1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani kutowa euro milioni 200 kwa Wapalestina

17 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CcT6

PARIS

Ujerumani imesema itatowa mchango wa euro milioni 200 kusaidia miradi ya maendeleo inayoendeshwa na serikali ya Mamlaka ya Palestina.

Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Ujerumani Heidemarie Wieczozorek-Zeul amesema fedha hizo zinakusudia kuboresha maisha ya shida wanaoishi Wapalestina ambako nako kutasaidia kukomeshaa machafuko ya umwagaji damu huko Mashariki ya Kati.

Tangazo hilo limekuja katika mkesha wa mkutano wa kimataifa wa wafadhili wa Wapalestina unaofanyika mjini Paris Ufaransa leo hii wenye lengo la kusaidia uundaji wa taifa la Wapalestina litakaloweza kujiendesha na kuupa nguvu mchakato wa amani uliozinduliwa upya kati ya Israel na Wapalestina.

Rais wa Wapalestina Mahmoud Abbas anataka kupatiwa dola bilioni 5.6 kwa mpango wa maendeleo wa miaka mitano wenye lengo la kufufuwa uchumi wa Palestina.

Mpango huo unajumuisha kanda ya viwanda katika mji wa Ukingo wa Magharibi wa Jenin itakayojengwa kwa msaada wa Ujerumani.