1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yataka uchaguzi huru na wa haki Myanmar

28 Septemba 2010

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amesema uchaguzi unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini Myanmar hautakuwa huru, mpaka pale utawala wa kijeshi wa nchi hiyo utakapowaachia wafungwa wote wa kisiasa.

https://p.dw.com/p/PODc
Katibu Mkuu wa UN Ban Ki-moonPicha: AP

Ban Ki-moon alisema hayo kwa niaba ya kundi la nchi zinazojuliknana kama marafiki wa Myanmar, baada ya kikao cha mawaziri wa nchi hizo mjini New York, Marekani.

Kundi hilo linajumuisha nchi jirani na Myanmar zikiwemo, China, India, Indonessia, Thailand na Singapore. Pia Marekani na mataifa mengine ya Ulaya yapo katika kundi hilo.

Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema, kuna umuhimu kwa mchakato wa uchaguzi huo kuwashirikisha watu wote na kuwa wa uwazi. Amesema wanachama wa kundi hilo wametaka hatua zichukuliwe za kuachiwa kwa wafungwa wote wa kisiasa akiwemo kiongozi wa upinzani nchini humo Aung San Suu Kyi.

Ameongeza kuwa jambo hilo ni muhimu katika kuufanya uchaguzi huo uonekane huru na wa haki na pia katika kuchangia maendeleo na uimara wa Myanmar. Katika kikao hicho cha kundi la marafiki wa Myanmar kilichofanyika pembezoni mwa kikao cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa, hakuna mwakilishi kutoka serikali ya Myanmar aliyehudhuria.

Hata hivyo mapema Ban Ki-moon alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Myanmar U Nyan Win katika makao makuu ya umoja huo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika mazungumzo yake na waziri huyo alisisitiza haja ya kuachiwa kwa Bibi Aung San Suu Kyi ambaye ametumikia takriban kipindi cha miongo miwili iliyopita katika kifungo cha nyumbani.

Utawala wa kijeshi wa Myanmar umekipiga marufuku chama cha San Suu Kyi pamoja na vyama vingine vinane kushiriki katika uchaguzi huo utakaofanyika tarehe 7 mwezi ujao, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miongo miwili iliyopita. Hata hivyo utawala huo wa kijeshi umesema Bibi San Suu Kyi ataruhusiwa kupiga kura.

Marekani na Umoja wa Ulaya, zimeiwekea vikwazo Myanmar. China lakini imekuwa ikiusaidia utawala huo wa kijeshi wa Myanmar kukabiliana na vikwazo vya Umoja wa Mataifa. India kwa upande wake ilimkaribisha kiongozi wa nchi hiyo, Than Shwe, kufanya ziara ya kiserikali nchini India Julai mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa katika kipindi hiki cha mpito huko Myanmar ni muhimu kwa kundi hilo la nchi marafiki wa Myanmar hususan zile zilizo jirani nayo, kushirikiana na ofisi yake kusaidia hali nchini humo.

Pia ametoa wito kwa jumuiya ya mataifa ya kusini mashariki mwa Asia ASEAN ambayo Myanmar pia ni mwanachama wake, kuchukua hatua mujarab kwa utawala wa kijeshi wa Myanmar kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki.

Ban Ki-moon pamoja na Waziri wa Nje wa Marekani Hillary Clinton wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo ya ASEAN utakaofanyika wiki ijayo huko Hanoi Vietnam, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa Myanmar

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya haki za binadamu, ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kubaini iwapo vitendo vilivyofanywa na utawala wa kijeshi wa Myanmar dhidi ya wafuasi wa upinzani, ni mateso yanayoweza kuufanya utawala huo kufunguliwa mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu. Ban Ki-moon hata hivyo amesema hatua yoyote ya kuchukuliwa italazimika kuamuliwa na wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP

Mhariri:Josephat Charo