Viongozi wa vyama vya siasa nchini Zimbabwe, wawasili Afrika kusini kwa mazungumzo. | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa vyama vya siasa nchini Zimbabwe, wawasili Afrika kusini kwa mazungumzo.

Viongozi wa vyama vya siasa nchini Zimbabwe, wamewasili Afrika kusini kwa ajili ya mazungumzo na wakuu wa nchi za eneo la kusini mwa Afrika, wakati ambao mkutano wa Jumuia ya nchi za SADC, unafanyika mwishoni mwa wiki.

default

Msuluhishi wa mzozo wa Zimbabwe, Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini na Rais Mugabe.

Mkutano wa Jumuia ya nchi hizo za SADC, unafanyika mwishoni mwa wiki hii, na kuzungumzia mzozo wa Kisiasa nchini Zimbabwe pia.

Msemaji wa Chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change -MDC-, George Sibotshiwe amesema kiongozi wa chama hicho, Morgan Tsvangirai leo atakutana na viongozi wa nchi tatu za Jumuia ya Maendeleo kusini mwa Afrika, ambao wanafuatilia kwa karibu mzozo wa Zimbabwe, ambazo inajumuisha Afrika kusini, nchi ambayo inasuluhisha mzozo wa Zimbabwe kwa kusimamia mazungumzo ya sasa ya kugawana madaraka kati ya Rais Robert Mugabe na upinzani.

Jana serikali ya Zimbabwe kwa muda ilizuia nyaraka za kusafiria za kiongozi wa chama cha MDC, Morgan Tsvangirai, hali iliyosababisha kushinda kwenda Afrika kusini kama ilivyopangwa siku hiyo ya jana.

Msemaji wa MDC, George Sibotshiwe amesema Tsvangirai na maafisa wengine wawili waandamizi wa chama hicho walitarajiwa kuwasili Afrika kusini leo asubuhi.

Kwa upande wake, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe anatarajiwa kuwasili Afrika kusini leo pia, kuhudhuria mkutano huo wa SADC.

Kiongozi wa ujumbe wa chama tawala nchini Zimbabwe, cha ZANU PF, katika mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mzozo wa kisiasa nchini humo, Patrick Chinamasa amethibitisha Rais Mugabe kuwasili leo nchini humo kwa ajili ya mazungumzo hayo.

Aidha amesisitiza kuwa mazungumzo ya kugawana madaraka nchini humo hayajavunjika na vyama vyote vimejidhatiti katika mazungumzo na kuongeza kuwa chama chake kinawajibu mkubwa wa kuona mazungumzo hayo yanafanikiwa haraka iwezekanavyo.

Katika hatua nyingine, msuluhishi wa mzozo wa kisiasa nchini Zimbabwe, Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini, alisema ana matumaini kwamba pande hizo mbili zinazopingana kisiasa nchini humo zitafikia suluhisho katika kugawana madaraka nchini Zimbabwe.

Chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU PF, na upinzani vitaendelea na mazungumzo yao ya kugawana madaraka mwishoni kwa wiki hii wakati wa mkutano wa Jumuia ya nchi za SADC.

Mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mzozo wa Zimbabwe yalianza mwezi uliopita baada ya Rais Robert Mugabe kufanya duru ya pili ya uchaguzi wa Rais, bila ya mpinzani, kufuatia mpinzani wake Morgan Tvangirai kususia uchaguzi huo, ulioshutumiwa na jumuia ya kimataifa, kutokana na madai ya kushambuliwa kwa wafuasia wake.

Mazungumzo hayo yataendelea tena baada ya kushindwa kuafikiana katika siku tatu za mazungumzo, yaliyofanyika Harare wiki hii.


 • Tarehe 15.08.2008
 • Mwandishi Nyanza, Halima
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Exq6
 • Tarehe 15.08.2008
 • Mwandishi Nyanza, Halima
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Exq6
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com