Ziara ya Musharraf Ulaya | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.01.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ziara ya Musharraf Ulaya

Rais wa Pakistan ameanza ziara ya nchi kadhaa za ulaya

default

Musharraf anaamkiana na muakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya Javier Solana

Rais Pervez Musharraf wa Pakistan leo hii ameanza ziara yake katika mataifa manne ya Ulaya kwa kuwatolea mwito viongozi wa nchi za magharibi kuwa na subira juu ya mwenendo wa kidemokrasia nchini mwake.Akiwa nchini Ubelgiji Musharraf amekiri kwamba kuna mivutano ya kisiasa nchini Pakistan ambayo huenda ikawafanya  watakaoshindwa katika uchaguzi mkuu ujao kutokubaliana na matokeo.
►◄


Katika ziara yake hii ambayo ni ya kwanza muhimu kabisa katika nchi za nje tangu kuanza kwa  mivutano ya  kisiasa nchini Pakistan  rais Pervez Musharraf amezitaka nchi za magharibi kutoa muda zaidi kwa utawala wake kufikia kiwango  cha juu cha demokrasia,haki za binadamu na uhuru wa kiraia.


Amesema nchi yake inaweza kufikia kiwango cha juu ya demokrasia kama yalivyo mataifa ya magharibi ikiwa tu taifa hilo litapewa muda wa kufika huko.


Katika kituo chake cha kwanza cha ziara hiyo nchini Ubelgiji rais Musharraf amefanya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kibiashara na kijeshi na waziri mkuu wa nchi hiyo Guy Verhofstadt.Mjini Brussels amesema uchaguzi unaokuja utafanywa kwa njia huru na ya wazi na yeyote atakayeshinda bila shaka atapewa uongozi na wala hakutakuwepo na ushindani wowote katika kuundwa serikali  na chama chochote kitakachoibuka na ushindi katika uchaguzi huo.

Pakistan imetumbukia ndani ya mzozo mkubwa wa kisiasa tangu kuuwawa  mwezi uliopita kwa kiongozi wa upinzani Benazir Bhutto mzozo ambao ulizusha ghasia na kusababisha kughairishwa kwa uchaguzi mkuu.


Kufuatia hali hiyo Rais Musharraf amekiri kwamba mivutano ya kisiasa imeligubika taifa lake na kwamba kuwa uwezekano mkubwa wa yoyote atakayeshindwa kwenye kinyang'anyiro hicho kudai kwamba kumepitika mizengwe.


Hata hivyo amesema vyombo vya habari ambavyo viliwekewa vikwazo katika utoaji habari katika muda wa wiki sita wa hali ya hatari iliyotangazwa mwezi Novemba vitakuwa huru kutangaza shughuli hiyo ya uchaguzi na kwamba havitawekewa mipaka katika kutekeleza kazi zao.


Rais Musharraf ambaye anatafuta uungaji mkono juu ya masuala ya kiuchumi pamoja na kisiasa katika ziara hiyo amesistiza kwamba makampuni ya kigeni sio walengwa wa ghasia za pakistan ingawa amekubali kwamba ni vita dhidi ya magaidi ni vigumu sana ijapokuwa amesema watashinda vita hivyo.


Miongoni mwa nchi za ulaya atakazozitembelea rais Musharraf ni pamoja na Ufaransa,uswisi na Uingereza,tayari ameshakutana na mkuu wa sera za nje wa Umoja wa ulaya Javier Solana na kuzungumzia miongoni mwa mada walizozizungumzia ni vita dhidi ya ugaidi.Itakumbukwa kwamba Musharraf amekuwa akishutumiwa kwa kushindwa kupambana na wapiganaji wa Kitaliban na hasa  katika eneo la mji wa Quetta.


Pia atakutana na katibu mkuu wa jumuiya ya kujihami ya nchi za magharibi NATO Jaap De Hoop Scheffer halikadhalika kuhutubia kamati ya bunge la umoja wa ulaya inayohusika na masuala ya mambo ya nje.

 • Tarehe 21.01.2008
 • Mwandishi Ramadhani Yusuf, Saumu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CvXC
 • Tarehe 21.01.2008
 • Mwandishi Ramadhani Yusuf, Saumu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CvXC

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com