Wapinga wafungwa wa Guantanamo Bay kuhamishiwa Marekani | Masuala ya Jamii | DW | 16.12.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Wapinga wafungwa wa Guantanamo Bay kuhamishiwa Marekani

Wabunge wa chama cha Republican nchini Marekani wamepinga vikali taarifa kwamba Rais Barack Obama anapanga kuwahamisha wafungwa wa jela la Guantanamo kwenda katika gereza lililoko kwenye jimbo la Ilinois nchini humo.

Wafungwa wa jela Guantanamo Bay

Wafungwa wa jela Guantanamo Bay

Hapo jana utawala wa Rais Obama ilitangaza mpango huo, katika barua iliyosema kuwa serikali ya shirikisho inapanga kulichukua jela la Thomson Correctional Center lililoko katika jimbo hilo la Illinois kwa ajili ya wafungwa hao wa Guantanamo .

Hatua hiyo imekuja mnamo wakati ambapo Rais Barack Obama anajaribu kutimiza ahadi yake ya kulifunga jela la Guantanamo Bay ambalo linatumika kwa ajili ya washukiwa wa ugaidi.Jela hilo liko katika eneo la Cuba na ambalo limekuwa likilaumiwa na jumuiya ya kimataifa.

Lakini taarifa ya kutaka kuwahamishia wafungwa wa jela hilo Guantamo Bay huko Illinois imewakasirisha wabunge wa Republican ambao wameapa kuipinga.

Mike Pence ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Indiana amesema kwa kuwahamishia katika ardhi ya Marekani wafungwa hao ambao wanajulikana kama magaidi, utawala wa Rais Obama unatoa kipaumbele kikubwa zaidi kwa mahusiano ya kimataifa, kuliko usalama wa nchi.

Naye kiongozi wa upande wa upinzani marepublican wenye idadi ndogo ya viti katika bunge John Boehner amesema hatopiga kura kuruhusu hatua hiyo ya kuwahamishia Marekani wafungwa hao wa Guantanamo .

Hata maseneta wa chama hicho cha Republican ambao waliunga mkono uamuzi wa kulifunga jela hilo la Guantanamo , wameelezea wasiwasi wao wa kuwahamishia Marekani wafungwa hao.

Seneta Lindsey Graham wa jimbo la Carollina ya Kusini amesema kuwa ana hisia kwamba utawala wa Rais Obama umepoteza mwelekeo katika jukumu lake la kutaka kulifunga jela hilo haraka iwezekanavyo.

Hata hivyo idadi kubwa ya wabunge wa jimbo hilo la Illinois wamekuwa wakipigia upatu wafungwa hao wapelekwe kwenye jela hilo la Thomson, wakisema kuwa hatua hiyo itafungua nafasi zaidi za ajira.

Gavana wa jimbo hilo la Illinois Pat Quinn pamoja na seneta mwandamizi wa jimbo hilo kutoka chama cha Democrat Dick Durbin katika taarifa yao ya pamoja walipongeza hatua hiyo ya utawala wa Rais Obama kuwahamishia wafungwa hao Illinois.

Ikulu ya Marekani inaonekana inafahamu fika kuhisiana na msimamo huo wa Republican kuhusiana na uamuzi wake huo, ambapo katika taarifa iliyotiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje Hillary Clinton pamoja na Waziri wa Ulinzi Roberts Gates, wamesisitiza kuwa wafungwa hao watapelekwa nchini Marekani kwa ajili tu ya kuwekwa kizuizini na siyo kufungwa.

Wamesema kuwa Rais Obama hana nia wala dhamira ya kuwaachia huru wafungwa hao wa Guantanamo huko nchini Marekani na kuongeza kuwa hatua hiyo inazuiwa na sheria zilizopo za Marekani.

Haijafahamika wazi ni wafungwa wangapi kati ya 210 wanaoshikiliwa katika jela hilo la Guantanamo ambao watahamishiwa katika jela la Thomson huko Illinois, ambako watawekwa sehemu tofauti na wafungwa wengine.

Waziri wa Ulinzi Roberts Gates amesema wafungwa 116 wa jela hilo wataachiwa huru au kurejeshwa katika nchi zao.

Hiyo itafanya zaidi ya wafungwa 100 kubakia kizuizini, wakiwemo wale ambao watashtakiwa katika mahakama za kijeshi au kiraia na wengine ambao watawekwa kizuizini kwa muda usiyojulikana, kutokana na kuchukuliwa kuwa ni watu hatari sana lakini hawawezi kushtakiwa kutokana na kutokuwepo kwa ushahidi wa kutosha kuwashtaki.

Afisa mmoja wa juu wa Marekani amesema kuwa wafungwa wanaotakiwa kushtakiwa katika mahakama ya kijeshi watashtakiwa wakiwa kwenye jela hilo la Thomson huko Illinois.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com