1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Utengenezaji silaha za nyuklia waongezeka duniani

Dotto Bulendu
27 Machi 2026

Wakati ulimwengu ukishuhudia kuongezeka kwa mizozo na mapigano kati ya mataifa yenye nguvu duniani, ripoti mpya imeonesha uwepo wa ongezeko la utengenezaji wa silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/5BHAV
Mazoezi ya roketi yakifanyika huko Rawalpindi, Pakistan
Mazoezi ya roketi yakifanyika huko Rawalpindi, PakistanPicha: AR-ZM-200121/Newscom World/IMAGO

Hali hii inazidisha wasiwasi juu ya usalama pamoja na kukiukwa mkataba wa kupinga uzalishaji wa silaha za nyukila.

Kwa  mujibu wa ripoti ya kila mwaka ya marufuku ya matumizi wa silaha za nyuklia,takriban nchi zote tisa zenye silaha za nyuklia Urusi, Marekani, China, Ufaransa, Uingereza, Pakistan, India, Israel na Korea Kaskazini zimeongeza akiba zao au zimetangaza mipango ya kuongeza uzalishaji wa silaha hizo.

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akitumia darubini kutazama mazoezi ya kijeshi
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akitumia darubini kutazama mazoezi ya kijeshiPicha: DW

Sawa na mabomu yaliyoshambulia Hiroshima

Ripoti hiyo iliyochapishwa na shirika la wanasayansi wa Marekani,wa Marekani, FAS pamoja na shirika la waokozi wa kujitolea la nchini Norway (NPA), inakadiria kuwa idadi ya silaha za nyuklia zilizo tayari kutumika ilifikia 9,745 mwaka uliopita idadi hiyo ikiwa ni ongezeko la mabomu 141 ikilinganishwa na mwaka 2024.

Uchambuzi wa waandishi wa ripoti hii unaonesha idadi hiyo ni sawa na nguvu ya mabomu 135,000 yaliyoshambulia mji wa Hiroshima, ambapo bomu moja  lilisababisha vifo vya watu 140,000 mnamo mwaka 1945

Takwimu za ripoti hiyo zinaonesha kuwa asilimia 40 kati ya mabomu 4,012 yalipachikwa kwenye makombora ya balistiki yaliyowekwa katika hifadhi za ardhini au kwenye manowari na katika vituo vya kufyatua mabomu vinavyohamishika mwaka uliopita, ambapo kwa mujibu wa ripoti hiyo hilo ni ongezeko la mabomu ya nyuklia 108 kulinganisha na mwaka 2024.

Ripoti hiyo imebaini kuwa nchi zenye silaha za nyuklia zilirundika jumla ya mabomu 12,187 mwanzoni mwa mwaka huu, ikilinganishwa na mabomu zaidi ya 70,000 yaliyokusanywa katikati ya miaka ya 80.

Kituo cha kutengeneza madini ya urani Iran
Kituo cha kutengeneza madini ya urani IranPicha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Matumizi yanaongezeka kila mwaka

Kudhoofika kwa mfumo wa muda mrefu wa kupunguza silaha, kuzuia uenezaji wake, na udhibiti wa silaha, ikiwemo kumalizika mwezi uliopita kwa mkataba wa New START kati ya Urusi na Marekani nchi zenye nguvu kubwa za nyuklia, ni sababu inayochangia ongezeko hilo la uzalishaji wa silaha za nyuklia.

Hans Kristensen, mkurugenzi wa Mradi wa Taarifa za Nyuklia katika Shirika la Wanasayansi wa Marekani (FAS) amesema matumizi ya silaha za nyuklia yanayoongezeka kila mwaka ongezeko la kila mwaka ni jambo la kutia wasiwasi na ameonya kwamba kasi hiyo inaongeza pia wasiwasi wa kushindwa kudhibiti ongezeko hilo pamoja kutokea hatua za matumizi ya silaha hizo japo kwa bahati mbaya na amesisitiza kwamba yote hayo yanaifanya dunia kuwa mahala hatari zaidi kwetu sote.