1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhispania na Italia zataka msaada zaidi kupambana na corona

Zainab Aziz Mhariri:Rashid Chilumba
29 Machi 2020

Uhispania na Italia zimezitaka nchi nyingine za bara Ulaya kuzisaidia wakati ambapo idadi ya maambukizi ya virusi vya corona ikiendelea kuongezeka katika nchi hizo.

https://p.dw.com/p/3aAr3
Corona Symbolbild Europa Spanien
Picha: Getty Images/J. Soriano

Ufaransa imesema mustakabali wa jumuiya ya Ulaya unategemea jinsi nchi wanachama zinavyopambana na mlipuko wa virusi vya corona hasa baada ya wajumbe wa jumuiya hiyo kushindwa wiki iliyopita kufikia makubaliano juu ya hatua za kuunusuru uchumi uliotetereka kutokana na janga la virusi vya corona.

Umoja wa Ulaya unakabiliwa na mtihani mzito tangu kuzuka na kuendelea kuenea kwa virusi vya corona, mtihani huu unafuatia migogoro ya hivi karibuni iliyoitikisa jumuiya hiyo kama suala la Brexit, mgogoro wa wahamiaji wa 2015-2016 na mgogoro wa madeni katika eneo zima la nchi zinazotumia sarafu ya euro.

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen
Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der LeyenPicha: picture-alliance/dpa/European Commission/E. Ansotte

Waziri wa Ufaransa anayeshughulikia masuala ya Ulaya Amelie de Montchalin amesema uchumi wa nchi kama Ujerumani na Uholanzi hauwezi kuimarika ikiwa nchi nyingine za Ulaya zitabaki nyuma na ameongeza kusema kwamba vyama vya mrengo mkali wa kulia vitaibuka washindi ikiwa viongozi wa Umoja wa Ulaya watashindwa kufanya kazi pamoja wakati huu wa janga kubwa.

De Montchalin ametoa mfano uamuzi wa Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya wa kuwachukua wagonjwa mahututi wa COVID-19 kutoka Ufaransa na amesema hilo ni uthibitisho kwamba mshikamano kati ya nchi wanachama unaendelea.

Kwingineko nchini Marekani mamlaka ya jiji la New York imewataka mamilioni ya wakazi wa jiji hilo linalokabiliwa na hali ngumu ya maambukizi yanayoongezeka kwa kasi kuacha heka heka za kutoka nje au kusafiri kwa ajili ya kuvikabili virusi vya corona

Kwenye sehemu nyingi duniani maafisa wa afya wanakabiliwa na wakati mgumu hasa katika kufanya maamuzi juu ya wagonjwa wanaopaswa kuokolewa huku hospitali nyingi zikiwa zinakabiliwa na uhaba wa mashine za kupulia.

Idadi ya watu waliokufa duniani kote kutokana na ugonjwa wa COVID-19 imepita watu 30,000 kwa mujibu wa chuo kikuu cha John Hopkins.

Maambukizi mapya yanaibuka kila uchao na kuifanya miji kadhaa ya Marekani kuwa ndio kitovu cha maambukizi. Mbali na jiji la New York sasa hali mbaya imeikumba miji ya Detroit, New Orleans na Chicago.

Vyanzo:/RTRE/DW