dhidi ya makundi mbali mbali mara hii anasema mashirika ya misaada yalitumia suala la uhaba wa chakula kuwabadili nia wapiga kura dhidi ya chama chake wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi mwezi Marchi.Mugabe amesema kutokana na hilo ndipo alipoamua kuyapiga marufuku mashirika hayo hadi yatakapofanyiwa uchunguzi wa kisawasawa kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao.Hali hiyo imesababisha madhara makubwa huku shirika la kuwahudimia watoto la Umoja wa mataifa UNICEF likisema watoto nusu millioni hawapati huduma za matibabu, ikiwa ni pamoja na dawa za virusi vya HIVna ukimwi au chakula baada ya kuwekwa marufuku hiyo.Aidha rais Mugabe anasema vyovyote itakavyokuwa hawezi kuachia madaraka kwa mtu yoyote ambaye hana mtizamo sawa na wake.kwa maana nyingine anasema hawezi kumuachia madaraka kibaraka yoyote wa nchi za magharibi kama vile Morgan Tsvangirai isipokuwa atakuwa tayari kuachia ngazi ikiwa kutakuweko kiongozi kutoka chama chake.Hivi karibuni pia rais huyo aliapa kwamba hawezi kumuachia madaraka Tsvangirai na kwamba yuko tayari kuingia vitani kwa ajili ya nchi yake.Tsvangirai alimshinda rais Mugabe kwenye uchaguzi wa rais wa mwezi Marchi lakini hakupata wingi wa kura wa kumuwezesha kushinda moja kwa moja kinyang'anyiro hicho.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com