1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapinzani wahimiza maandamano zaidi Iran

Grace Kabogo afp, ap, reuters
8 Januari 2026

Makundi ya kutetea haki za binaadamu yamesema kuwa vikosi vya usalama nchini Iran vimetumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za moto kuwatawanya waandamanaji, ambao wamegadhabishwa na mzozo wa kiuchumi.

https://p.dw.com/p/56WC9
Iran Ilam 2026 | Maandamano dhidi ya serikali Iran
Vikosi vya usalama vya Iran vimetumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za moto kuwatawanya waandamanaji.Picha: UGC

Wanaharakati hao wa kutetea haki za binaadamu pia wamewashutumu maafisa kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo kuvamia hospitali ili kuwakamata waandamanaji waliojeruhiwa. Mashirika hayo yamesema Alhamisi kuwa vikosi vya usalama vimetumia nguvu kinyume cha sheria kuwakabili waandamanaji.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International, limesema vikosi vya usalama vya Iran vimewajeruhi na kuwaua waandamanaji na wapita njia. Makundi ya wapinzani wanaoishi uhamishoni yametoa wito wa kufanyika kwa maandamano mapya pamoja na migomo.

Siku 12 za maandamano zimeutikisa utawala wa Iran, ambao tayari unapambana na mzozo wa kiuchumi baada ya miaka mingi ya vikwazo na ikiwa inajiweka sawa kutokana na vita vya mwezi Juni, 2025 dhidi ya Israel.

Serikali yadai waandamanaji wanasababisha ghasia 

Mamlaka imewashutumu waandamanaji kwa kusababisha ghasia na mwanasheria mkuu ameapa kwamba hakutakuwa na huruma katika kuwafikisha mbele ya sheria. Shirika la habari la Iran, Fars limeripoti kuwa katika maandamano ya Jumatano, askari polisi wa Iran aliuawa kwa kuchomwa kisu magharibi mwa Tehran, katika juhudi za kudhibiti ghasia.

Iran Teheran 2026 | Ayatollah Ali Khamenei
Kiongozi wa Juu wa Iran Ayatollah Ali KhameneiPicha: IRANIAN LEADER PRESS OFFICE/Anadolu/picture alliance

Maandamano makubwa zaidi yalishuhudiwa Jumatano, ambapo yalifika hadi kwenye vijiji na miji mikubwa katika kila jimbo. Kulingana na shirika la wanaharakati wa haki za binadamu lenye makao yake nchini Marekani, hadi sasa ghasia zinazoyazunguka maandamano hayo, zimewaua takribani watu 38, huku wengine zaidi ya 2,200 wakiwa wamekamatwa.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema kuwa nchi yake haitaki vita na Israel wala Marekani, lakini iko tayari kupambana ikiwa itashambuliwa tena.

"Hatutaki vita. Lakini tumejiandaa kwa vita. Pia tumejiandaa kwa mazungumzo. Lakini mazungumzo ambayo yanategemea maslahi ya pande zote na yenye kuheshimu pande zote," alisisitiza Araghchi.

Türkei Istanbul | Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas AraghchiPicha: Arif Hudaverdi Yaman/Anadolu/IMAGO

Akizungumza Alhamisi mara baada ya kuwasili mjini Beirut, Lebanon Aragchi amewaambia waandishi habari kuwa pia Iran iko tayari kwa mazungumzo na Marekani kuhusu mpango wake wa nyuklia, ikiwa tu kama mazungumzo hayo yataheshimu pande zote, badala ya Marekani kutoa amri.

Aragchi ameyatoa matamshi hayo huku kukiwa na hofu kwamba Israel, mshirika wa karibu wa Marekani anaweza kuilenga tena Iran kama ilivyofanya wakati wa vita ya siku 12 iliyoanzisha dhidi ya Tehran, mwezi Juni. Israel iliwaua maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi na wanasayansi wa nyuklia, na Marekani ilishambulia vituo muhimu vya nyuklia vya Iran.

Aidha, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema lengo la ziara yake nchini Lebanon ni kujadili ''changamoto na vitisho'' vya Israel kwa usalama wa kikanda, pamoja na kutanua uhusiano baina ya nchi hizo mbili.