Von der Leyen kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Von der Leyen kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Ursula Von der Leyen ameahidi kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, kuongeza makamishna zaidi wanawake katika Umoja wa Ulaya na kurefusha muda wa Uingereza kujiondoa katika umoja huo.

Akizungumza katika hotuba yake ya mwisho katika Bunge la Ulaya, kabla ya kura inayofanyika baadae leo, Von der Leyen ambaye anawania kuchaguliwa kuwa rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, amesema changamoto kubwa inayowakabili ni kuifanya dunia kuwa salama na yenye afya.

''Nitapendekeza sheria kuhusu mazingira ndani ya siku zangu 100 za kwanza ofisini, ili kuifanya Ulaya kuwa bara la kwanza duniani lenye hali ya hewa ya kawaida ifikapo mwaka 2050,'' alisisitiza waziri huyo wa Ujerumani anayetafuta kuungwa mkono na wabunge wa Umoja wa Ulaya ili kupata wadhifa huo.

Von der Leyen anayetoka katika chama cha Christian Democratic kutoka kundi la chama cha European People's Party, ameahidi kwamba atatoa kipaumbele katika masuala ya mazingira na ya kijamii katika mpango wake wa miaka mitano ijayo, wakati akitarajia kupata kura 374 katika bunge la Ulaya lenye wabunge 747.

Makundi matatu makuu ndani ya bunge hilo yanatarajiwa kumuunga mkono mwanasiasa huyo wa Ujerumani, lakini wanasiasa wanaotetea mazingira na wale wanaofuata siasa kali za mrengo wa kushoto hawatomuunga mkono.

EU-Gipfel in Brüssel | Jean-Claude Juncker, Kommissionspräsident (Getty Images/T. Monasse)

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker

Ama kwa upande mwingine, Von der Leyen anayetarajiwa kurithi mikoba ya Jean-Claude Juncker, amesema ataongeza muda mwingine wa mwisho kwa Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya, maarufu kama Brexit, iwapo Uingereza itataka muda zaidi ili kuhakikisha inajiondoa kwa utaratibu mzuri kwenye umoja huo.

Uingereza inapaswa kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya ifikapo Oktoba 31, mwaka huu, muda ambao umecheleweshwa kwa nusu mwaka kutoka katika muda wake wa awali. Boris Johnson anayepigiwa chapuo kumrithi Theresa May kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, amesema anataka kuondoka kwenye umoja huo Oktoba 31 kwa makubaliano au hata bila makubaliano.

Wakati huo huo, Von der Leyen ameahidi kuwateua makamishna wa Umoja wa Ulaya kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na kuchukua hatua kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake. Tangu Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ilipoanzishwa mwaka 1958, makamishna 35 kati ya 183 ndiyo wamekuwa wanawake.

Waziri huyo wa ulinzi wa Ujerumani ambaye amesema kesho Jumatano atajiuzulu wadhifa huo hata kama asipochagulia kushika nafasi hiyo ya juu ya Umoja wa Ulaya, amefafanua kuwa wanawake wanaiwakilisha nusu ya idadi ya watu duniani, hivyo wanataka mgawanyo sawa. Amesema iwapo wataondoa tofauti kati yao, watakuwa na umoja wenye nguvu.

 

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com