Umoja Mataifa wakumbuka miaka mitano ya kuripuliwa makao yake Baghdad | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja Mataifa wakumbuka miaka mitano ya kuripuliwa makao yake Baghdad

Umoja wa Mataifa leo hii utakuwa na kumbukumbu ya miaka mitano ya kuripuliwa kwa ofisi yake mjini Baghdad ambapo wafanyakazi wake 22 waliuwawa akiwemo mjumbe mwandamizi wa Umoja wa Mataifa Sergio Viera de Mello.

Hali ya usalama Iraq bado ni ya mashaka.Pichani ni mripuko uliotokea nje ya Hoteli ya Baghdad

Hali ya usalama Iraq bado ni ya mashaka.Pichani ni mripuko uliotokea nje ya Hoteli ya Baghdad

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon atakatiza mapumziko yake ya wiki mbili ili kuhudhuria kumbukumbu hiyo ambayo itatowa heshima kwa wahanga kwa kusoma majina yao na kukaa kimya kwa dakika moja.

Uwekaji wa shada la mauwa pia utafanyika kwenye ukuta wa kumbukumbu katika ukumbi wa jengo la Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Kutakuwepo na muziki wa dakika 15 uliotungwa na mtunzi wa Marekan Steve Heitzeg unaoitwa Wimbo bila ya Mipaka kuwakumbuka wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliofariki wakiwa kazini.

Tokea mwaka 1948 wakati chombo hicho cha dunia kilipoanzisha shughuli zake za kwanza za kulinda amani huko Mashariki ya Kati wanajeshi wa kulinda amani 709 wameuwawa wakiwa kazini kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Uripuaji wa kujitolea muhanga ambao umelenga makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Baghdad hapo tarehe 19 mwezi wa Augusti mwaka 2003 ulimuuwa Viera de Mello wa Brazil balozi mahiri wa Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wengine 21.Watu wengine 150 walijeruhiwa.

Mara tu baada ya mripuko huo Umoja wa Mataifa ulijiondowa nchini Iraq.

Mripuko huo wa Baghdad umezusha wasi wasi mkubwa juu ya uwezo wa Umoja wa Mataifa kuwalinda wafanyakazi wake wanaotumika katika shughuli za kulinda amani kwenye maeneo ya mizozo duniani kote.

Mwezi wa Desemba mwaka jana mirupuko miwili ya kujitolea muhanga iliolenga ofisi za Umoja wa Mataifa imeuwa watu 18 nchini Algeria watatu wakiwa ni raia wa kigeni.

Mashambulizi hayo yamedaiwa kufanywa na tawi la mtandao wa Al Qaeda la Osama bin Laden.

Katika kukabaliana na hali hiyo wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walidai uchunguzi huru juu ya kuwepo kwa usalama wa kutosha katika vituo vya Umoja wa Mataifa duniani kote.

Ban baadae aliunda jopo la watu sita lililoongozwa na mjumbe mwandamizi wa Umoja wa Mataifa Lakhdar Brahimi kufanya uchunguzi huo.

Mwezi wa Juni uliopita jopo hilo la Brahimi limetowa repoti ambayo inasema kuna ushahidi wa kutosha kwamba wafanyakazi kadhaa wa Umoja wa Mataifa kuanzia ngazi ya juu hadi ya chini ya mamlaka hiyo yumkini wakawa wameshindwa kutowa habari ipasavyo kwa mashambuliuzi ya Algiers kabla na baada ya maafa hayo.

Ugunduzi huo umepelekea kujiuzulu kwa Mkuu wa usalama wa Umoja wa Mataifa Sir David Veness.

Repoti hiyo pia imesema kwamba kulengwa mahsusi kwa Umoja wa Mataifa kunakofanywa na makundi ya kigaidi kunawakilisha mabadiliko ya mwenendo miongoni mwa vitisho vinavyokabili chombo hicho cha dunia hivi sasa na kipindi cha usoni.

Hapo tarehe 7 mwezi wa Augusti Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kwa kauli moja kuongeza muda wa mamlaka ya wanajeshi wake wa kulinda amani 767 nchini Iraq UNAMI na kuelezea kuwa tayari kwake kuangalia upya mamlaka ya kikosi hicho katika kipindi cha miezi 12 au hata mapema zaidi iwapo itaombwa na serikali yas Iraq.

 • Tarehe 18.08.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F0OO
 • Tarehe 18.08.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/F0OO
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com