Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakutana baadae hii leo mjini Brussels | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakutana baadae hii leo mjini Brussels

Ajenda kuu ya mkutano wao wa kilele ni kuhakikisha uwezo wao wa kuumaliza mgogoro usiokwisha wa deni la Ugiriki, na kuepusha balaa la mgogoro huo kuenea katika zoni ya Euro.

default

Viongozi wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wao december mwaka jana mjini Brussels

Hakuna maajabu yoyote yanayotazamiwa kutokea wala uamuzi mpya utakaopitishwa wakati wa mkutano huo wa siku mbili utakaoanza leo usiku mjini Brussels. Labda mawaziri wa fedha watakapokutana kama ilivyopangwa July tatu ijayo.

Katika wakati ambapo umoja wa sarafu ya Ulaya unazongwa na migogoro, viongozi wa taifa na serikali wa nchi 27 za Umoja wa Ulaya wanapanga kuthibitisha utayarifu wao wa kuipatia Ugiriki msaada ziada katika awamu ya kwanza ya mpango wa kuiokoa nchi hiyo ulioanzishwa mwaka mmoja uliopita, kwa sharti kama wiki ijayo bunge la Ugiriki litaidhinisha mpango wa kufunga mkaja uliokubaliwa baada ya majadiliano pamoja na wafadhili wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia wa nchi za Ulaya, viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa Ulaya watabidi "watoe dhamana inayotakiwa na shirika la fedha la kimataifa" ili Ugiriki iweze kupatiwa fedha taslimu ifikapo mwezi ujao wa July.

Demonstrationen vor dem griechischen Parlament

Wagiriki waandamana kupinga hatua za kufunga mikaja

Kitisho cha kufilisika Ugiriki hakiwashughulishi peke yao viongozi wa Umoja wa Ulaya. Ni kitisho kinachoushughulisha ulimwengu mzima-amesema hayo John Lipsky, ambae ni mwenyekiti wa muda wa shirika la fedha la kimataifa, IMF na kuendelea

"Mnauliza kama mambo yatakwenda kombo. Sisi tunajitahidi kuona na kuhakikisha mambo yanapita vizuri."

Mbali na mgogoro wa Ugiriki, mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya unatazamiwa kuidhinisha hatua kadhaa zilizolengwa kuhifadhi sarafu ya Euro dhidi ya migogoro.

NATO-Angriff auf Libyen

Madege ya NATO yapiga katika eneo wanakoishi raia mjini Tripoli

Kesho itakuwa zamu ya kuzungumzia suala la Libya katika wakati ambapo lawama zinazidi kusikika dhidi ya kuendelea opereshini za jumuia ya kujihami ya NATO nchini humo na pia mzozo wa Syria.

Viongozi wa taifa na serikali watazungumzia pia kuhusu wahamiaji. Suala la kufanyiwa marekebisho mkataba wa Schengen litazingatiwa, na hivyo kurahisisha uwezekano wa kuendelezwa ukaguzi wa mpakani, ikilazimika.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp,Reuters

Mhariri:Miraji Othman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com