1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza: Wabunge kupiga kura kuchelewesha tena Brexit

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
3 Septemba 2019

Mjadala mkali utakuwepo kwenye Bunge la Uingereza ambapo Waziri Mkuu Boris Johnson anaushikilia mpango wa kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya bila ya mkataba huku chama kikuu cha upinzani kinauzuia mpango huo.

https://p.dw.com/p/3Ovhj
England, London: Houses of Parliament
Picha: Getty Images/AFP/C. Court

Vyama vya upinzani vimesimama kidete kuupinga mpango wa waziri mkuu Boris Johnson wa kutaka kuiondoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya bila ya mkataba, hapo tarehe 31 mwezi Oktoba. Vyama vya upinzani leo vitawasilisha bungeni ajenda ya kuuzuia mpango wa waziri mkuu Johnson ambaye amewataka wabunge wa chama chake cha Conservative wasiunge mkono ajenda ya wapinzani ya kuizuia Uingereza kuondoka Umoja wa Ulaya bila ya mkataba. Katika tamko alilolitoa, waziri mkuu Johnson amewataka wabunge wa chama chake wauunge mkono mpango wa serikali yake.

Waziri kuu Johnson aliitoa kauli hiyo huku akizomewa na wapinzani wa Brexit pia amesema kuwa hataki  uchaguzi mkuu wa mapema. Lakini pia ameeleza wazi kwamba ikiwa serikali yake itashindwa leo, itawasilisha mswada hapo kesho, juu ya kuidhinisha uchaguzi. Lakini amesisitiza kwamba hataki  uchaguzi. Amesema ni lazima kusonga mbele na ajenda ya umma.

Kiongozi wa upinzani nchini Uingereza Jeremy Corbyn
Kiongozi wa upinzani nchini Uingereza Jeremy CorbynPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Byrne

Kiongozi wa chama cha upinzani Jeremy Corbyn anawataka wabunge wake wapige kura kuunga mkono kufanyika uchaguzi tarehe 14 oktoba na kuambatanisha na hatua ya kuuomba Umoja wa Ulaya kutoa muda zaidi kwa Uingereza.  Bwana Corbyn anafanya juhudi kwa kushirikiana na baadhi ya wabunge waasi wa chama cha Consevertive ili Uingereza iweze kuchelewesha kuondoka Umoja wa Ulaya, kwa muda wa miezi mitatu. 

Kiongozi huyo wa chama cha upinzani amesema ikiwa serikali itashindwa leo, ataitisha uchaguzi. Waziri mkuu Johnson anataka kulitumia suala la Uingereza kujindoa bila ya mkataba kama njia ya kuushinikiza Umoja wa Ulaya ukubaliane na matakwa yake. Hata hivyo Umoja wa Ulaya umesema hakuna uwezekenao  wa kuanzisha mazungumzo mapya juu ya mkataba ambao tayari umeshafikiwa. Mkataba huo ulifikiwa na waziri mkuu wa Uingereza wa hapo awali Theresa May lakini Boris Johnson amesema mkataba huo  haukubaliki. 

Vyanzo: /RTRE7AFP/AP