Urusi na nchi za magharibi zazozana kuhusu misaada kwa Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.07.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Urusi na nchi za magharibi zazozana kuhusu misaada kwa Syria

Urusi na mataifa ya Magharibi wanazozana juu ya suala la kuendelea kutuma misaada ya kiutu nchini Syria hasa katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi.

Mzozo huo wa suala la kupeleka misaada kaskazini magharibi mwa Syria, umejiri baada ya idhini ya uwasilishaji huo wa misaada ya Umoja wa Mataifa kumalizika muda wake Ijumaa.

Mnamo Alhamisi, Ujerumani na Ubelgiji ziliitisha kura juu ya rasimu ya azimio ambalo litaruhusu kuendelea kwa miezi sita kutuma misaada kupitia vituo viwili vya mpakani kutoka Uturuki kwenda kaskazini magharibi mwa Syria.

Azimio hilo linaungwa mkono na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengi yanayotoa misaada ya kibinadamu. Matokeo ya kura hiyo yanatarajiwa kutangazwa baadaye leo.

Azimio jipya la Urusi

Bila ya kusubri matokeo hayo kutolewa, mnamo Alhamisi usiku, Urusi ilianza kusambaza azimio jipya la kutafuta idhini ya kuruhusiwa kusafirisha misaada kupitia eneo moja tu la mpakani kwa mwaka.

Mamia ya wahamiaji kutoka Syria wamekimbilia Iraq kufuatia machafuko nchini Syria (Picha ya maktaba)

Mamia ya wahamiaji kutoka Syria wamekimbilia Iraq kufuatia machafuko nchini Syria. (Picha ya maktaba)

Kupitia mfululizo wa ujumbe wa Twitter, naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Dmitry Polyansky alitangaza azimio hilo jipya la Urusi, na kuzisisitiza nchi za Magharibi kuliunga mkono, huku akiashiria kuwa Urusi itapinga rasimu ya azimio iliyowasilishwa na Ujerumani na Ubelgiji kupitia kura ya turufu.

Urusi ambayo ni mshirika wa karibu wa Syria, imekuwa ikisema kwamba misaada inapaswa kusambazwa kupitia njia za ndani ya Syria zenye mapigano.

Lakini Umoja wa Mataifa na makundi ya kutoa misaada ya kibinadamu wamekuwa wakisema kuwa misaada kwa ajili ya watu wenye shida wapatao milioni 2.8 haiwezi kusambazwa kwa namna hiyo.

Azimio la Ujerumani na Ubelgiji

Magari ya shirika la Hilal Nyekundu yaliyobeba vyakula vya misaada yakiwa katika kituo cha al-Wafideen nje ya viunga vya Damascus karibu na eneo la waasi. Machi 5.2018

Magari ya shirika la Hilal Nyekundu yaliyobeba vyakula vya misaada yakiwa katika kituo cha al-Wafideen nje ya viunga vya Damascus karibu na eneo la waasi. Machi 5.2018

Azimio la Ujerumani na Ubelgiji linalopigiwa kura linatafuta idhini ya kurefusha muda wa kutuma misaada kupitia maeneo mawili ya mpakani kutoka Uturuki kwenda Bab al-Salam na Bab al-Hawa kwa miezi sita.

Rasimu ya azimio la Urusi litaruhusu kupitisha misaada kwenye kituo cha mpakani cha Bab al-Hawa, kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Balozi wa Ujerumani kwa Umoja wa Mataifa, Christoph Heusgen, amesema Jumatano kwamba wakati kituo cha mpakani cha Bab al-Hawa kinatumika kutuma misaada katika mkoa wa idlib, kituo cha mpakani cha Bab al-Sham kinafikisha misaada hadi eneo la kaskazini mwa Aleppo, ambako kuna raia wa Syria wapatao 300,000 waliopoteza makazi yao kutokana na mashambulizi.

Azimio la awali lililowasilishwa na Ujerumani na Ubelgiji kuidhinisha kusambazwa misaada nchini Syria kupitia vituo viwili vya mpakani kwa mwaka mmoja lilipata uugwaji mkono kutoka kwa wajumbe 13 kati ya 15 wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumanne iliyopita, lilipigwa na Urusi pamoja na Uchina.