1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yakumbwa na joto kali huku Uingereza ikivunja rekodi

Zainab Aziz Mhariri: Chilumba Rashid
19 Julai 2022

Joto kali linaloikumba Ulaya ya Magharibi leo Jumanne linatarajiwa kuvunja rekodi ya joto nchini Uingereza, huku maeneo mengine katika bara hilo yakikabiliwa na jua kali linalosababisha kuzuka mioto.

https://p.dw.com/p/4ELNs
Frankreich La Test-de-Buch | Waldbrand
Picha: SDIS 33/AP/picture alliance

Watabiri wa hali ya hewa nchini Uingereza kwa siku kadhaa wamekuwa wakitabiri hali iliyopo sasa katika taifa hilo. Wamesema kiwango cha nyuzi joto 38.7 Celsius kilichoorodheshwa mwaka 2019, kitavunjwa leo hii Jumanne kwani Uingereza itashuhudia kiwango cha nyuzi joto 40 Celcius.

Watu wamejipumzisha ufukweni kulikimbia joto kali nchini Uingereza
Watu wamejipumzisha ufukweni kulikimbia joto kali nchini UingerezaPicha: Christopher Furlong/Getty Images

Hali hii ya joto na kiangazi ambayo inatokea barani Ulaya kuanzia wiki iliyopita sasa imeingia katika eneo la kaskazini, na imetatiza shughuli za usafiri, huduma za afya na hata shule nchini Uingereza. Madaktari wanawahimiza watu kuziangatia ishara za magonjwa yanayohusiana na joto. Daktari Laura McArthur katika chuo kikuu cha Exeter nchini Uingereza ameeleza kuwa ni bora kunywa maji ya kutoshana sio vinywaji vyenye sukari nyingi. Amesema ukiweza, kunywa kinywaji chenye chumvi na sukari ndani yake.

Hali ya joto kali nchini Italia
Hali ya joto kali nchini ItaliaPicha: Manuel Silvestri/REUTERS

Hali ya joto kali pia imetanda katika maeneo ya kusini mwa bara Ulaya tangu wiki iliyopita, huku nchi za Uhispania, Ureno na Ufaransa zikikabiliana na mioto mikubwa inayozuka kutokana na joto kali. Karibu vifo 600 vinavyohusiana na joto kali vimeripotiwa nchini Uhispania na Ureno, ambapo hali ya joto ilifikia kiwango cha nyuzi joto 47 Celcius wiki iliyopita. Maelfu ya watu wamehamishwa kutoka kwenye nyumba zao na kwenye sehemu za kufanyia likizo katika mkoa wa Gironde kusini magharibi mwa Ufaransa tangu majanga ya moto yalipozuka katika misitu ya miti ya misonobari.

Wazima moto kazini katika eneo la Gironde nchini Ufaransa
Wazima moto kazini katika eneo la Gironde nchini UfaransaPicha: SDIS 33/AP/picture alliance

Maafisa wa Shirika la hali ya hewa duniani wanatarajiwa kutoa taarifa juu ya kuongezeka kwa joto barani Ulaya. Shirika hilo awali lilitahadharisha juu ya uharibifu wa ubora wa hewa kutokana na kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira unaohusishwa na hali hii ya viwango vya juu vya joto. Hapa nchini Ujerumani hii leo sehemu nyingi zinatarajia kupata kiwango cha juu cha joto kufikia nyuzi joto 38 Celcius.

vyanzo:AFP/AP