Wazimbabwe wakabiliwa na uhaba wa chakula | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wazimbabwe wakabiliwa na uhaba wa chakula

Wazimbabwe wanaokabiliwa na njaa wanakimbilia nchini Afrika Kusini kununua mahitaji yao. Huku mfumuko wa bei ukiwa umezidi asilimia 1,700, uchumi wa Zimbabwe unasambaratika kwa kasi kubwa na watu wanapata tabu ya kununua vyakula.

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe (kushoto) na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe (kushoto) na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini

Ni wakati wa chakula cha mchana katika duka kubwa la kuuza bidhaa la Patel katika mji wa mpakani wa Musina baina ya Zimbabwe na Afrika Kusini na Wazimbabwe wengi wanamiminika kununua bidhaa huku nchi yao ikikabiliwa na mzozo mkubwa. Ikiwa ni mojawapo ya maduka ya mwisho kabla kufikia mpaka wa Afrika Kusini, duka la Patel limekuwa likiuza kila kitu kutoka tomato ya mkebe na nguo za kulalia kwa Wazimbabwe wanaokabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na mfumko mkubwa wa bei.

Zimbabwe iliyokuwa zamani nchi iliyonawiri zaidi kiuchumi barani Afrika inatumbukia katika tatizo kubwa la kiuchumi. Maduka mengi yamejaa aina mbili ya bidhaa, mafuta na sabuni. Watu hawawezi kufikiria kuhusu vitu vya starehe kama vile biskuti au marashi, amesema Gilbert Dube, anayefanya biashara ya kuuza vyakula na mboga katika eneo la mpakani kwenda mjini Harare. Wanataka tu kununua vitu wanavyohitaji. Wanalazimika kufua, kuoga na kupika chakula,´ ameongeza kusema mfanyabiashara huyo.

Huku mfumko wa bei ukifikia zaidi ya asilimia 1,700, na ukosefu wa jira ukiwa zaidi ya asilimia 80, uchumi wa Zimbabwe unasambaratika kwa kasi kubwa ikilinganishwa na eneo lengine lililo nje ya eneo la vita na watu wengi wanang´ang´ana kulipia vyakula.

´Viwanda vyote vimeporomoka. Viwango vya umasikini, mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira. Watu hawawezi hata kugharamia nauli ya kwenda kazini na kurudi nyumbani. Hatujawaona Wazimbabwe wakiwa katika umaskini kama huu. Hali ni ngumu imekuwa kama janga.´

Wachambuzi wanasema mzozo unaendelea nchini Zimbabwe unahatarisha ustawi wa kiuchumi katika eneo zima na maafisa wa Afrika Kusini, ambayo imekuwa ikiendeleza sera ya kukaa kimya juu ya jirani yake, wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu mzozo unaobisha hodi mlangoni.

Uhaba wa chakula katika maeneo mengi ya Zimbabwe umesababisha bei za vyakula kupanda kufikia viwango ambavyo wananchi hawawezi kuvimudu. Hivyo Wazimbabwe wengi wanaoweza huenda kununua bidhaa katika maduka ya mjini Musina karibu na mpakani. Chupa moja ya mafuta inauzwa kwa randi 14 sawa na dola 1.94 ya Marekani, amesema Beauty Hotel, alipokuwa akiepua magunia mawili barabarani mjini mwake, Kwekwe, katikati mwa Zimbabwe. Msichana huyo pamoja na mamake hupeleka chakula katika kituo cha Musina.

Wazimbabwe wengi hutegemea chakula kutoka kwa jamaa zao walioihama Zimbabwe kwenda kufanya kazi nchini Afrika Kusini. Mabasi yanayosafiri kila siku kutoka Johannesburg kwenda Zimbabwe hubeba idadi ndogo ya abiria na kujaza vyakula na magunia ya mchele, unga wa mahindi na hata mbuzi. Wazimbabwe wengi kati ya Wazimbabwe milioni mbili wanaoishi nchini Afrika Kusini huwapelekea chakula jamaa zao kupitia madareva wanaosafirisha bidhaa hizo hadi mjini Harare na miji mingine kutumia magari madogo ya kubebea mizigo.

Herbert Mabara ni dereva wa basi linalosafiri kutoka Durban na Johannesburg kwenda mjini Beitbridge nchini Zimbabwe kila baada ya siku kadhaa. Hakuna kitu nchini Zimbabwe. Aidha maduka ni matupu au yanauza bidhaa kwa bei ya juu mno,´ amesema dereva huyo. Watu wetu wanakabiliwa na njaa, tafadhali mkamateni Mugabe mmpeleke nchini Uingereza na mmtupe gerezani, ´ameongeza kusema Mabara kwa hasira.

Wakosoaji wanamlaumu rais Robert Mugabe kwa kuvuruga uchumi wakati wa utawala wake wa miaka 27, lakini Mugabe anazilaumu nchi za magharibi ambazo anasema zina njama ya kumuondoa madarakani kwa sababu ya kuyateka mashamba ya wazungu na kuwapa ardhi hiyo Wazimbabwe.

 • Tarehe 27.03.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHHQ
 • Tarehe 27.03.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHHQ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com