Waathirika wa mafuriko Pakistan wakabiliwa na njaa na magonjwa | Masuala ya Jamii | DW | 23.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Waathirika wa mafuriko Pakistan wakabiliwa na njaa na magonjwa

Hayo yameelezwa na Umoja wa Mataifa na kwamba bado inawawia vigumu wafanyakazi wa mashirika ya misaada kugawa chakula katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo.

Mama wa Kipakistani akiwa amewabeba watoto wake akiwaokoa na mafuriko.

Mama wa Kipakistani akiwa amewabeba watoto wake akiwaokoa na mafuriko.

Umoja wa Mataifa umesema kuwa mamilioni ya wananchi wa Pakistan wanakabiliwa na njaa na magonjwa baada ya nchi hiyo kukumbwa na mafuriko mabaya kabisa kuwahi kutokea katika historia ya nchi hiyo. Vijiji 11,000 vimefurika kutokana na mvua kubwa, ambapo pia mafuriko hayo yameharibu zaidi ya nyumba milioni moja, mamilioni ya hekta na kuwaathiri zaidi ya watu milioni 16.

Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula-WFP, Amjad Jamal amesema kuwa wanafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa wanagawa chakula kwa waathirika wa mafuriko hayo ambao wanaishi katika kambi za muda na wale wanaoishi katika maeneo ya wazi, ingawa bado kuna mamilioni ya watu wengine ambao wanapata msaada kidogo wa chakula au hata kutopata kabisa chakula. Jamal amesema maeneo mengi bado hayafikiki kutokana na kuharibika kwa barabara na kuvunjika kwa madaraja na zaidi ya watu 800,000 bado wamekwama. Kwa mujibu wa msemaji huyo wa WFP, wamefanikiwa kuzifikia wilaya za Kohistan na Shangla kaskazini-magharibi mwa jimbo la Khyber-Pakhtunkhwa, kiasi wiki mbili baada ya maeneo hayo kukumbwa na mafuriko.

Jamal anasema kuwa watu sasa wanaishiwa vyakula vyao vya akiba na shirika lake bado halijafanikiwa kugawa chakula kinachohitajika na waathirika hao wa mafuriko. Viongozi nchini Pakistan na wafanyakazi wa mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa wanatumia helikopta na nyumbu kwa ajili ya kusafirisha chakula kwenye wilaya ya Kohistan iliyopo maeneo ya milimani. Leo Umoja wa Mataifa umetoa ombi la kupatiwa helikopta 40 zaidi kwa ajili ya kubeba chakula cha maelfu ya watu ambao bado wamekwama.

Aidha, Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa magonjwa miongoni mwa maelfu ya watu walioathiriwa na marufiko hayo. Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa misaada ya kibinaadamu nchini Pakistan-OCHA, Maurizo Giuliano, amesema kuwa kiasi watu milioni 1.5 walioathirika na mafuriko hayo wanapatiwa matibabu ya magonjwa ya kuhara, magonjwa ya ngozi na matatizo mengine. Giuliano ameongeza kusema kuwa idadi ya watu walioathiriwa na mafuriko hayo imefikia milioni 16.68, ambapo milioni tano kati yao hawana makaazi.

Marufiko hayo yameanza kupungua katika eneo la kaskazini na kati mwa Pakistan, lakini Mto Indus uliofurika bado unaliathiri jimbo la Sindh lililopo eneo la kusini mwa nchi hiyo ambako vijiji kadhaa vimezingirwa na maji kwa kipindi cha zaidi ya saa 24. Khair Mohammad Kalor, mkurugenzi wa operesheni wa idara ya majanga katika jimbo la Sindh, amesema kuwa zaidi ya watu 200,000 wameondolewa kutoka eneo la Thatta na wilaya mbili za karibu na kwamba wataendelea na zoezi hilo pindi itakapohitajika kufanya hivyo. Mtabiri mkuu wa hali ya hewa nchini Pakistan amesema kuwa hali ya mafuriko itaendelea kwa siku mbili au tatu zijazo.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Pakistan, Shah Mehmood Qureshi, amesema hadi sasa jumuiya ya kimataifa imeshatoa zaidi ya dola milioni 815 kama msaada wa dharura. Hata hivyo, Umoja wa Mataifa umesema umepokea asilimia 70 ya dola milioni 460 ambazo iliomba mwanzoni mwa mwezi huu. Nalo Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF, leo linatarajiwa kufanya mazungumzo na maafisa wa Pakistan mjini Washington, Marekani kuangalia jinsi shirika hilo linavyoweza kuisadia nchi hiyo kukabiliana na uchumi wake uliovurugika kutokana na mafuriko hayo. Wakati huo huo, watu 20 wameuawa nchini Pakistan baada ya mtu mmoja kujiripua katika msikiti katika wilaya ya Waziristan Kusini. Mauaji hayo yamefanyika wakati nchi hiyo ikiendelea kukabiliana na mafuriko mabaya kuwahi kutokea nchini humo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE/AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 23.08.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OuBo
 • Tarehe 23.08.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OuBo
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com