1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi na Belarus zaanza luteka ya pamoja ya kijeshi

Admin.WagnerD10 Februari 2022

Urusi na Belarus zimeanza luteka ya pamoja ya kijeshi ambayo imechochea mvutano zaidi na mataifa ya Magharibi huku juhudi za kidiplomasia kuepusha uwezekano unaohofiwa wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraine zikiendelezwa.

https://p.dw.com/p/46nMT
Militärübung zwischen Russland und Weißrussland
Picha: Belarus Defense Ministruy/AA/picture alliance

 

Viongozi katika mataifa ya Magharibi wamekuwa wakionya kuwa Urusi inajiandaa kuzidisha mzozo huo kwa kuwapeleka wanajeshi laki moja katika mpaka na Ukraine. Marekani ilikuwa imesema Urusi pia inapeleka wanajeshi elfu 30 katika taifa jirani la Ukraine, Belarus kwa mazoezi hayo ambayo yameanza Alhamisi (10.02.2022).

Urusi bado haijafichua idadi ya wanajeshi wanaoshiriki katika mazoezi hayo ya kijeshi lakini wizara ya ulinzi ya nchi hiyo imethibitisha kuwa luteka hiyo tayari imeanza. Katika taarifa, wizara hiyo imeendelea kusema kuwa lengo la mazoezi hayo ni kufanya mazoezi ya kukandamiza na kuzuwia uchokozi wa nje kwa operesheni ya kujihami na kwamba mazoezi hayo yatazingatia kukabiliana na ugaidi na kulinda maslahi ya mataifa hayo mawili ikimaanisha muungano unaozileta pamoja Urusi na Belarus katika ushirikiano wa kijeshi na kiuchumi.

Ikulu ya Urusi imesisitiza kuwa vikosi hivyo vya kijeshi vitarejea nchini humo baada ya zoezi hilo.

Ukraine Kiew | Pressekonferenz Wolodymyr Selenskyj
Volodymyr Zelensky - Rais wa UkrainePicha: Ukrainian Presidential Press Office/AP/picture alliance

Huku hayo yakijiri, rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ametaja luteka hiyo ya pamoja ya kijeshi kuwa shinikizo la kisaikolojia. Haya ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa ofisi yake. Ukraine pia imeanzisha mazoezi yake ya kijeshi yanayotarajiwa kufanana na yale yalioanzishwa na Belarus na Urusi. Lakini maafisa wa kijeshi nchini humo, hawajatoa habari zaidi kuyahusu kutokana na hofu ya kuzidisha mvutano.

Ufaransa pia imelaani luteka hiyo ya pamoja ya kijeshi ya Urusi na Belarus na kuitaja kuwa ishara ya vurugu mbali na kuongezeka kwa wanajeshi wa Urusi katika mpaka na Ukraine. Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amekiambia kituo cha redio cha France Inter radio kwamba mazoezi hayo ya siku 10 ni makubwa mno na yanawahusu.

Wakati huo huo, waziri mkuu mpya wa Ujerumani Olaf Scholz ambaye amekuwa chini ya shtuma kali kutokana na hatua za kutatanisha kuhusiana na mzozo huo wa Ukraine na Urusi, atasafiri kuelekea katika mataifa hayo mawili wiki ijayo kwa mikutano tofauti na viongozi wa mataifa hayo ikiwa ni pamoja na mkutano wa kwanza wa ana kwa ana na rais wa Urusi Vladmir Putin. Scholz  pia anatarajiwa kukutana na viongozi wa eneo la Baltic mjini Berlin  siku ya Alhamisi  huku waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson akitarajiwa kukutana na maafisa wakuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO kabla ya kusafiri kuelekea Poland kukutana na rais wa nchi hiyo Andrzej Duda.