1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi: Shambulio la ndege ya Syria ni ‘uchokozi’

Jane Nyingi
19 Juni 2017

Urusi imeitaka Marekani kuheshimu uhuru na mipaka ya Syria baada ya kuangusha ndege ya jeshi la Syria katika mkoa wa Raqqa. Ndege hiyo  ilikuwa katika harakati za kushambulia kundi linalojjita dola kiislamu IS.

https://p.dw.com/p/2evOd
Russland Treffen von Lavrov, Javad Zarif  und Muallem in Moskau
Picha: Reuters/S. Karpukhin

Akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa maswala  ya kigeni mjini Beijing nchini China,waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema shambulizi hilo na Marekani dhidi ya ndege ya jeshi la Syria  huenda likazidisha mzozo nchini Syria na pia kuhatarisha vita dhidi ya ugaidi. Kisa hicho  kimetokea  wakati ambapo majeshi ya Syria yameimarisha mashambulizi yake dhidi ya wapiganaji wa IS kusini na magharibi mwa  Raqqa, huku nalo jeshi la waasi wa Syria lijulikanlo kama Syria Democratic forces linaloungwa mkono na Marekani likiendeleza  vita  dhidi ya kundi kundi hilo  la IS ndani ya mji wa Raqqa,ambao ndio ngome ya wapiganaji hao wa IS. Katika taarifa Marekani imesema ilichukua hatua za kujilinda baada ya majeshi hayo ya Syria kuangusha mabomu karibu na  eneo linalosimamiwa na jeshi la waasi la Syria Democratic forces. Marekani pia iliweka wazi kuwa haiyalengi majeshi ya Syria au Urusi, na iwapo  muungano wa vikosi vyake utahitajika kufanya mashambulizi ya kujilinda basi havitasita kuchukua hatua.

Syrien Demokratische Kräfte Syriens bei Raqqa
Waasi wa jeshi la Syrian Democratic Forces wakipiga doria mji wa RaqqaPicha: picture-alliance/AP Photo/Syrian Democratic Forces

Marekani inaunga mkono magaidi

Hata hivyo kamanda wa jeshi la Syria amelitaja shambulizi hilo dhidi ya ndege ya Syria kama ushahidi wa jukumu la Marekani katika kuunga mkono wapiganaji wa IS.Jeshi la Syria  limeonya kutokea madhara makubwa kufuatia shambulizi hilo, na kusisitiza  kuwa vitendo kama hivyo  havitalizuia kuendelea na  harakati zake za kupiga vita makundi ya kigaidi na kurejesha amani na usalama  kwa wa Syria wote.Saa chache kabla ya kuangushwa kwa ndege hiyo ya jeshi ya Syria, Marekani ilisema kuwa vikosi vinavyomuunga mkono rais wa Syria Bashar al-Assad viliwashambulia wanajeshi wa jeshi la  waasi la Syria Democratic forces  na baadhi yao kujeruhiwa. Mapema mwezi huu, Marekani iliangusha ndege isiyo na rubani ya serikali ya Syria, baada ya ndege hiyo kushambulia vikosi karibu na kivuko cha mpaka cha al-Tanf kwenye mpaka kati ya Syria na Iraq.Taarifa nyingine ni kuwa jeshi la Ukombozi  la Iran limetoa onyo kali dhidi ya wapiganaji wa IS,na kusema mashambulizi yeyote dhidi ya Iran yatailazimisha kutumia nguvu zaidi.Tangazo hilo lilitolewa baada ya jeshi hilo la Iran  kurusha makombora yaliyolenga kundi hilo la IS mashariki mwa Syria. 
Mwandishi:Jane Nyingi/AP/AFP
Mhariri:Josephat Charo

Syrien Flüchtlinge aus Rakka bei Ain Issa
Wasyria wanaokimbia vita mji wa RaqqaPicha: Reuters/R. Said