1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Ukraine | Krieg | Stomausfall nach Raketenangriffen auf Infrastuktur in Kiew
Picha: Danylo Antoniuk/AA/picture alliance
SiasaUkraine

Umeme warejea kwenye maeneo karibu yote ya Kiev

Grace Kabogo
27 Novemba 2022

Maafisa wa kijeshi katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev wamesema umeme umerejeshwa katika maeneo takribani yote ya mji huo, ikiwa ni siku nne baada ya shambulizi baya la Urusi kuharibu miundombinu yake.

https://p.dw.com/p/4K94h

Taarifa ya maafisa hao wa kijeshi katika mtandao wa kijamii wa Telegram, imeeleza kuwa hadi kufikia Jumapili asubuhi, umeme mwingi, maji, joto na huduma za simu za mkononi zilikuwa zikiendelea kufanya kazi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kazi ya mwisho inaendelea katika gridi ya umeme, lakini mahitaji makubwa huenda yakasababisha kukatika kwa umeme ndani ya jiji hilo.

Meya wa Kiev, Vitali Klitschko ambaye amekosolewa na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky kwa kutofanya juhudi za haraka kurejesha huduma, siku ya Jumapili ameliambia gazeti la Ujerumani la Bild kwamba kazi ilikuwa inaendelesa kwa kasi.

Aidha, theluji kali inatarajiwa kudondoka Kiev kuanzia Jumapili, huku hali ya joto ikishuka chini ya viwango vya baridi mchana na usiku, na mamilioni ya watu ambao bado wanaishi ndani na kuizunguka Kiev bado wakiwa hawana umeme na joto la kutosha.

Ukraine | Krieg | Zerstörung in Borodjanka
Theluji ikiwa imedondoka kwenye mji wa Borodianka, UkrainePicha: Philip Reynaers/BELGA/dpa/picture alliance

Huku hayo yakijiri, mji wa Kryvyi Rih ulioko kusini mwa Ukraine umeshambuliwa kwa makombora ya urusi. Gavana wa kijeshi wa mji huo, Valentyn Resnichenko amesema Jumapili katika mtandao wa Telegram kwamba makombora mawili yameharibu kituo cha miundombinu ya usafiri Jumapili asubuhi. Nyumba kadhaa na majengo mengine yameharibiwa, lakini hapakuwa na vifo wala majeruhi. Hata hivyo, Resnichenko hakutoa ufafanuzi zaidi. 

Uongozi wa kijeshi umewataka wananchi kutafuta makazi kwenye maeneo ambako itakuwa rahisi kusikia taarifa kuhusu mashambulizi ya anga. Tahadhari ya shambulizi la anga ilitolewa kwenye maeneo kadhaa ya mashariki na kusini mwa Ukraine.

Nikopol yashambuliwa

Kwa mujibu wa duru za Ukraine, wilaya ya Nikopol iliyoko kaskazini mwa Mto Dnipro, pia imeshambuliwa kwa makombora. Taarifa ya jeshi imeeleza kuwa usiku wa kuamkia Jumapili, makombora mawili yalishambulia shamba kwenye kitongoji cha kusini mwa mji wa Ukraine wa Zaporizhzhia.

Urusi iliivamia Ukraine, Februari 24 na tayari Urusi imetangaza kuyanyakua majimbo manne ya mashariki na kusini mwa Ukraine na kuwa sehemu ya eneo la Urusi.

Polisi ya Ukraine ilisema siku ya Jumamosi kwamba watu wapatao 32 wameuawa kwa mashambulizi ya Urusi kwenye jimbo la Kherson lililoko kusini mwa Ukraine, tangu vikosi vinavyoiunga mkono Urusi vilipoondoka kwenye jimbo hilo wiki mbili zilizopita.

Ukraine | Krieg | Zerstörung in Nikopol
Jengo likiwa limeharibiwa kwa shambulizi kwenye mji wa NikopolPicha: Evgeniy Maloletka/AP Photo/picture alliance

Aidha, siku ya Jumamosi Rais Zelensky alikuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele mjini Kiev Pamoja na mataifa washirika kwa ajili ya kuanzisha mpango wa kusafirisha nafaka yenye thamani yad ola milioni 150 kwenda kwenye nchi zinazokabiliwa zaidi na ukame na njaa.

Zelensky alisema bei ya mafuta yanayochimbwa baharini ya Urusi, inapaswa kupunguzwa kati ya dola 30 na 40 kwa pipa moja, ikiwa ni chini ya kiwango kilichopendekezwa na kundi la mataifa saba yaliyoendelea kicuhumi duniani ya G7.

Kiongozi wa EPP aitaka Ulaya kuwapokea wakimbizi wa Ukraine

Wakati huo huo, kiongozi wa chama cha European People’s, EPP katika Bunge la Ulaya Manfred Weber, ametoa wito kwa Ulaya kuongeza mshikamano katika kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi wa Ukraine.

"Iwapo watu zaidi wa Ukraine wanalazimika kuyakimbia makaazi yao wakati wa msimu wa baridi kwa sababu ya mashambulizi ya Urusi,, basi Ulaya Magharibi inapaswa kuwajibika zaidi," Weber aliliambia gazeti la Ujerumani la Bild am Sonntag.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa ka kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, takribani watu milioni 7.9 kutoka Ukraine hadi sasa wametafuta hifadhi nje ya nchi, kwa sababu ya vita vinavyoendelea nchini humo. 

Westbalkan Konferenz Sicherheit und Migration Berlin
Kamishna wa masuala ya ndani wa Umoja wa Ulaya, Ylva JohanssonPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Kati yao, zaidi ya milioni moja tu wameandikishwa Ujerumani. Ufaransa imewachukua wakimbizi wapatao 119,000, Italia, 173,000 na Uhispania takribani 154,000. UNHCR imesema idadi hiyo ya wakimbizi kwenye nchi hizo tatu ni ndogo sana. Hadi sasa, Poland imewachukua zaidi ya wakimbizi milioni 1.5.

Kamishna wa masuala ya ndani wa Umoja wa Ulaya, Ylva Johansson ameliambia pia gazeti la Bild am Sonntag kwamba nchi wanachama ambazo bado zina uwezo wa kuwachukua wakimbizi zaidi, zinaongeza juhudi zaidi za kuyasaidia mataifa wanachama ambayo hayawezi tena kuwachukua.

Vita haviidhoofishi Urusi 

Ama kwa upande mwingine, Waziri wa Ulinzi wa Estonia Hanno Pevkur, amesema haamini kwamba Urusi imedhoofika sana hata baada ya miezi tisa ya vita vya Ukraine. "Lazima tuwe wakweli na wazi. 

Jeshi la wanamaji la Urusi na kikosi cha anga cha Urusi ni kubwa kama walivyokuwa kabla ya vita," Pevkur aliliambia shirika la habari la dpa, wakati wa ziara yake mjini Berlin, Ujerumani. 

Pevkur amesema Estonia inapanga kutumia asilimia 2.84 ya pato lake la ndani katika ulinzi kwa mwaka ujao. 

Belgien | PK Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa NATO, Jens StoltenbergPicha: Johanna Geron/REUTERS

Naye Katibu Mkuu wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg ameipongeza Ujerumani kwa kuisaidia Ukraine katika kupinga uvamizi wa Urusi. Matamshi hayo yamechapishwa katika gazeti la Jumapili la Ujeurmani, Die Welt.

Kuisaidia Ukraine kunaleta mabadiliko

"Uungwaji mkono wa Ujerumani unaleta mabadiliko makubwa," alifafanua Stoltenberg. Akizungumza siku mbili kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO utakaofanyika Bucharest, Stoltenberg amesema silaha za Ujerumani zinayaokoa maisha ya watu wa Ukraine.

Ameongeza kusema kuwa wote wanapaswa kuongeza juhudi katika kuisaidia Ukraine. Miongoni mwa silaha ambazo Ujerumani imeipatia Ukraine ni mfumo wa kisasawa kujikinga na makombora wa Iris-T, unaokusudia kuzuia mshambulizi ya makombora ya Urusi. Mengine matatu yatatolewa mwakani. 

Mkuu huyo wa NATO amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa akijibu vikwazo dhidi ya nchi yake kwa kuongeza kufanya ukatili. Alikuwa akizungumzia hatua ya vikosi vya Urusi kuilenga miundombinu ya nishati kabla ya msimu wa baridi. Stoltenberg amesema Putin anajaribu kuyatumia majira ya baridi kama silaha, lakini hatofanikiwa.


(AFP, DPA, AP, Reuters)
 

Ruka sehemu inayofuata Mada zinazohusiana