USHAWISHI MPYA WA UTURUKI MASHARIKI YA KATI | Magazetini | DW | 14.09.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

USHAWISHI MPYA WA UTURUKI MASHARIKI YA KATI

Mzozo wa fedha barani Ulaya, ripoti ya OECD kuhusu viwango vya elimu Ujerumani na Uturuki inayoibuka kama taifa lenye ushawishi katika Mashariki ya Kati, ni baadhi ya mada katika magazeti ya Ujerumani leo Jumatano.

Gazeti la HANNOVERSCHE ALLGEMEINE ZEITUNG likiandika juu ya ripoti ya hivi karibuni ya shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo-OECD- juu ya viwango vya elimu nchini Ujerumani, linaeleza hivi:

"Hakuna yeyote yule atakayebisha kuwa viwango vya elimu nchini Ujerumani bado ni dhaifu. Lakini ripoti kama hizo, haziwasaidii wanafunzi wanaozidi kushinikizwa kwa viwango vya kimataifa. Sera ya elimu hivi sasa inakabiliwa na changamoto kali: kutimiza malengo ya mfumo wa elimu na wakati huo huo kutowaweka wanafunzi katika hali ya kushinikizwa. Kwa hivyo, hapo tarakimu za OECD hazitosaidia."

SÄCHSISCSHE ZEITUNG likiendelea na mada hiyo hiyo linasema:

"Nchi zingine zinatoa nafasi nyingi zaidi za kusoma, maprofessa zaidi na hata huduma bora katika sekta ya elimu. Katika nchi nyingi zilizoendelea kiviwanda, elimu ya juu ni mada inayopewa kipaumbele na hugharimiwa ipasavyo. Lakini Ujerumani, tangu miaka kadhaa, kila jimbo lina mfumo wake wa elimu na hujiamulia gharama za walimu na wanafunzi kama litakavyo. Katika hali kama hiyo, hatimae, katika taifa lililo maarufu kwa wasanii na wasomi wake, watu kama hao watakuwa adimu."

Lakini gazeti la NEUE PRESSE linsema: "Ujerumani,tangu muda mrefu sio tena taifa la watu walio na vipaji. Hakuna nchi yo yote iliyoendelea kiviwanda inayowekeza kiwango kidogo kabisa cha pato la jumla la taifa katika sekta ya elimu, kama Ujerumani inavyofanya. Vile vile, kuna tatizo jingine la kijamii. Mara nyingi, ni vigumu sana kwa mwanafunzi anaetoka familia masikini kuendelea na masomo mpaka chuo kikuu."

Sasa tunaugeukia mzozo wa fedha unaowaumiza vichwa viongozi wanaohangaika kutafuta ufumbuzi. Gazeti la EMDER ZEITUNG linaandika:

"Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekanusha uvumi unaohusika juu ya uwezekano wa Ugiriki kufilisika. Hadharani matamshi yake hayakupokewa vizuri, kwani ni dhahiri kuwa Ugiriki bado haikuchukua hatua za kutosha kupunguza madeni yake. Kawaida hapo hatua ingepaswa kuchukuliwa dhidi ya Ugiriki. Lakini, kuna hatari ya mzozo huo kuathiri kanda nzima ya Umoja wa Ulaya na sio nchi zinazotumia sarafu ya Euro pekee."

Mada nyingine iliyogonga vichwa vya habari katika magazeti ya leo nchini Ujerumani inahusika na Uturuki na jinsi inavyoibuka kama taifa linalozidi kuwa na ushawishi katika Mashariki ya Kati. NEUE OSNABRÜCKER ZEITUNG linasema:

"Wanasiasa wa Ulaya ambao tangu miaka kadhaa, wamekuwa wakiiwekea vizuizi Uturuki inayotaka kujiunga na Umoja wa Ulaya, wala hawakudhania kile wanachokishuhudia hivi sasa. Kwani ionekanavyo, imekua kheri kwa Uturuki kukataliwa uanachama. Baada ya kuvunjika moyo Uturuki imeanza kugeukia nchi zingine. Na ionekanavyo, sasa ina nafasi nzuri ya kuwa na dhima ya uongozi katika eneo la Mashariki ya Kati linalopitia enzi ya mageuzi."

Mwandishi: Martin,Prema/dpa

Mhariri: Charo, Josephat