Viongozi wa Ulaya wampongeza Ursula von Der Leyen | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa Ulaya wampongeza Ursula von Der Leyen

Salamu za pongezi zimemininika kutoka kila kona zaidi barani Ulaya kumsifu Ursula von Der Leyen kwa kuchaguliwa kwake usiku wa kuamkia leo Jumatano kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekuwa miongoni mwa mfululizo wa viongozi wa Ulaya waliompongeza Bi Von der Leyen kwa kuchaguliwa kwake, akisema anaamini mwanasiasa huyo kutoka Ujerumani atakabiliana na changamoto za umoja huo kwa ujasiri mkubwa.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Bi. Merkel imemnukuu Kansela huyo akisema ingawa amepoteza moja ya mawaziri wa muda mrefu na wa kutumainiwa katika serikali yake, bado anajiona mshindi kwa sababu Von der Leyen anakuwa mshirika mpya kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels.

Salamu za pongezi zimetolewa muda mfupi baada ya Bunge la Umoja wa Ulaya kumuidhinisha Von der Leyen kuwa rais ajaye wa halmashauri kuu ya Umoja huo kwa ushindi mwembamba wa kura 383 dhidi ya 327 ya waliompinga.

Muda mfupi baada ya kura ya kumuidhinisha, Von der Leyen mwenyewe alisema "Nimepata ahueni na nina furaha kwa sababu ushindi ulikuwa mwembamba. Nilikuwa na siku 13 pekee kuwashawishi wabunge hapa katika bunge la Ulaya. Na bila shaka walihitaji kufahamu mimi ni nani, ninawaza nini na mpango wangu ni upi. Na kutimiza hilo ndani ya siku 13 ilikuwa kama mbio ndefu lakini ilistahili kuwa hivyo."

Von der Leyen kuchukua mikoba ya Junker mwezi Novemba

Von der Leyen ambaye leo anawachia wadhifa waziri wa ulinzi wa Ujerumani atamrithi Jean-Claude Junker mapema mwezi Novemba kuongoza halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, ambacho ni chombo muhimu cha ngazi ya juu cha muungano huo.

Junker aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter kwamba wadhifa wa rais wa halmashauri kuu ni nafasi yenye wajibu mzito na kuelezea imani yake kwamba Von der leyen  anayekuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo atakuwa kiongozi wa aina yake.

Chini ya wadhifa huo Von der Leyen atakuwa na jukumu la mstari wa mbele la kuweka malengo ya kisiasa ya Umoja wa Ulaya katika kipindi cha miaka mitano ijayo, huko akisimamia zaidi ya wafanyakazi 32,000 wa umoja huo.

NATO yaelezea imani yake kwa Von der Leyen

Kwenye salamu zake za pongezi, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nato, Jens Stoltenberg amesifu ujuzi alionao Von der Leyen kuhusu taasisi ya NATO akiongeza kwamba hilo litasaidia pakubwa kwenye kuimarisha ushirikiano katia ya Ulaya na mataifa ya Amerika Kaskazini.

Serikali za Ugiriki, Austria na Ubelgiji ni miongoni mwa zile zilizoukaribisha ushindi wa Von der Leyen zikisema zinalenga kushirikiana kwa karibu na taasisi za Umoja wa Ulaya wakati wakuu wa mataifa ya eneo la Baltiki wameahidi kushirikiana kwa karibu na rais mpya wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya ili kuifanya ulaya kuwa imara na yeyne mshikamano.

Wabunge kutoka chama mshirika na Kansela Merkel cha Social Democratic, SPD hawakuunga mkono uteuzi wa Von der Leyen lakini hata hivyo naibu wa kansela Olaf Scholz kutoka chama cha SPD amekuwa sehemu ya waliompongeza Von der Leyen kwa ushindi alioupata jana mjini Brussels.

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com