Ukraina na Georgia zakubaliwa uwanachama wa NATO | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ukraina na Georgia zakubaliwa uwanachama wa NATO

Suala muhimu lililozungumziwa leo kwenye mkutano wa jumuiya ya kujihami ya magharibi, NATO ni uwanachama wa nchi nyingine tano: Ukraine, Georgia, Croatia, Albania na Macedonia.

Viongozi wa jumuiya ya NATO waliokutana mjini Bukarest, Romania

Viongozi wa jumuiya ya NATO waliokutana mjini Bukarest, Romania

Kimsingi, nchi zote zimeruhusiwa kujiunga na shirika la NATO, ila tu muda hadi kupewa uwanachama kamili ni tofauti. Kwanza itakuwa zamu ya Croatia na Albania, kama alivyotangaza katibu mkuu wa jumuiya ya NATO, Jaap de Hoop Scheffer: “Wanachama wameamua kuzialika nchi mbili za eneo la Magharibi mwa Balkan kwa mazungumzo kuhusu uwanachama. Kwa niaba ya wote ninasema Hongereni na karibuni katika familia hii.”


Wajumbe wa nchi nyingine ya Balkan, yaani Macedonia, walisikitishwa. Macedonia haikualikwa kujiunga na NATO kwa sababu ya mgogoro juu ya jina la taifa hilo. Ugiriki ambayo pia ni nchi mwanachama wa NATO, inadai Macedonia ni jina la mkoa wake wa Kaskazini na taifa la Macedonia lijiite Jamhuri mpya ya Macedonia. Jina hilo lakini linapingwa na taifa la Macedonia.


Katibu mkuu wa NATO, Bw. De Hoop Scheffer alisifu mageuzi yaliyotekelezwa Macedonia na alisema kulingana na katiba ya nchi na hali yake ya kijeshi, taifa hilo liko tayari kujiunga na NATO. Sasa, juhudi za kutatua mgogoro juu ya jina ambazo hazikufanikiwa huko Bukarest zinatarajiwa zitaongezwa.

Rumänien NATO Gipfel in Bukarest Generalsekretär Jaap de Hoop Scheffer

Katibu mkuu wa NATO, Jaap de Hoop Scheffer

Baada ya mjadala mwingine mrefu na mgumu, Bw. De Hoop Scheffer alikuwa na taarifa nyingine. Alisema: “Shirika la NATO linakaribisha hamu ya Ukraine na Georgia kujiunga na jumuiya hii. Leo tulikubaliana kwamba nchi hizi zitapewa uwanachama wa NATO. Mataifa hayo yote mawili yametoa michango muhimu katika operesheni za jumuiya. Tunapongeza mageuzi katika nchi za Ukraine na Georgia na tutafurahi kuona uchaguzi wa haki na hura unafanyika Georgia mwezi wa Mei.”


Hata hivyo, itachukua muda hadi uwanachama huu kutekelezwa. Ujerumani, Ufaransa na nchi nyingine zilipinga ombi la Marekani ambayo imetaka Ukraine na Georgia zikaribishwe mara moja katika mradi wa kutayarisha uwanachama. Badala yake, mawaziri wa nje wa NATO watachunguza tena hatua hiyo mwezi wa Disemba mwaka huu na halafu wataamua ikiwa nchi hizo mbili zitakaribisha katika mradi huu.


Mradi wa kutayarisha uwanachama ni hatua ya mwisho kabla mazungumzo juu ya uanachama kuanzishwa. Wanasiasa wa Ujerumani walionya kutoikasirisha Urusi kwa kukubali uwanachama wa Ukraine na Goergia. Kansela Angela Merkeli lakini leo alikataa kwamba Urusi ina ushawishi wowote katika uamuzi huu: “Ninaamimi, makubaliano yetu yalionyesha wazi kwamba hakuna tofauti kati ya nchi wanachama wa NATO na kwamba nchi yoyote kama Urusi ina haki ya kuingilia katika suala nani atapewa uanachama. Inabidi lakini tuzingatie hali ya ndani ya nchi hizo, " alisema Kansela Merkel wa Ujerumani.


Urusi, kwa mara nyingine tena, ilionya vikali kutokubali uwanachama wa Ukraine na Georgia katika NATO, nchi hizo zikiwa jamhuri za zamani za Urusi. Naibu waziri wa masuala ya kigeni, Bw. Alexander Grushko, alisema hatua hiyo imekuwa kosa kubwa ambalo litaathiri usalama wa Ulaya kwa ujumla.


Wakati huo huo, shirika la NATO limetoa taarifa kwa pamoja la kuunga mkono mpango wa Marekani wa kuweka mitambo ya kufyatua makombora katika Poland na Jamhuri ya Tchek na kutoa mwito kwa Urusi kutupilia mbali wasiwasi wake wote. Rais Bush anatarajiwa kuwasili kesho mjini Bukarest kama mgeni wa shirika la NATO.

 • Tarehe 03.04.2008
 • Mwandishi Riegert, Bernd / Bukarest
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DbW0
 • Tarehe 03.04.2008
 • Mwandishi Riegert, Bernd / Bukarest
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DbW0
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com