1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Ukraine zakubaliana kusitisha mapigano

Saleh Mwanamilongo
9 Machi 2022

Mamlaka nchini Ukraine zinasema kuwa ndege za kijeshi za Urusi zimefanya mashambulizi mapya kwenye makaazi ya raia katika sehemu za kati na mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/48CqC
Kyiv yajitayarisha kwa mashambulizi zaidi ya Urusi
Kyiv yajitayarisha kwa mashambulizi zaidi ya UrusiPicha: Andrew Marienko/AP/picture alliance

Maafisa wa Ukraine wanasema katika mji wa Malyn ulio kwenye jimbo la Zhytomyr, magharibi mwa mji mkuu Kyiv, watu watano, wakiwemo watoto wawili, wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Urusi. Makombora mengine yametuwa kwenye viunga vya Kyiv, huku maji, chakula na umeme ukikatwa, kwa mujibu wa Yaroslav Moskalenko, anayeratibu huduma za kiutu kwenye jimbo la Kyiv.

Rais wa Ukraine Volodimyr Zelensky amesema misaada ya kiutu itaendelea kutolewa kwa raia:

''Leo tumefanikiwa kuandaa njia ya misaada ya kibinadamu kutoka Sumy hadi Poltava. Mamia ya watu wanaokolewa, misaada ya kibinadamu inatolewa, lakini hii ni asilimia chache tu ya kile tunachopaswa kufanya na kile kinachotarajiwa na watu wetu, ambao wamekwama.''

Dmytro Shyvytskyy mkuu wa mkoa wa Sumy amesema zoezi la uokoaji wa raia kutoka mji wa Sumy hadi mji wa Poltava,katikati mwa Ukraine litaendelea leo Jumatano. Amesema timu ya mazungumzo imekuwa ikifanya kazi usiku kucha. Na zoezi la uokoaji lilipaswa kuanza saa tatu asubuhi. Kulingana na Shyvytsky, watu wanaweza kuondoka mjini kwa magari yao wenyewe. Pia kutakuwa na mabasi 22 inapatikana. Amesema operesheni hiyo inafanyika kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu.

Marekani yakataa pendekezo la Poland kutuma ndege za kijeshi Ukraine

Raia wa Ukraine waendelea kukimbia mashambulizi ya Urusi
Raia wa Ukraine waendelea kukimbia mashambulizi ya UrusiPicha: Ukrainian Presidency/AA/picture alliance

Naibu waziri Mkuu wa Ukraine,Iryna Vereshchuk amesema leo kwamba Moscow iliapa kuheshimu mapatano hayo ya usitishwaji mapigano kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa tatu usiku, karibu na maeneo sita ambayo yameathiriwa pakubwa na mapigano, ikiwa ni pamoja na mikoa karibu na Kyiv, huko Zaporizhzhia kusini, na baadhi ya maeneo ya kaskazini mashariki mwa Ukraine.

Rais Zelensky amewashukuru viongozi wa Marekani na Uingereza kwa kupiga marufuku mafuta ya Urusi kuingia kwenye nchi zao. Zelensky ameiita marufuku hiyo kuwa ni ishara kubwa kwa ulimwengu mzima, akisema sasa Urusi itapaswa kuheshimu sheria za kimataifa na kuacha kuanzisha vita ama ikose fedha.

Maafisa wa Poland leo wamesema utoaji wowote wa ndege za kivita kwa Ukraine lazima ufanyike kupitia Jumuiya ya NATO, kauli hiyo imefuatia Marekani kukataa hapo jana pendekezo la kushangaza la Poland kwamba ingeliipa Marekani ndege zake za kijeshi kwa ajili ya kutumiwa na Ukraine.