Ujerumani na Uturuki zaahidi kuujenga upya uhusiano wao | Matukio ya Kisiasa | DW | 29.09.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani na Uturuki zaahidi kuujenga upya uhusiano wao

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan anaendelea na ziara yake Ujerumani inayolenga kupunguza mivutano kati ya nchi hizo. Usiku wa kuamkia leo aliandaliwa chakula cha jioni na Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.

Berlin Staatsbankett für Erdogan (Getty Images/AFP/A. Berry)

Rais Steinmeier na Rais Erdogan

Akizungumza katika chakula hicho cha jioni Rais Steinmeier amekielezea kitendo cha kushikiliwa raia wa Ujerumani nchini Uturuki kama kilichochochewa kisiasa. Amesema akiwa kama kiongozi wa nchi ya Ujerumani, ana wasiwasi kuhusu raia wa nchi hiyo waliofungwa Uturuki kutokana na sababu za kisiasa. Steinmeier alikuwa akiwazungumzia waandishi habari, vyama vya wafanyakazi, wanajeshi, wanasayansi na wataalamu waliofungwa tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi nchini Uturuki mwaka 2016.

Sio kazi ya Uturuki kuwalinda magaidi 

Kwa upande wake Erdogan alihutubia kwa kutumia lugha isiyo ya kidiplomasia baada ya kusema kuwa sio kazi ya Uturuki kuwalinda magaidi. Kiongozi huyo wa Uturuki alisema iwapo waandishi habari wanajihusisha na vitendo vya kigaidi na wamehukumiwa na mahakama ya Uturuki, mtu unawezaje kuendelea kuwatetea? Erdogan amesema bila shaka Ujerumani imepokea taarifa za uongo.

Kabla ya dhifa hiyo ya kitaifa, Erdogan alikutana na Kansela Angela Merkel ambapo kwa pamoja waliapa kuujenga upya uhusiano kati ya Uturuki na Ujerumani baada ya miaka miwili ya mzozo, licha ya kuendelea kuwepo kwa tofauti kuhusu haki za raia na masuala mengine.

Berlin Staatsbesuch Erdogan PK mit Kanzlerin Merkel (Reuters/F. Bensch)

Rais Erdogan na Kansela Merkel

Viongozi hao wawili washirika wa Jumuia ya Kujihami ya NATO, walikubaliana kwa pamoja kuuzungumzia mzozo wa Syria katika mkutano utakaofanyika mwezi ujao pamoja na Rais wa Urusi, Vladmir Putin na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

Lakini mvutano ambao bado upo kati yao ni pamoja na uhuru wa vyombo vya habari, hatma ya Wajerumani au Waturuki wenye uraia wa nchi mbili waliofungwa Uturuki na kuhusu suala la iwapo Ujerumani inapaswa kuwarejesha Uturuki wapinzani wa Erdogan.

Erdogan amesema Ujerumani haifanyi juhudi za kutosha kukabiliana na maelfu ya wapiganaji wa Kikurdi walioko Ujerumani. Hata hivyo, Merkel amesema Ujerumani inakichukulia chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi, PKK kilichopigwa marufuku kama kundi la wapiganaji, lakini haiamini kama Uturuki inapaswa kulichukulia kundi la kiongozi wa kidini anayeishi nchini Marekani, Fethullah Gulen kama la wapiganaji.

Uhusiano na waandishi habari

Wakati wa mkutano wa viongozi hao wawili, mwandishi habari wa Uturuki aliyetambulika kama Adil Yigit, alikuwa amesimama huku amevalia fulana iliyoandikwa ''Waachie Huru Waandishi Habari wa Uturuki'', alitolewa nje haraka na walinzi. Mwandishi huyo anaishi Ujerumani na anaendesha gazeti la mtandaoni la Avrupa Postasi.

Deutschland | Protest T-Shirt auf PK vom Merkel und Erdogan (picture-alliance/dpa/M. Kappeler)

Mwandishi habari wa Uturuki, Adil Yigit

Mwandishi mwingine wa Uturuki anayeishi uhamishoni, Can Dundar alisema ameamua kutohudhuria mkutano wa viongozi hao wawili baada ya kugundua kuwa Erdogan alikuwa akifikiria kuahirisha mkutano na waandishi habari, iwapo angehudhuria. Dundar ni mhariri wa zamani wa gazeti la upinzani nchini Uturuki, Cumhuriyet.

Baadae leo, Erdogan ataufungua msikiti uliopo mjini Cologne ambao umejengwa na jumuiya ya Waislamu wa Uturuki, DITIB. Hata hivyo, maandamano kadhaa yamefanyika kuipinga ziara ya siku tatu ya Erdogan. Polisi wa ziada 4,000 walipelekwa Berlin ili kuimarisha ulinzi wakati wa ziara hiyo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DPA
Mhariri: Gakuba, Daniel

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com