1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yadhibiti karibu asilimia ishirini ya ardhi ya Ukraine

Saleh Mwanamilongo
2 Juni 2022

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameonya katika kile alichokiita "nyakati za giza kumfikia kila mtu barani Ulaya" iwapo Urusi itashinda katika vita vyake nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4CD54
Internationale Filmfestspiele von Cannes 2022 | Videoansprache
Picha: Christophe Simon/AFP/Getty Images

Akilihutubia bunge la Luxembourg kwa njia ya video hii leo, rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, amesema iwapo Kyiv itashinda vita hivyo dhidi ya Urusi, raia wote wa Ulaya wataendelea kufurahia uhuru wao.

Zelensky ameeleza kuwa Urusi sasa inadhibiti takriban asilimia ishirini ya ardhi ya Ukraine hii ikiwa ni zaidi ya upana wa Ubelgiji, Luxembourg na Uholanzi zikiwekwa pamoja.

''Hadi leo, karibu asilimia 20 ya eneo letu liko chini ya udhibiti wa wavamizi, karibu kilomita 125,000. Upana huu ni mkubwa zaidi kuliko eneo la nchi zote za Benelux kwa pamoja. Takriban kilomita za mraba 300,000 zimechafuliwa na mabomu ya kutegwa ardhini na vifaa visivyolipuka. Takriban raia wa Urkaine milioni 12 wamekuwa wakimbizi wa ndani. Zaidi ya watu milioni 5, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wamekimbilia nje ya nchi.", alisema Zelensky.

Zelensky ameomba uungwaji mkono zaidi wa dunia, na kuongeza kuwa maelfu ya watu wamekufa katika siku 99 za kwanza za vita. Wakati huo huo Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema ni kwa maslahi ya kimkakati ya Umoja huo lakini pia wajibu wao wa kimaadili kufanya kila linalowezekana kwa Ukraine kujiunga na umoja huo.

Soma pia →Urusi yatangaza kudungua ndege ya kivita ya Ukraine

Urusi yazionya nchi za Magharibi

Putin kukutana na mwenye kiti wa Umoja wa Afrika
Putin kukutana na mwenye kiti wa Umoja wa AfrikaPicha: Mikhail Metzel/Sputnik/AP/picture alliance

Urusi imekosoa tena mipango ya nchi za Magharibi ya kutuma silaha zaidi kwa Ukraine. Msemaji wa ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, amewaambia waandishi wa habari kwamba upelekaji wa silaha utaleta zaidi mateso kwa Ukraine, ambayo ni chombo tu katika mikono nchi zinazoipatia silaha.

Uingereza imesema itaipa Ukraine roketi za masafa ya kati ya mifumo ya kisasa ya silaha. Ahadi hiyo imekuja siku moja baada ya Marekani na Ujerumani kusema zitatuma silaha za kisasa kwa Ukraine za kudungua ndege na kuripua vifaru.

Kwa upande wake serikali ya Sweden inataka kuisaidia Ukraine na misaada ya kiuchumi na vifaa vya kijeshi huku kukiwa na kile kilichoelezwa kuwa ni awamu mpya ya uvamizi wa Urusi.

Soma pia→Ukraine: Urusi inadhibiti asiliamia 70 ya Severodonetsk

Upatanishi wa Umoja wa Afrika ?

Hayo yamejiri wakati Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika ambaye pia ni Rais wa Senegal Macky Sall, anasafiri kuelekea Urusi kujadili mzozo wa chakula uliosababishwa na vita nchini Ukraine. Lengo la ziara hiyo ni kuachiliwa kwa maghala ya nafaka na mbolea ambazo kwa sasa vimezuiwa kwenye bandari za Ukraine. Nchi za Afrika zimeathirika pakubwa na ongezeko la bei la bidhaa muhimu lililosababishwa na vita.