1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukeketaji ni nini na unafanyika wapi?

Caro Robi
6 Februari 2019

Viongozi wa dunia wameahidi kutokomeza ukeketaji ifikapo mwaka 2030, lakini wanaharakati wanasema utamaduni huo hatari na  uliopitwa na wakati bado umekita mizizi katika maeneo mengi.

https://p.dw.com/p/3CpgE
Stephanie Sinclair - Gewinnerin des Anja Niedringhauspreis 2017
Picha: IWMF/Stephanie Sinclair

Tarehe 6 Februari ni siku ya Kimataifa ya kupambana na ukeketaji dhidi ya wasichana na wanawake, lengo likiwa kuangazia juhudi zinazofanywa za kutokomeza desturi hiyo ambayo inawaathiri takriban wasichana na wanawake milioni 200 kote duniani.

Ukeketaji unaaminika ulianza miaka 2,000 iliyopita na unafanywa na makabila na dini mbali mbali duniani.

Kulingana na takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto UNICEF, ukeketaji unafanyika katika mataifa yasiyopungua 30, mengi yakiwa ya Afrika, Mashariki ya Kati na Asia.

Ukeketaji unamaanisha baadhi ya viungo vya sehemu za siri za msichana au mwanamke ama zinakatwa kwa sehemu fulani au zinanyofolewa kabisa. Katika baadhi ya makabila huwa wanashona sehemu hizo au kuzichanja.

Sheria zipo bali ni dhaifu

Ukeketaji unaweza kusababisha matatizo ya muda mrefu ya kiafya na kisaikolojia, ikiwemo maambukizi ya mara kwa mara ya maeneo ya siri, kupata matatizo wakati wa hedhi, kukosa kuzaa na matatizo wakati wa kujifunga.

Bildergalerie Afrika Genitalverstümmelung
Msichana wa jamii ya Pokot-Kenya aliyetoka kukeketwaPicha: Reuters/S. Modola

Somalia inatajwa nchi ambayo karibu asilimia 98 ya wasichana wamekeketwa ikifuatiwa na Guinea, Djibouti, Mali na Sierra Leone. Kati ya nchi 28 za Afrika ambako ukeketaji unafanyika, 22 kati ya hizo zimepitisha sheria za kuharamisha utamaduni huo lakinii sheria hizo zinatajwa kuwa dhaifu na wahusika ni nadra kushitakiwa.

 Nusu ya wasichana wote waliokeketwa au kuishi katika nchi ambazo kuna hatari ya wao kukeketwa wanaishi katika mataifa matatu, Misri, Ethiopia na Nigeria, zote zikiwa na sheria za kupambana na ukeketaji.

Chad, Liberia, Mali, Sierra Leone, Somalia na Sudan ambazo zina idadi ya wasichana milioni 16 hazina sheria za kuzuia ukeketaji. Hata hivyo, Somalia ilitangaza mwaka jana muswada wa sheria wa kupambana na utamaduni huo hatari baada ya msichana wa miaka kumi kufariki baada ya kuketewa.

Kumekuwa na ongezeko la mtindo wa wahudumu wa afya kufanya ukeketaji badala ya mangariba wa kimila hasa Misri, Guinea, Kenya, Nigeria na Sudan. Sababu kubwa inayotolewa ya kuwakeketa wasichana huwa ni kujaribu kudhibiti hamu ya ngono.

Hivi karibuni, Uingereza ilimfunga mtu wa kwanza nchini humo kuhusiana na ukeketaji, miaka 30 baada ya kupitisha sheria ya kupiga marufuku ukeketaji.

Sierra Leone mwezi uliopita ilipiga marufuku ukeketaji lakini kuna mashaka iwapo amri hiyo itaheshimiwa. Huko Liberia marufuku ya mwaka mmoja dhidi ya ukeketaji iliisha mwezi uliopita na wanaharakati wanaendelea kupigania kuwepo sheria madhubuti za kutomokeza desturi hiyo.

 

Mwandishi: Caro Robi/Thomson Reuters

Mhariri: Daniel Gakuba