Waziri Steinmeier wa Ujerumani ziarani Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.04.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waziri Steinmeier wa Ujerumani ziarani Afghanistan

Shambulio la kujitolea maisha muhanga nchini Afghanistan limejeruhi wanajeshi 4 wa Kijerumani muda mfupi tu baada ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani kuwasili Kabul kwa ziara ya siku mbili nchini Afghanistan.

German Foreign Minister Frank-Walter Steinmeier, left, shakes hands with Afghan counterpart Rangin Dadfar Spanta during their meeting in Kabul Wednesday, April 29, 2009. Steinmeier arrived in the Afghan capital Wednesday morning on an unannounced two-day visit to meet with senior Afghan leadership. (AP Photo/Rahmat Gul)

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,Frank-Walter Steinmeier na waziri mwenzake wa Afghanistan Rangin Dadfar Spanta mjini Kabul,April 29,2009.

Waziri Frank-Walter Steinmeier, akifanya ziara yake ya nne nchini Afghanistan, amelilaani shambulio lililolenga mlolongo wa magari ya wanajeshi wa Kijerumani, kaskazini mwa nchi hiyo. Amesema vitendo hivyo havitoitisha Ujerumani na kuifanya iachane na jukumu lake la kuisaidia Afghanistan.Akaongezea:

"Shambulio la hii leo huko Kunduz limedhihirisha mawili: kwanza ni kuwa hata kaskazini mwa Afghanistan hali ya usalama si nzuri hivyo. Pili ni kuwa wanajeshi wetu wanakabiliwa na jukumu kubwa katika eneo hilo."

Ziara ya Steinmeier ambayo haikutangazwa hapo kabla, inafanywa majuma matatu baada ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, kuizuru Afghanistan na kukutana na baadhi ya wanajeshi wa Kijerumani ambao ni sehemu ya vikosi vya kimataifa kusaidia kulinda usalama, chini ya uongozi wa NATO nchini Afghanistan.

Baada ya kukutana na Rais Hamid Karzai wa Afghanistan, Steinmeier, aliefuatana na Bernd Muetzelburg, mjumbe wake maalum huko Afghanistan na Pakistan, alisema lengo kuu ni lile lile- kurejesha hali ya utulivu nchini Afghanistan. Njia ya kutekeleza jukumu hilo kubwa ni kutafuta suluhisho la pamoja katika kanda hiyo. Kwa hivyo, ni muhimu kuishirikisha Pakistan katika jitahada za kupiga vita ugaidi katika eneo hilo.

Iwapo hatua hazitochukuliwa kuwazuia Wataliban wanaoendelea kujiimarisha nchini Pakistan, basi jitahada za huko Afghanistan zitafanikiwa kwa kiwango fulani tu. Eneo la Pakistan linalopakana na Afghanistan hutumiwa kama maficho ya wanamgambo wanaoishambulia Afghanistan mara kwa mara. Juma lijalo, Rais Karzai wa Afghanistan na rais Asif Ali Zardari wa Pakistan wanatazamiwa kukutana na Rais wa Marekani, Barack Obama, mjini Washington.

Ujerumani ina kama wanajeshi 3,800 nchini Afghanistan na katika miezi ijayo idadi hiyo itaongezwa kufikia 4,400, huku Afghanistan ikijitayarisha kwa uchaguzi wa urais uliopangwa kufanywa mwezi wa Agosti.

Kwa upande wake,Rais Karzai amemshukuru Steinmeier kwa ziara yake ya nne nchini Afghanistan. Amesema ziara hiyo pia inathibitisha urafiki wa muda mrefu kati ya Ujerumani na Afghanistan.Waziri Steinmeier anatazamia kurejea Ujerumani siku ya Alkhamisi.

Mwandishi: P.Martin

Mhariri: Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com