Ujerumani yajizatiti kusaka malighafi za viwanda vyake | Masuala ya Jamii | DW | 23.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Ujerumani yajizatiti kusaka malighafi za viwanda vyake

Licha ya kwamba Ujerumani ni mtumiaji mkubwa wa malighafi kwa ajili ya uchumi wake wa viwanda na teknolojia ya kiwango cha juu, nchi hii haina rasilimali za kutosha katika ardhi yake.

Malighafi

Malighafi

Mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu, Waziri anayeshughulikia Uchumi kwenye serikali ya Shirikisho la Ujerumani alifungua rasmi wakala wa malighafi mjini Hannover, ambao umepewa jina la Taasisi ya Shirikisho ya Ukuzaji na Uendelezaji wa Malighafi, kwa kifupi BGR. Taasisi hii iko chini ya Wizara ya Uchumi na Teknolojia ya Serikali ya Shirikisho, ambayo yenyewe tayari inatimiza miaka 50.

BGR inaishauri serikali kuu juu ya mambo yote ya mambo yote ya kijilojia, kwa mfano suala la utunzaji na udhibiti wa mionzi ya ununurifu, pamoja na kufanya kazi pamoja na washirika wa kimaendeleo duniani kwenye masuala ya jiolojia. Kwa ufupi, jukumu la BGR ni kuangalia wapi, vipi na kiwango gani cha malighafi kipo na kinaweza kupatikana kwa ajili ya kuendeleza uchumi wa Ujerumani.

Taasisi hii ina jukumu la kukusanya taarifa na kuzichambua kwa ufanisi kabla ya kuziwasilisha kwa wahusika kufanyiwa kazi. Kila malighafi inayoingia Ujerumani lazima ijuilikane imetoka wapi, kwa kiwango gani na kwa matumizi gani, na kama imetumika kuzalisha bidhaa, basi bidhaa hiyo nayo inapaswa kujuilikana kwa undani wake. Wataalamu wa BGR huchambua kila kitu kuhusu bidhaa hiyo, thamani, gharama na faida yake kwenye soko, lakini pia hasara inayoweza kupatikana.

Lakini, jukumu la BGR halipo kwenye uchambuzi wa soko na bidhaa za malighafi tu, bali upo zaidi kwenye kufanya siasa ya kupatikana kwa vyanzo vyengine vya malighafi nje ya mipaka ya Ujerumani. Kwa hivyo, inapotokezea kwamba upatikanaji wa rasilimali husika umehusisha nchi nyengine, basi wataalamu wa BGR hupaswa kulionesha hilo na mahusiano gani ambayo yalipelekea kupatikana kwa rasilimali hiyo.

Ukweli ni kuwa, Ujerumani linaendelea kuwa taifa linalotegemea uchumi wa viwanda na bidhaa zote zinazozalishwa viwandani zinategemea upatikanaji mkubwa wa rasilimali, hasa hasa madini yanayochimbwa ardhini.

Vifaa vya kielektroniki kama simu, kamera, na kompyuta za mkononi, ni miongoni tu mwa bidhaa zinazozalishwa hapa Ujerumani, lakini zinazotumia rasilimali ambazo zinatoka nje ya ardhi ya Ujerumani.

Na ni hili ndilo linalolazimisha kuwepo na chombo kama hiki cha BGR, ambacho kinaangalia pia mahusiano baina ya mataifa mbalimbali linapokuja suala la upatikanaji na utumiaji wa malighafi.

Mwandishi: Sabine Kinkartz/Mohammed Khelef

Mhariri: Othman Miraj

 • Tarehe 23.11.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QGLy
 • Tarehe 23.11.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/QGLy

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com