Umoja wa Afrika wajiandaa kuingia Nzuwani | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.03.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Afrika wajiandaa kuingia Nzuwani

Mtawala wa Nzuwani Mohammed Bacar apinga juhudi zote za upatanishi za umoja wa Afrika

default

Fukwe za Komoro jua linapokuchwa


 Mkuu wa ofisi ya ushirikiano kati ya Umoja wa Afrika na visiwa vya Komoro Murad Taiati anasema "ufumbuzi wa kijeshi ndio njia pekee iliyosalia kuufumbua mzozo uliosababishwa na kanali Mohammed Bakar kisiwani Nzuwani."Hakuna chochote kinachomfanya mtu aamini kwamba ufumbuzi mwengine ambao si wa kijeshi unawezekana" amesema hayo bwana Mourad Taiati wakati wa mahojiano pamoja na shirika la habari la Ufaransa AFP.


Juhudi za upatanishi za Ujumbe wa Umoja wa Afrika zilizoangaliwa kama fursa ya mwisho ya kung'oka madarakani kwa amani watawala wa kisiwa kinachoasi cha Nzuwani zimekataliwa na kanali Mohammed Bacar wiki iliyopita.Alishauriwa na Umoja wa Afrika akubali kuitisha uchaguzi mwengine wa rais ambapo yeye binafsi anaruhusiwa kutetea,au akubali kwenda kuishi nchini Ufaransa ikiwa nchi jirani zitaridhia.


 Mkuu wa ofisi ya mawasiliano ya Umoja wa Afrika Mourad Taiati amesema kanali Mohammed Bacar ameyakataa mapendekezo yote hayo  na kudai hataki kujadiliana na Umoja wa Afrika.

Umoja wa Afrika unashughulikia mzozo wa kisiwa cha Nzuwani tangu ulipoanza miaka zaidi ya kumi iliyopita.


Umoja wa Afrika unapanga kuitisha mkutano maalum March nane ijayo mjini Daresalam kuzungumzia maandalizi ya mwisho kabla ya opereshini ya kijeshi kukikomboa kisiwa cha Nzuwani.


Nchi nne za Umoja wa Afrika,Tanzania,Senegal,Sudan na Libya zimeahidi kuchangia wanajeshi  kwaajili hiyo.


Ufaransa imeahidi kuchangia ndege itakayowasafirisha wanajeshi 200 wa Tanzania walioppelekwa visiwani Komoro tangu kati kati ya mwaka jana kufuatia maombi ya Umoja wa Afrika.


Mourad Taiati amezungumzia pia ripoti zinazozidi kumiminika kuhusu kuvunjwa haki za binaadam kisiwani Nzuwani.Maelfu ya wanzuwani wameyapa kisogo maskani yao na kukimbilia katika visiwa vya Ngazija na Mwali.


Kwa mujibu wa serikali kuu ya Komoro wanzuwani elfu mbili na mia tano kati ya wakaazi laki mbili na nusu wa kisiwa hicho wamekimbilia Ngazija.


"Maelfu wanakimbia madhila na mateso wanayofanyiwa na utawala haramu wa Bakar-"Amesema bwana Mourad Taiati.


Wahanga wa mateso ya watawala wa Nzuwani wamelazwa katika hospitali kuu ya  El Maarouf mjini Moroni na wanaelezea visa vya kikatili walivyotendewa na askari kanzu wa kanali Mohammed Bakar.

 Mpinzani mkubwa wa mtawala huyo wa Nzuwani Mohammed Djaafar anazungumzia juu ya mamia ya watu waliokamatwa kinyume na sheria na kutiwa ndani na kuteswa au hata kunajisiwa tangu Umoja wa afrika ulipoamua kuingilia kati kijeshi kisiwani Nzuwani.


Mwanaharakati mmoja wa shirika linalopigania haki za binaadam ambae hakutaka jina lake litajwe amethibitisha na wao pia wanapokea ushahidi wa watu wanaoadhibiwa na kunajisiwa kisiwani Nzuwani.


Kisiwa cha Nzuwani kimeanza kuasi tangu mwaka 1997 viongozi wa wakati ule wa kisiwa hicho walipotangaza kutaka kurejea kua chini ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa,kabla ya kujiunga upya na visiwa vyengine vya Komoro mwishoni mwa mwaka 2001 kufuatia juhudi za upatanishi za umoja wa Afrika. • Tarehe 05.03.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DIrs
 • Tarehe 05.03.2008
 • Mwandishi Hamidou, Oumilkher
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DIrs
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com