1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa kibiashara kati ya ulimwengu wakiarabu na Amerika kusini.

6 Aprili 2009
https://p.dw.com/p/HRJ2
Rais al-Bashir wa Sudan pia alihudhuria mkutano huo, licha ya waranti wa kukamatwa uliotolewa na mahakama ya kimataifa ya The Hague .Picha: AP

Viongozi wa mataifa ya Amerika Kusini wamegundua umuhimu wa ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa na ulimwengu wa kiarabu. Hayo yalijitokeza wakati wa mkutano wa kilele wa pande hizo mbili mwanzoni mwa wiki iliyopita katika mji mkuu wa Qatar-Doha, uliofuatia mkutano wa kilele wa jumuiya ya nchi za kiarabu mjini humo.

Ingawa kijografia Amerika kusini na ulimwengu wa kiarabu ziko mbali, lakini pande hizo mbili zinatafuta njia za kuimarisha biashara na uwekezaji.

Mkutano huo ulizingatia mabadiliko ya mtazamo wa nchi za Amerika Kusini, wakati ambapo serikali za siasa za mrego wa shoto wa bawa la kati zikitawala sehemu kubwa ya eneo hilo na kukiwa na hali ya kuipa mgongo Marekani na badala yake kuwa na ushirikiano mpana zaidi na sehemu nyengine za dunia.

Lula da Silva
Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil ni muasisi wa jukwaa hilo.Picha: AP

Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva alisema," Utajiri wa ulimwengu wa kiarabu sasa umegeuka msingi wa maendeleo na hauna budi kulindwa. Matamshi yake yalifuatia hotuba ya ufunguzi wa mkutano iliyotolewa na Amiri wa Qatar Sheikh Hamad bin Kahalifa Al Thani ambaye alisema," Tunahisi kuna mambo mengi yanayofanana kati ya Amerika kusini na ulimwengu wa kiarabu. Sote akaongeza mfalme huyo wa Qatar, "tuna matumaini ya kuwa na mustakbali mwema kwa wakaazi wetu na katika hilo tunakabiliwa na changamoto nyingi."

Ni rais Lula wa Brazil aliyekua wa kwanza kupendekeza fikra hiyo ya mkutano wa kilele kati ya nchi za kiarabu na za Amerika kusini, pale alipokua katika ziara ya Mashariki ya Kati 2003. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo Celso Amorim alisema kwamba kitu kimoja kilichosaidia kutokuwepo na msukosuko mkubwa sana wa kiuchumi nchini Brazil, ni kwa sababu ya kuwa na biashara katika nyanja tafauti. Katika muda wa miaka mitatu hadi minne, biashara ya nchi hiyo na ulimwengu wa kiarabu iliongezeka kutoka dola bilioni 8 hadi bilioni 20.

Maeneo hayo mawili yanawajumuisha wachimbaji wakubwa wa mafuta-Saudi Arabia na Venezuela, na ambazo ni miongoni mwa wasafirishaji wakubwa wa mafuta duniani. Biashara kati ya maeneo hayo mawili imeongezeka mara tatu zaidi tangu mkutano wa kwanza wa kilele uliofanyika Brazil 2003.

Kiongozi wa Venezuela Hugo Chavez amekwenda umbali wa kupendekeza sarafu ya petro "mafuta" kuchukua nafasi ya dola ya Marekani na itakayoungwa mkono na nchi yake na washirika wake wa kiarabu katika jumuiya ya nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi-OPEC.

Chavez alisema" hatimae wakati wa kuanguka himaya ya Marekani sasa umefika."

Maswala yaliyojadiliwa katika mkutano huo wa kilele wa nchi za Amerika Kusini na za kiarabu mjini Doha, yalikua ni pamoja na kukwama mazungumzo ya amani kati ya Israel na wapalestina na waranti wa kimataifa wa kukamatwa kiongozi wa Sudan Omar Hassan al-Bashir kwa tuhuma za uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur. Bila shaka Bw al-Bashir alipata afuweni kumsikia kiongozi wa Venezuela Chavez akipinga hatua hiyo alipouliza kwa nini hawakuamuru kukamatwa rais wa zamani wa Marekani George Bush ?

Lakini baadhi ya viongozi wa Amerika kusini walikata kuonyesha mshikamano na rais wa Sudan, akiwemo rais wa Argentina Cristina Kirchner ambaye alitoka nje ya kikao rasmi kujiepusha kupigwa picha ya pamoja na Rais al-Bashir.

Bibi Kirchner pamoja na hayo alizitaka nchi za kiarabu kuiunga mkono Argentina katika mgogoro wake na Uingereza kudai visiwa vya Falkland ambavyo Argentina inaendelea kuvidai kuwa ni sehemu yake, ikiwa miaka 27 baada ya nchi hizo mbili kupigana vita kuwania visiwa hivyo vilivyoko kusini mwa bahari ya Atlantic.

Mwandishi: M.Abdul-Rahman/IPS

Mhariri: Nyiro,Josephat Charo