UN kukabiliana na udhalilishaji wa kingono | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.03.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

UN kukabiliana na udhalilishaji wa kingono

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limedhinisha azimio lake la kwanza kabisaa siku ya Ijumaa, kukabaliana na tatizo linaloongezeka na udhalilishaji wa kingono na wanajeshi wa kulinda amani katika maeneo ya migogoro.

Umoja wa Mataifa umemulikwa kwa miezi kadhaa kuhusiana na madai ya kuwabaka watoto na na ukiukaji mwingine wa kingono unaofanywa na wanajeshi wake w akulinda amani, hasa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati na DRC. Umoja wa Mataifa unasema kulikuwa na madai 69 ya udhalilishaji wa kingono na dhuluma nyingine dhidi ya walinda amani mwaka 2015, na visa vingine 25 zaidi kwa mwaka huu wa 2016.

Azimio hilo liliidhinishwa kwa kura 14 kwa 0, huku Misri ikijizuwia baada ya kushindwa kwa marekebisho ya dakika za mwisho iliyoyapendekeza, ambayo yangedhoofisha maandishi ya muswada wake. Muswada huo ulioandaliwa na Marekani unaidhinisha mpango wa mageuzi wa Katibu Mkuu Ban Ki-Moon, ikiwemo uamuzi wa kuvirejesha vikosi vya kijeshi au polisi, "pale inapobainika kuna ushahidi wa ukiukaji mkubwa na udhalilishaji wa kingono."

Pia linamtaka Katibu Mkuu Ban kubadili vikosi pale ambapo madai hayajachunguzwa vizuri, wakosaji hawajawajibishwa ipasavyo, au iwapo katibu mkuu hajafahamishwa kuhusu maendeleo ya uchunguzi. Marekebisho yaliokuwa yamependekezwa na Misri, yangetaka masharti yote matatu yatimizwe kabla ya kikosi cha jeshi au polisi kurejeshwa nyumbani, na siyo moja wapo kama inavyotakiwa sasa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.

Ujumbe mzito kwa mataifa husika

Marekani, ambayo ndiyo mchangiaji mkubwa zaidi wa kifedha kwa operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, ilisema ilitaka chombo hicho chenye nguvu zaidi cha Umoja wa Mataifa kutuma ujumbe mzito kwamba hakitavumilia tatizo hilo linalozidi kukuwa.

"Kwa waathirika wa dhuluma za kingono na ukiukaji unaofanywa na walinda amani, tunaahidi kwamba tutafanya zaidi," alisema Samantha Power, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa. "Tutafanya kazi nzuri zaidi kuhakikisha kwamba wanajeshi wa kulinda amani tunaowatuma kama walinzi wenu hawageuki kuwa wahalifu."

Zaidi ya wanajeshi 100,000 na polisi wanashirki katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, wengi wao kutoka katika mataifa yanayoendelea. Umoja wa Mataifa unayarudishia pesa za mshahara mataifa yanayotoa wanajeshi na pia kutoa posho za wanajeshi wanaolinda amani.

Kama sehemu ya mageuzi ya Katibu Mkuu, Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza umeanza kuyataja mataifa wanakotokea wanajeshi wanaodaiwa kushiriki vitendo vya udhalilishaji wa kingono, hatua inayonuwia kuongeza shinikizo kwa mataifa kufuatilia madai ambayo, taarifa za Umoja wa Mataifa zinaonyesha yamekwenda bila kuchunguzwa.

Ban pia aliahidi kuharakisha uchunguzi na kuweka wazi taarifa kuhusu madai yanayoendelea kwenye tovuti mpya ya Umoja wa Mataifa.

Misri, Urusi na mataifa kadhaa menngine yalihoji kwamba azimio hilo la baraza lingewaadhibu maelfu ya walinda amani kutokana na matendo ya wachache. Wanasema suala hilo linapaswa kushughulikiwa na Hadhira Kuu ya Umoja wa Mataifa. Lakini maamuzi ya Hadhira Kuu hayana nguvu ya kisheria, wakati maazimio ya baraza la usalama yanayo nguvu hiyo.

Balozi wa Misri katika Umoja wa Mataifa Amr Abdellatif Aboulatta alisema "kuyataja na kuyaaibisha mataifa mazima" ni jambo lisilokubalika kabisaa na "linaathiri morali ya wanajeshi." Alisema ingekuwa bora zaidi iwapo baraza la usalama lingejikita kwenye mizizi ya uhalifu wa kingono, ikiwemo kutoa mafunzo na usimamizi kwenye makambi ya walinda amani.

Wanajeshi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC - MONUSCO.

Wanajeshi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC - MONUSCO.

"Tunataka mageuzi makubwa zaidi UN"

Moja ya madai 25 ya mwaka huu ni dhidi ya mwanajeshi wa kulinda amani wa Misri nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mamlaka za Misri zinachunguza kisa hicho, kulingana na mtandao wa Umoja wa Mataifa. Urusi na China zilunga mkono marekebisho yaliyopendekezwa na Misri, lakini zilipiga kura kuunga mkono azimio hilo.

Naibu balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Petr iliichev alisema hakiuwa sahihi kwa baraza kukataa marekebisho ya Misri ambayo yaliakisi mtazamo wa mataifa yanayochangia wanajeshi. Lakini alisema Urusi iliamua kuunga mkono azimio kwa sababu maandishi ya mwisho yalipanuliwa kuhusisha majeshi yote yaliyotuma na baraza la usalama - akimaanisha wanajeshi wa Ufaransa wanaotuhumiwa kuwadhalilisha kingono watoto katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, na wanajeshi wa Umoja wa Afrika nchini Somalia, Darfur na kwingineko.

"Leo imepigwa hatua muhimu kuelekea njia sahihi," alisema Mkurugenzi wa Uitikiaji wa migogoro wa shirika la haki za binaadamu la Amnesty International Tirana, Tirana Hassan. "Lakini bado tunahitaji mageuzi makubwa kwenye mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape

Mhariri: Caro Robi

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com